TAARIFA KWA UMMA
UFAFANUZI KUHUSU
UINGIZWAJI WA MIFUGO NCHINI TANZANIA
Hivi karibuni kumekuwa na taarifa katika baadhi ya
vyombo vya habari na kutoka kwa baadhi ya wanasiasa kuishutumu Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia hatua ya kukamata na kupiga mnada
mifugo iliyoingizwa nchini bila kufuata sheria. Aidha, taarifa hizo zinajenga
sintofahamu kuhusiana na suala la vifaranga vya kuku vilivyoteketezwa kufuatia
kuingizwa nchini bila kufuata sheria. Baadhi ya taarifa hizo zimeenda mbali
zaidi na kudai kuwa hatua hizi zinaweza kudhoofisha mahusiano yetu na nchi
jirani.
Kadhalika, kufuatia suala hilo la kupigwa mnada kwa
ng’ombe walioingia nchini kinyume cha sheria, na wenye ng’ombe hao kukaidi
kuondoa mifugo yao hata baada ya kupewa muda kufanya hivyo, na kufuatia
kuteketezwa kwa vifaranga vilivyoingia nchini kinyume cha sheria na kanuni,
Serikali ya Kenya ilimwita Balozi wetu aliyeko Nairobi kutaka maelezo. Balozi
wetu alisikiliza maelezo ya Serikali ya Kenya na akatumia fursa hiyo kuelezea
masuala haya kwa Serikali ya Kenya. Vile vile Serikali imepokea barua kutoka
Serikali ya Kenya kuhusu masuala haya, na Serikali itaijibu barua hiyo kutoa
ufafanuzi.
Serikali inapenda kuufahamisha umma kwa ujumla kuwa
uingizwaji wa mifugo na bidhaa zake nchini Tanzania huongozwa na sheria za nchi,
makubaliano ya kikanda na kimataifa.
Sheria na taratibu hizi ni pamoja na:
(i) Sheria
ya Magonjwa ya Wanyama (Animal Disease Act) Na. 17 ya mwaka 2003 na kanuni zake
za mwaka 2007 na 2010, ambazo zinatumika kudhibiti na kukagua uingizaji wa
mifugo na mazao yake katika maeneo ya mpakani, bandarini na viwanja vya ndege;
(ii) Sheria
ya Nyanda za Malisho na Rasilimali ya Vyakula vya Wanyama (Grazing-land and
Animal Feed Resources Act) Na. 13 ya mwaka 2010 ambayo inasimamia nyanda za
malisho na ubora wa malighafi za kusindika vyakula vya mifugo;
(iii) Zuio (quarantine)
la uingizaji ndege na mazao yake nchini
la mwaka 2006, kutokana na uwepo wa ugonjwa hatari wa Homa ya Mafua Makali ya
Ndege katika nchi mbalimbali duniani. Ugonjwa huo umejitokeza kwenye nchi
jirani ya Uganda mwanzoni mwa mwaka 2017 na hivyo kuiweka nchi yetu katika
hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu iwapo zuio hili litakiukwa. Zuio hilo
halijaondolewa hadi leo.
(iv) Ukweli kwamba katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki mifugo na bidhaa za mifugo zinavuka mipaka kwa utaratibu maalum
kupitia kwenye vituo vya mipakani ambapo maofisa mifugo kutoka pande zote za
mipaka hufanya shughuli ya udhibiti.
Utekelezaji wa sheria na makubaliano haya hufanyika
bila ubaguzi wa uraia wa mwingizaji wa mifugo au nchi inakotoka mifugo hiyo.
Nchi zote duniani, zikiwemo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, zinadhibiti
uingizwaji wa mifugo na mimea katika nchi zao. Udhibiti huu hufanyika katika
viwanja vya ndege, bandari na vituo vya mipakani. Kwa mfano, katika Kituo cha
Huduma za Pamoja Mpakani cha Namanga, wapo maofisa wa mifugo na kilimo kutoka
Kenya na Tanzania wanaodhibiti uingizwaji wa mifugo na mimea kwenye nchi zao.
