Tuesday, January 28, 2014

TANZANIA YACHAGULIWA TENA MJUMBE BARAZA LA AMANI NA USALAMA LA AU

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) ambaye pia anaongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU), mjini Addis Ababa akisikiliza hotuba ya ufunguzi wa Baraza hilo. Wengine katika picha ni Mhe. Naimi Aziz, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Balozi Vincent Kibwana, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Mhe. Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa na Bw. Samwel Shelukindo, Afisa Mwandamizi kwenye Ubalozi wa Tanzania, Addis Ababa.
---------------------------------------------------------------------

Na Mwandishi wetu, Addis Ababa


Tanzania imechaguliwa kwa mara nyingine tena kuwa Mjumbe wa Baraza la  Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (PSC)  kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2014 hadi 2016.

Katika uchaguzi huo uliofanyika leo tarehe 28 Januari, 2014 wakati wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika, Tanzania na Ethiopia zimechaguliwa kuiwakilisha Kanda ya Afrika Mashariki katika Baraza hilo muhimu linaloshughulikia masuala ya amani na usalama Barani Afrika.

Tanzania ilichaguliwa kwa mara ya kwanza katika Baraza hilo mwaka 2012. Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa aliongoza ujumbe wa Tanzania katika uchaguzi huo.

Matokeo ya uchaguzi huo yanaonyesha kuwa Tanzania na Ethiopia zilipata kura 40 kati ya kura 50 zilizopigwa ambayo ni zaidi ya theluthi mbili ya kura zinazotakiwa huku Eritrea ikipata kura 13.

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lina Wajumbe 15 wanaochaguliwa na Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika. Wajumbe hao wanaowakilisha Kanda tano ambazo ni Afrika ya Kati, Afrika Mashariki, Afrika Kaskazini, Afrika ya Kusini na Afrika Magharibi.

Malengo ya Baraza hili ni pamoja na kulinda amani na usalama Barani Afrika; kuzuia migogoro; kulinda amani na kujenga amani katika maeneo yenye migogoro; kusimamia demokrasia, utawala bora, utawala wa sheria na haki za binadamu.

-Mwisho-



Tanzania na Algeria kudumisha ushirikiano

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Mhe. Ramtane Lamamra (hayupo pichani) walipokutana pembezoni mwa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) unaoendelea mjini Addis Ababa. Mazungumzo hayo yalihusu ushirikiano kati ya Algeria na Tanzania katika masuala mbalimbali ikiwemo sekta ya gesi na umeme. Wengine katika picha ni Balozi Vincent Kibwana (kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Togolani Mavura, Msaidizi wa Waziri na Bi. Zuleikha Tambwe, Afisa Mambo ya Nje.
Mhe. Lamamra naye akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yao.
Mhe. Membe akiagana na Mhe. Lamamra mara baada ya mazungumzo yao.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI






 Waziri Mkuu wa Finland kuzuru Tanzania

Waziri Mkuu wa Findland, Mhe. Jyrki Katainen atafanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Tanzania tarehe 29 na 30 Januari, 2014.Mhe.Katainen anategemewa kuwasili usiku wa tarehe 28 januari akitokea Addis Ababa, Ethiopia, na atafanyiwa mapokezi rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete, kesho yake asubuhi.

Mhe. Katainen atafuatana na Waziri wake wa Maendeleo ya Kimataifa, Mhe. Pekka Haavisto, na wafanyabiashara 25 wa Finland.

Baada ya mapokezi rasmi, Mhe. Waziri Mkuu wa Finland atafanya mazungumzo na Mwenyeji wake, Rais Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam, na baadaye atashiriki majadiliano kuhusu ushirikiano kati ya Ulaya na Afrika, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi  kwenye hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro.

Wakati wa ziara hiyo, Tanzania na Finland zitatiliana saini Mkataba wa Msaada wa Bajeti (General Budget Support) na Makubaliano ya Ushirikiano (Memorandum of Understanding) kwenye Nyanja za madini na misitu.

Mhe.Rais Kikwete atamwandalia mgeni wake chakula rasmi cha jioni, Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 29 Januari, Mhe. Katainen anatarajiwa kuzuru Unguja  na kukutana na Rais  wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein. Kadhalika, atafanya mazungumzo na Wafanybiashara, wachumi na maafisa wa mashirika ya kimataifa jijini Dar es Salaam, pamoja na kutembelea bandari, kabla ya kuondoka nchini Januari 30 usiku.

