TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mashauriano
kuhusu mgogoro wa Burundi baina ya Tanzania, Angola, Uganda na Jumuiya ya
Afrika Mashariki
Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ameihakikishia dunia
leo kuwa mazungumzo ya kuleta amani nchini Burundi bado yanaendelea vizuri licha
ya taarifa zilizosambaa kuwa mazungumzo hayo yamegonga mwamba.
Dkt. Mahiga ameyasema hayo kwenye mkutano na
waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mashauriano baina yake na Mhe. George
Pinto Chicoti, Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola na Mwenyekiti wa Baraza la
Mawaziri wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR); Mhe. Dkt. Crispus Kiyonga,
Waziri wa Ulinzi wa Uganda ambaye ni mwakilishi wa msuluhishi wa mgogoro wa
Burundi Rais Yoweri Kaguta Museveni, pamoja na Dkt. Richard Sezibera, Katibu
Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha tarehe 6 Januari 2016.
Akielezea madhumuni ya mashauriano hayo Dkt.
Mahiga alisema kuwa wadau hawa wanaunga mkono na kusifu jitihada zinazofanyika
ndani na nje ya Burundi zenye lengo la kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa
kisiasa na kiusalama nchini humo kwa njia ya majadiliano.
Aidha Waziri Mahiga alisema mazungumzo hayo
pia yanalenga kubadilishana ushauri, mawazo na kuandaa taarifa ya pamoja kabla
ya mikutano mikubwa ya kikanda; yaani ule wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu
(ICGLR Summit), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Summit) na Umoja wa Afrika (AU
Summit) inayotarajiwa kufanyika mwezi Januari mwaka huu.
Dkt. Mahiga alisema mazungumzo yao
yaliyojumuisha nchi za Tanzania, Angola na Uganda ambazo zimekasimiwa majukumu ya
uenyekiti na usuluhishi na jumuiya zao, yatatoa uelewa wa pamoja wa jinsi ya kuendesha
mashauriano ya kuleta amani ya kudumu kabla ya mikutano tarajiwa ambayo pamoja
na mambo mengine, itajadili pia suala la amani na usalama nchini Burundi.
“Naomba nirudie tena mbele yenu waandishi wa
habari kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya
uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli; kama wenyekiti wa jumuiya hii, bado
tuna nia ya dhati kabisa ya kuhakikisha kuwa kwa pamoja tunapata suluhu ya
mgogoro huu, ambayo ni muhimu sana kwa usalama na maendeleo ya eneo letu na
bara la Afrika kwa ujumla” alisisitiza Dkt. Mahiga kabla ya kuanza mazungumzo
ya faragha na viongozi wenzake.
Waziri Dkt. Mahiga alipongeza jitihada za
wadau wengine na jumuiya ya kimataifa zinazoendelea ili kuhakikisha amani ya
kudumu inapatikana nchini humo.
MWISHO.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara
ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kikanda
na Kimataifa.
06
Januari 2016
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.