Mhe. Membe kumwakilisha Rais Madagascar
Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) atamwakilisha Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye sherehe
za kumwapisha Rais Mteule wa Madagascar, Mhe. Henry Rajaonarimampianina
zitakazofanyika nchini humo tarehe 25 Januari, 2014.
Mhe. Membe ataondoka
kwenda Madagascar tarehe 24 Januari, 2014. Mahakama Maalum ya Uchaguzi nchini
Madagascar ilimtangaza Mhe. Rajaonarimampianina kuwa mshindi wa uchaguzi wa
Urais tarehe 17 Januari, 2014.
Duru ya kwanza ya
uchaguzi huo ilifanyika tarehe 31 Julai, 2013, ambapo hakupatikana mshindi. Katika
duru ya pili iliyofanyika tarehe 20 Desemba, 2013, Mahakama Maalum ya Uchaguzi
ilitangaza kuwa Mhe. Rajaonarimampianina alipata asilimia
53.49 ya kura zote zilizopigwa huku mpinzani wake Bw. Jean Louis Robinson akipata
asilimia 46.51.
Kwa kushirikiana na wanachama
wengine wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Tanzania, ambayo ilikuwa mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa mwaka
mmoja ulioishia Agosti, 2013, ilitoa mchango mkubwa kuhakikisha Madagascar
inaendesha uchaguzi wake katika hali ya amani na utulivu na kwa kuzingatia
misingi ya demokrasia, ili kumaliza mgogoro wa kisiasa ulioibuka mwaka 2008
baada ya Bw. Andry Rajoelina kuingia madarakani kwa kusaidiwa na Jeshi.
IMETOLEWA
NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA,
DAR
ES SALAAM23 JANUARI, 2014, Januari 23, 2014
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.