Katika utekelezaji na usimamizi wa sheria hii, ilibainika
kuwa idadi kubwa ya mifugo kutoka nchi za jirani imeingizwa nchini pasipo
kufuata sheria na taratibu zilizopo. Serikali iliagiza mifugo hiyo irudishwe
kwenye nchi ilikotoka kwani ilikuwa inahatarisha mazingira na kuongeza
uwezekano wa kusambaa magonjwa ya mifugo. Serikali ilitoa muda wa kutosha kwa
wamiliki wa mifugo hiyo kuiondoa nchini. Tahadhari ilitolewa kwamba muda uliotengwa
ukifikia ukomo, mifugo hiyo itakamatwa na kushugulikiwa kwa mujibu wa sheria za
nchi.
Pamoja na agizo hilo, Serikali kupitia Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilituma Waraka wa
Kidiplomasia kwa Serikali za Burundi,
Kenya, Rwanda na Uganda, ikizihimiza kuwataka raia wao walioingiza mifugo nchini
isivyo halali waiondoe. Wamiliki wengi walitii agizo hilo la Serikali ya
Tanzania na kuondoa mifugo yao nchini.
Hata hivyo, wapo wamiliki wachache kutoka nchi za jirani waliokaidi
agizo hilo na hivyo ng’ombe wapatao 1113 walikamatwa katika Wilaya ya Mwanga,
Mkoa wa Kilimanjaro na kupigwa mnada baada ya wamiliki wake kushindwa
kujitokeza. Katika mkoa huo wa Kilimanjaro wapo ng’ombe 74 ambao wamiliki wake
walijitokeza, wakalipa faini kwa amri ya mahakama na kuondoka na ng’ombe wao. Katika
Mkoa wa Kigoma ng’ombe 324 ambao wamiliki wake hawajajitokeza wamekamatwa na hatua stahiki
zinachukuliwa. Aidha, katika mkoa huo wa Kigoma ng’ombe 728 walikamatwa na
wamiliki wao walijitokeza na kulipa faini kutokana na maamuzi ya Mahakama. Katika
mkoa wa Kagera jumla ng’ombe 1,536 ambao wamiliki wake bado hawajulikani wanashikiliwa
na vyombo vya ulinzi na usalama na sheria itachukua mkondo wake.
Kwa
takwimu hizi ni wazi kwamba zoezi hili halijalenga nchi yeyote, kwa sababu sio
nchi moja tu imeathirika. Zoezi hili limelenga kutekeleza sheria na kanuni za
nchi yetu ili kulinda mazingira na kupunguza uwezekano wa kusambaa kwa magonjwa
ya mifugo. Hili suala halipaswi kusababisha mgogoro wa kidiplomasia na nchi
yeyote, labda tu mtu aamue kwa makusudi yasiyo mema kupotosha na kuchochea
mgogoro.
Aidha, tarehe 24 Oktoba, 2017 jumla ya
vifaranga vya kuku wa mayai 6,400 vilikamatwa
katika Mkoa wa Arusha kwa kuingizwa nchini bila kufuata sheria na kanuni.
