Tanzania
na Burundi zimekubaliana kuimarisha ushirikiano kwa kusimamia kikamilifu
utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa Sita wa Tume ya
Pamoja ya Kudumu kati ya nchi hizo ulimalizika mkoani Kigoma tarehe 5 Machi
2021.
Makubaliano yaliyofikiwa yamejikita kwenye maeneo kuimarisha sekta za
siasa na mahusiano ya kidiplomasia, ulinzi na usalama, maendeleo ya
miundombinu, ushirikiano katika sekta ya uchumi na kijamii.
Akizungumza
wakati wa Mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amesema kuwa Tanzania imedhamiria
kukuza uchumi wa watu wake kupitia jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi nyingine ikiwemo Burundi.
Ameongeza
kuwa, Tanzania chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imekuwa ikitekeleza
mikakati mbalimbali ya kujenga uchumi na kuinua maisha ya watanzania.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imeendelea kuwekeza
na kuboresha sekta mbalimbali pamoja na kujenga miradi mikubwa ya kimkakati
ukiwemo mradi wa Bwawa la kufua Umeme la Nyerere litakalozalisha Megawati 2,115
na ujenzi wa Reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa
kilomita 1,219.
Alisisitiza
mbali na jitihada hizo, upo umuhimu mkubwa wa Tanzania kushirikiana na nchi nyingine
ikiwemo Burundi ili mafanikio haya yawe na tija zaidi kwa wananchi. “Tanzania
chini ya uongozi wa Mhe. Rais Magufuli imeendelea kuwekeza kwenye miradi ya
kimkakati ili kukuza uchumi wa wananchi wake. itihada hizi haziwezi kufanikiwa
kama Tanzania haitashirikiana na nchi nyingine na kama Tanzania haitawahimiza
wananchi wake kuvuka mipaka na kufanya biashara na wenzao wan chi nyingine. Ni
kwa msingi huo Mkutano huu wa Tume ya Pamoja ya kudumu una umuhimu mkubwa kwa
nchi zetu mbili hususan kuingia makubaliano ya ushirikiano katika sekta
mbalimbali” alisisitiza.
Kadhalika
alisema kuwa maeneo ya ushirikiano yaliyokubalika kwenye mkutano huo ni sehemu
tu ya maeneo mengi muhimu ambayo Tanzania na Burundi zitaendelea kuyaibua kadri
ushirikiano huo unavyoendelea.
“Kuna
maeneo mengi sana ambayo nchi zetu zinaweza kushirikiana, ni dhahiri mpaka sasa
hatujaweza kuzitumia fursa zote zilizopo. Tumeanza na sekta za ulinzi na
usalama; biashara na uwekezaji, uendelezaji wa miundombinu ya uchukuzi
inayounganisha nchi hizi pamoja na masuala ya kijamii na tutaendelea kuvumbua
maeneo mengine mapya ya ushirikiano kadri tunavyoimarisha ushirikiano huu”
alisema Prof. Kabudi.
Prof.
Kabudi alitumia fursa hiyo kuzihimiza sekta zinazohusika na usimamizi wa miradi
ya kikanda ya miundombinu inayotekelezwa
na Serikali za Tanzania na Burundi chini ya uratibu wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki ukiwemo mradi wa ujenzi wa
Barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (260km) na Barabara ya Rumonge-Gitaza
(45km) na ujenzi wa Kituo cha Huduma kwa
Pamoja Mpakani (OSBP) cha Manyovu/Mugina kutekeleza kikamilifu ili kuharakisha
maendeleo ya wananchi wa Tanzania na Burundi.
Pia
alitoa rai kwa watendaji wa Tanzania na Burundi kusimamia kikamilifu utelezaji
wa makubaliano yaliyofikiwa ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ili mikutano ya
tume iwe yenye tija.
Kwa
upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano
wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu, Mhe. Balozi Albert Shingiro alisema nchi
yake imedhamiria kutekeleza makubaliano yote yaliyofikiwa na kutaja mkutano wa
sita kama mwanzo mzuri wa kuendeleza ushirikiano wa kindugu uliopo baina ya
Tanzania na Burundi.
Mkutano
wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi umehitimishwa
kwa kusainiwa kwa Makubaliano ya Ushirikiano kwenye maeneo matano ambayo ni
Ushirikiano wa Kidiplomasia; Ulinzi na Usalama; Uendelezaji Miundombinu ya
Usafirishaji; Elimu na Utamaduni na Biashara na Uwekezaji. Kadhalika Mkutano
huo umeshuhudia kusainiwa kwa Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano kati ya
Chemba za Biashara za Tanzania na Burundi ukiwa na lengo la kuimarisha biashara
baina ya nchi hizi mbili.
Mkutano
wa Sita wa Tume ya Pamoja ambao umefanyika mjini Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5
Machi 2021 umehudhuriwa na Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu
Makatibu Wakuu na viongozi wengine waandamizi kutoka sekta mbalimbali za
Tanzania na Burundi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.