JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), limeiomba radhi Serikali ya Tanzania kufuatia taarifa waliyoitoa kwenye Mkutano wa 64 wa Kamati Tendaji (EXCOM) ya shirika hilo uliofanyika Geneva, Uswisi tarehe 30 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba, 2013. Katika taarifa yao kuhusu Afrika, UNHCR ilieleza kuwa Tanzania imewafukuza Wakimbizi wa Rwanda na Burundi katika operesheni ya kuwaondoa Wahamiaji haramu inayoendelea nchini.
UNHRC imeiomba radhi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia barua yake ya tarehe 2 Oktoba, 2013. Barua hiyo imeandikwa na Mkurugenzi wa UNHCR Kanda ya Afrika Bw. George Okoth-Obbo kwenda kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Pereira Ame Silima aliyeongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo unaofanyika kila mwaka.
Katika barua hiyo, UNHCR imeeleza kusikitishwa na taarifa hiyo ambayo si ya kweli na imekiri kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikishirikiana kwa karibu na UNHRC katika ngazi zote kuhakikisha kwamba hakuna mkimbizi anayerejeshwa kwao katika zoezi la kuwakamata na kuwarejesha kwao wahamiaji haramu linaloendelea nchini Tanzania.
Aidha, Bw. Okoth Obbo ameeleza kuwa UNHCR na Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla inatambua na kuthamini kwa dhati mchango mkubwa ambao Tanzania imeutoa na inaendelea kuutoa katika kuwahifadhi wakimbizi wa mataifa mbalimbali kwa kipindi cha takribani miaka 40.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea kauli hiyo na kueleza kwamba inatarajia na inaamini kwamba UNHCR itaendelea kutoa taarifa sahihi zenye kutoa picha halisi inayoonesha namna Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyotekeleza wajibu wake kuwalinda na kuwahifadhi Wakimbizi kwa mujibu wa Sheria za nchi na mikataba ya Kimataifa ambayo nchi imeridhia.
Mwisho.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
06, Oktoba, 2013
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.