Vifaranga hivyo vilikuwa kwenye maboksi 60 vikiwa kwenye gari lenye namba za
usajili T 285 BAY. Mmiliki wa vifaranga hivi alidai kwamba ameviingiza nchini
kutokea Kenya. Vifaranga hivi viliteketezwa kutokana na msafirishaji wa
vifaranga hivi kutokuwa na kibali cha aina yoyote kutoka mamlaka husika ya
udhibiti wa magonjwa ya mifugo hapa nchini ambayo ni Idara ya Huduma za Afya
Mifugo katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Pia,
mmiliki huyu alishindwa hata kuonesha kibali cha Serikali ya Kenya kumruhusu
kusafirisha vifaranga hivyo kutoka Kenya kuvileta Tanzania pamoja na kwamba
mmiliki huyu alidai kwamba vifaranga hivyo amevitoa Kenya. Ni muhimu ikafahamika kwamba nchi zote duniani, ikiwemo Kenya, hufuata
miongozo ya WTO na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) kwa kutoa vibali (export permit) kwa mtu yeyote anayetaka
kusafirisha mifugo nje ya nchi. Kosa
jingine kubwa ni kwamba vifaranga hivi havikupitishiwa kwenye vituo rasmi vya
Ukaguzi wa Mifugo na Mazao yake mipakani (zoosanitary
border posts) kwa mujibu wa sheria na kanuni husika.
Pamoja na yote haya, Mkurugenzi wa
Huduma za Mifugo Tanzania alimpigia simu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo (Director of Veterinary Services) wa
Kenya kutaka kujua kama Mamlaka za Kenya zina habari kuhusu vifaranga
waliokamatwa na kama Kenya itakubali kuruhusu vifaranga hivyo virudishwe Kenya.
Mkurugenzi huyu wa Kenya alisema hana
taarifa kuhusu vifaranga hivyo na kwamba Kenya haiko tayari kuruhusu vifaranga
hivyo kurudishwa nchini mwao kwa sababu havina nyaraka kulingana na miongozo ya
kimataifa.
Ni vizuri umma ukajua kwamba hii si mara
ya kwanza kwa Serikali kuteketeza vifaranga vilivyoingizwa nchini bila kufuata
sheria kanuni na taratibu. Vipo vifaranga vingi tu vimeteketezwa kwa namna hiyo
hiyo baada ya kukamatwa kwenye viwanja vyetu vya ndege na sehemu nyingine.
Kadhalika vifaranga ambavyo vimekuwa vikiteketezwa havitokei nchi moja tu.
Vifaranga vyote vinavyoingizwa nchini bila kufuata sheria na kanuni
zinazotulinda dhidi ya uwezekano wa magonjwa vinateketezwa mara moja bila
kujali vinatoka nchi gani. Hatua hizi tumekuwa tukizitekeleza tangu tuweke zuio
mwaka 2006, na hazijaathiri kwa namna yeyote ile mahusiano yetu na nchi yeyote.
Hatua yeyote ya kujaribu kufanya jambo hili kuwa ni la mgogoro wa kidiplomasia
dhidi ya nchi yeyote ile ni hatua isiyo sahihi.
Serikali inawaasa wananchi
na raia wa kigeni wazingatie sheria, kanuni na taratibu
pale wanapotaka kuingiza nchini au
kusafirisha nje ya nchi mifugo na mazao yake. Serikali ya Tanzania itaendelea kusimamia sheria, kanuni na taratibu za
nchi, kikanda na kimataifa zinazohusu utoaji na uingizaji wa mifugo na mazao
yake nchini. Tunapenda kuuhakikishia umma kwamba, usimamizi wa sheria hizi
hauwezi na hautakiwi kwa namna yoyote ile kuathiri mahusiano yetu na nchi
nyingine kwa sababu nchi zote duniani zinasimamia sheria kama hizi.
Mojawapo ya misingi ya Sera ya Mambo ya Nje ya
Tanzania ni kujenga na kuimarisha mahusiano na nchi nyingine pamoja na
kudumisha ujirani mwema. Hivyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea
kuhakikisha kuwa inalinda mahusiano mazuri yaliyojengwa kwa muda mrefu kati
yake na nchi nyingine duniani. Kadhalika, Serikali itaendelea kutumia fursa
mbali mbali, kama vile vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki na vikao vya pande
mbili kati yetu na jirani zetu, na pia vikao vya ujirani mwema mipakani,
kutatua changamoto zozote za kimahusiano zitakazo jitokeza kwa nia ya kuendelea
kuimarisha ujirani mwema.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
19 Novemba, 2017
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.