 

IMETOLEWA NA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

 

DAR ES SALAAM, JANUARI 27, 2014

Monday, January 27, 2014

Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa AU wafunguliwa rasmi Addis Ababa

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma akitoa hotuba ya ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika unaofanyika Mjini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 27 na 28 Januari, 2014. Mkutano huo ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi  na Serikali wa Umoja wa Afrika utakaofanyika mjini hapa tarehe 30 na 31 Januari, 2014.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia anaongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa AU, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa inatolewa na Dkt. Dlamini-Zuma (hayupo pichani). Wengine katika picha ni Mhe. Naimi Aziz (kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Balozi Vincent Kibwana, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mhe. Balozi Tuvako Manongi (kulia), Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani akiwa na Wajumbe wengine wakifuatilia kwa makini hotuba ya Dkt. Dlamini-Zuma (hayupo pichani)
Makamishna wa AU na Wawakilishi wa Mashirika mbalimbali wakifuatilia hotuba ya Dkt. Dlaini-Zuma  (hayupo pichani).
Mawaziri kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa baraza la mawaziri.
Kabla ya ufunguzi Dkt. Dlamini-Zuma aliwaongoza Wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri kusimama kwa heshima na kumkumbuka aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Hayati Mzee Nelson Mandela aliyefariki dunia mwezi Desemba, 2013.
Picha ya Pamoja mara baada ya ufunguzi.
Mhe. Membe akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe, Mhe. Simbarashe Mumbengegwi (katikati) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Mhe. Maite Nkoana-Mashabane
Maafisa Waandamizi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia wakibadilishana mawazo nje ya Ukumbi mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri.
Bw. Bujiku Sakila, Afisa Mambo ya Nje akimweleza jambo Bi. Zuleikha Tambwe, Afisa Mambo ya Nje mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri.



Na Rosemary Malale, Addis Ababa

Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) imetoa rai kwa nchi za Afrika kuongeza uzalishaji na uwekezaji katika kilimo kwa vile kinachangia kwa kiasi kikubwa Pato la Taifa kwa nchi Barani Afrika.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma wakati akifungua Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ulioanza leo tarehe 27 Januari, 2014 Mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Dkt. Dlamini-Zuma alisema kuwa,  kwa Afrika kuhakikisha ukuaji wa pato la taifa kwa asilimia 7 na zaidi ni vema kilimo kiwe kipaumbele kwa nchi wanachama, kwa vile kinachangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa kwa nchi zao. Alisema kuwa kwa mwaka huu wa 2014 ni muhimu kuongeza uwekezaji katika kilimo, uzalishaji, kuboresha miundombinu na ujuzi ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika tafiti za kilimo.

Alisisitiza kuwa Kamisheni yake kwa mwaka huu imejipanga kuchukua hatua madhubuti katika kuboresha kilimo ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wanawake ambao ndio kundi kubwa linaloshughulika na kilimo na chakula kwa kuwapatia  mafunzo, mitaji na kuwasaidia kuanzisha vikundi vya ushirika na masoko kwa bidhaa za kilimo. Pia, alieleza kuwa imefika wakati sasa kwa Afrika kuwa na kauli katika kupanga bei ya mazao na bidhaa zitokanazo na kilimo.

Aidha aliongeza kuwa, ili kufikia malengo hayo, Kamisheni ya Umoja wa Afrika itashirikiana na Taasisi nyingine za Kimataifa kama UNECA, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Nchi Wanachama, Vyama vya Kiraia na Jumuiya za Kikanda za Kiuchumi.
Dkt. Dlamini-Zuma alieleza kuwa Mkutano wa mwaka huu wenye kaulimbiu isemayo “Mwaka 2014 ni mwaka wa Kilimo na Usalama wa Chakula; Kuadhimisha miaka 10 ya Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Afrika (CAADP)” unalenga kuweka mikakati madhubuti katika kuhakikisha kilimo kinakuwa ni mkombozi wa Watu Barani Afrika kiuchumi na kwa usalama wa chakula.

Katika hatua nyingine, Dkt. Dlamini-Zuma ametoa wito kwa Waafrika wote kutoa michango na mawazo yao kuhusu Muundo wa Agenda 2063 ambayo inalenga katika kujenga Afrika Tunayoitaka katika kipindi cha miaka 50 ijayo kuanzia mwaka 2014.

Aidha, aligusia migogoro inayoendelea kusumbua baadhi ya nchi za Afrika kama vile Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo alisema kuwa Umoja wa Afrika, Jumuiya za Kikanda za Kiuchumi na Jumuiya ya Kimataifa zitaendelea kushirikiana ili kuzisaidia nchi hizi kupata suluhisho la kudumu katika migogoro yao.

