Sunday, June 16, 2024

DKT. MPANGO AMWAKILISHA RAIS SAMIA KWENYE MAZISHI YA KITAIFA YA MAKAMU WA RAIS WA MALAWI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mazishi ya Kitaifa ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Malawi, Hayati Dkt. Saulos Klaus Chilima. Ibada ya Mazishi hayo imefanyika katika Uwanja wa Taifa wa Bingu uliopo Lilongwe nchini Malawi leo Jumapili tarehe 16 Juni 2024.

Akitoa salamu za rambirambi, Dkt. Mpango amesema Tanzania inatoa salamu za pole na kuungana na waombolezaji wote walioguswa na musiba katika kipindi hiki kigumu.

Dkt. Mpango amesema Hayati Dkt. Chilima alikuwa kiongozi imara, mwanamajumui wa kweli wa Afrika ambaye wakati wote alitanguliza mbele masilahi ya wananchi anaowaongoza na Afrika kwa ujumla.

Ametoa wito kwa wananchi wa Malawi na Afrika kwa ujumla kuenzi mambo ambayo Hayati Dkt. Chilima aliyaamini na kiyasimamia. 

Katika safari hiyo Dkt. Mpango ameambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hamza Hassan Juma, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.), pamoja na Balozi wa Tanzania, Mhe. Agnes Richard Kayola.

Hayati Dkt. Chilima alifariki dunia katika ajali ya ndege na watu wengine nane iliyotokea tarehe 10 Juni 2024 kutokana na hali mbaya ya hewa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akitoa heshima kwenye jeneza la mwili wa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Malawi, Hayati Dkt. Saulos Klaus Chilima, katika Ibada ya Mazishi iliyofanyika katika Uwanja wa Taifa wa Bingu jijini Lilongwe, Malawi tarehe 16 Juni 2024.








No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.