“Mwezi Mei mwaka uliopita wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya Umoja wa Afrika tuliahidi  kwa watu wetu kuwa hatutavirithisha vizazi vijavyo vita na migogoro bali tuliapa kufanya kazi bila kuchoka kuhakikisha migogogro Barani humu inamalizwa kabisa hadi kufikia mwaka 2020” alisema Dkt. Dlamini Zuma. Vile vile, Dkt. Dlamini-Zuma alizipongeza nchi za Mali, Madagascar na Somalia kwa hatua waliyofikia katika kushughulikia migogoro yao.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri  ambao utamalizika tarehe 28 Januari, 2014 ni matayarisho ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika ambao utafanyika mjini hapa tarehe 30 na 31 Januari, 2014. Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri unaongozwa na Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

-mwisho-






Friday, January 24, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Mhe. Membe kumwakilisha Rais Madagascar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye sherehe za kumwapisha Rais Mteule wa Madagascar, Mhe. Henry Rajaonarimampianina zitakazofanyika nchini humo tarehe 25 Januari, 2014.

Mhe. Membe ataondoka kwenda Madagascar tarehe 24 Januari, 2014. Mahakama Maalum ya Uchaguzi nchini Madagascar ilimtangaza Mhe. Rajaonarimampianina kuwa mshindi wa uchaguzi wa Urais tarehe 17 Januari, 2014.
Duru ya kwanza ya uchaguzi huo ilifanyika tarehe 31 Julai, 2013, ambapo hakupatikana mshindi. Katika duru ya pili iliyofanyika tarehe 20 Desemba, 2013, Mahakama Maalum ya Uchaguzi ilitangaza kuwa Mhe. Rajaonarimampianina alipata asilimia 53.49 ya kura zote zilizopigwa huku mpinzani wake Bw. Jean Louis Robinson akipata asilimia 46.51.

Kwa kushirikiana na wanachama wengine wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Tanzania,  ambayo ilikuwa mwenyekiti wa  Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa mwaka mmoja ulioishia Agosti, 2013, ilitoa mchango mkubwa kuhakikisha Madagascar inaendesha uchaguzi wake katika hali ya amani na utulivu na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia, ili kumaliza mgogoro wa kisiasa ulioibuka mwaka 2008 baada ya Bw. Andry Rajoelina kuingia madarakani kwa kusaidiwa na Jeshi.

IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA,

DAR ES SALAAM23 JANUARI, 2014, Januari 23, 2014

Wednesday, January 22, 2014

Mhe. Waziri afungua Kongamano kuhusu masuala ya Diaspora

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano kuhusu masuala ya Uhamiaji na Watanzania waishio nje (Diaspora). Ufunguzi huo ulifanyika katika Hoteli ya JB Belmont Jijini Dar es Salaam tarehe 22 Januari, 2014. Mwingine katika picha ni Bw. Jo Rispoli, Mtaalam wa masuala ya Uhamiaji katika Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.
Baadhi ya wajumbe waliohudhuria ufunguzi wa kongamano hilo wakimsikiliza Mhe. Waziri Membe (hayupo pichani)


Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) hapa nchini Bw. Damien Thuriaux naye akizungumza huku Mhe. Membe na Bw.Rispoli wakimsikiliza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bibi Rosemary Jairo akifuatilia kwa makini ufunguzi wa kongamano kuhusu masuala ya Diaspora.

Wajumbe wakifuatilia hotuba ya ufunguzi. Kutoka kulia ni Bw. Seif Kamtunda, Afisa Mambo ya Nje, Bi. Linda Helgesson, Mtaalam wa masuala ya Maendeleo ya Wahamiaji, Bi. Sudah Lulandala, Afisa Mipango na Bi. Tunsume Mwangolombe, Afisa Mambo ya Nje.

Picha ya pamoja.


Mhe. Membe akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ufunguzi wa kongamano hilo.



Na Reginald Philip Kisaka

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) amesisitiza umuhimu wa Tanzania kuridhia uraia wa nchi mbili ili Watanzania wanaoishi ughaibuni waweze kufaidika na fursa za kiuchumi na kijamii zinazotolewa kwa raia katika nchi wanazoishi.

Mhe. Waziri alitoa kauli hiyo katika ufunguzi wa kongamano lililoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na kufanyika katika Hoteli ya JB Belmont jijini Dar es Salaam tarehe 22 Januari, 2014. Kongamano hilo ambalo linawakutanisha wawakilishi kutoka Serikalini, wanazuoni, asasi za kiraia na watafiti mashuhuri lina lengo la kujadili njia mbalimbali ambazo wanadiaspora wanaweza kuzitumia kuchangia maendeleo ya nchi yao kwa mazingira ya Tanzania.

Mhe. Waziri aliwambia wajumbe wa kongamano hilo kuwa hoja ya uraia wa nchi mbili itawasilishwa na kutetewa katika Kikao Maalum cha Bunge la Katiba ambacho kinatarajiwa kufanyika katika siku za karibuni. “Endapo uraia wa nchi mbili utaridhiwa, Watanzania wanaoishi ughaibuni wataweza kupata kazi nzuri na kukopa benki  katika nchi wanazoishi, hivyo kipato chao kitaongezeka ambacho watakitumia pia kuwekeza nyumbani. Mhe. Waziri alisikika akisema.

Mhe. Membe alitolea mfano wa nchi zilizoweka mazingira mazuri ya wanadiaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi zao kuwa ni pamoja na Nigeria, Ghana na Kenya.


Awali, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji hapa nchini Bw. Damien Thuriaux alisema kuwa, kongamano hilo ambalo litafanyika kuanzia tarehe 22 hadi 29 Januari 2014 lina lenga kuhamasisha uratibu wa masuala ya Uhamiaji na Diapora kwa kuzishirikisha Wizara na Taasisi mbalimbali. Aidha katika kushirikiana na Serikali ya Tanzania, Bw. Damien alisema kuwa Shirika lake litasaidia uundwaji wa Tovuti maalum kwa ajili ya watu waishio Nje (Diaspora) na masuala mengine yanayohusu uhamiaji.


Naibu Waziri akutana na Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda wa Afrika Kusini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb.) akizungumza wakati wa kikao chake na Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda wa Afrika Kusini, Mhe. Elizabeth Thabethe (wa pili kushoto). Mhe. Thabete anaongoza ujumbe wa Wafanyabiashara kutoka Afrika Kusini utakaoshiriki Semina kuhusu Biashara na Uwekezaji itakayofanyika hapa nchini tarehe 23 Januari, 2014. Wengine katika picha ni Mhe. Radhia Msuya (kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini na Mhe. Thanduyise Chiliza, Balozi wa Afrika Kusini hapa nchini.
Mama Hellen Rwegasira (wa pili kulia), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati wa kikao kati ya Mhe. Maalim na Mhe. Thabethe (hawapo pichani)
Wajumbe wengine kutoka Afrika Kusini na Tanzania wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Maalim na Mhe. Thabete (hawapo pichani). Kulia ni Bw. Adam Isara, Msaidizi wa Mhe. Maalim.
Mhe. Maalim akiagana na Mhe. Thabete mara baada ya mazungumzo yao.
Picha ya pamoja.






Tuesday, January 21, 2014

Mhe. Rais Kikwete apokea Hati za Utambulisho za Balozi wa Oman nchini



Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Oman hapa nchini Mhe.Soud Ali Bin Mohamed Al Ruqaishi. Hafla hiyo ilifanyika Ikulu, Dar es Salaam tarehe 21 Januari, 2014.

Mhe. Rais Kikwete akimtambulisha kwa Balozi Ruqaishi Mhe. Mahadhi Juma Maalim, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Mhe. Rais Kikwete akimtambulisha kwa Balozi Ruqaishi, Balozi Simba Yahya, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Mhe. Rais Kikwete katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Ruqaishi (wa pili kushoto) na Maafisa waliofuatana na Balozi huyo.

Mhe. Rais Kikwete akiwa katika mazungumzo na Balozi Ruqaishi mara baada ya kupokea hati zake za utambulisho.


Mhe. Mahadhi (wa kwanza kushoto),  Balozi Yahya (wa pili kushoto) na Maafisa Waandamizi katika Ofisi ya Rais wakifuatilia mazungungumzo ya Mhe. Rais na Balozi Ruqaishi (hawapo pichani)

Maafisa wakinukuu mazungumzo ya Mhe. Rais Kikwete na Balozi Ruqaishi (hawapo pichani). Kutoka kulia ni Dkt. Laurean Ndumbaro, Msaidizi wa Rais katika masuala ya Siasa, Bw. Muhidin Michuzi, Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais na Bw. Abbas Mngwali, Afisa Mambo ya Nje.

Balozi Ruqaishi akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Ikulu.

Balozi Ruqaishi (katikati) akisikiliza wimbo wa Taifa lake uliokuwa ukipigwa na Bendi ya Polisi kwa heshima yake mara baada ya kuwasili Ikulu. Kulia ni Mkurugenzi na Mkuu wa Itifaki, Balozi Maharage Juma na Mnikulu, Bw. Shaaban Gurumo.

Kikosi cha Bendi ya Polisi kikiwa kazini.

Balozi Ruqaishi akimshukuru Kiongozi wa Bendi ya Polisi.