Na Mwandishi Maalum,
Mwanza
Wajasiriamali
wametakiwa kuendelea kuboresha bidhaa zao ili kudhibiti soko la nchi za Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC) na hatimaye Afrika nzima, hususan katika kipindi hiki
Bara la Afrika limeanzisha Soko Huru la Biashara (CfTA).
Hayo
yamesemwa leo tarehe 4 Desemba 2021 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama
(Mb) ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika Siku ya Tanzania kwenye Maonesho ya 21 ya
wajasiliamali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayofanyika jijini Mwanza
kuanzia tarehe 2 hadi 12 Desemaba 2021.
“Nimetembelea
mabanda ya wajasiriamali na kushuhudia bidhaa zenye ubora wa hali ya juu. Hivyo,
tuendelee kuboresha bidhaa zetu ili tuingie masoko mengine badala ya kutegemea
soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki pekee”, Waziri Mhagama alisema.
Waziri
Mhagama alitoa ahadi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi
nyingine za Jumuiya, kuimarisha maonesho hayo ili yaweze kupanua soko, kuongeza
ajira, kukuza uchumi na hatimaye kuondoa umasikini kwa raia wa nchi wanachama
wa EAC.
Maonesho
hayo ambayo yatafunguliwa rasmi tarehe 5 Desemba 2021 na Waziri wa Viwanda na
Biashara, Prof. Kitila Mkumbo (Mb) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan yanapambwa na shughuli mbalimbali zikiwemo
mafunzo kwa wajasiriamali yenye mada tofauti tofauti kama vile; vikwazo visivyo
vya kibiashara, wepesi wa kufanya biashara ndani ya Jumuiya, fursa za biashara
katika nchi ya Sudan Kusini, UVIKO-19 na biashara na namna ya kusafirisha
bidhaa baina ya nchi za Jumuiya.
Mada
hizo zinazowasilishwa na wabobezi kutoka sekta mbalimbali, zikiwemo Wizara ya
Viwanda na Biashara, Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na taasisi zinazosimamia
urasimishaji wa bidhaa, kwa siku ya tarehe 4 Desemba 2021, wajasiliamali
wamejifunza falsafa ya Kaizen ambayo inahimiza umuhimu wa mjasiriamali
kuboresha utendaji wake kila siku katika maeneo yote kama ya ubunifu, utafutaji
wa masoko, vifungashio, utoaji wa huduma kwa mteja n.k.
Mkurugenzi
wa Biashara na Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Keneth Bagamuhunda alieleza
namna maonesho hayo yanavyondelea kuimarika mwaka hadi mwaka na kubainisha kuwa
maonesho ya mwaka huu yameandaliwa vizuri na washiriki wamekuwa wengi zaidi
ukilinganisha na miaka mingine.
Wajasiriamali
zaidi ya 900 wanashiriki maonesho hayo wakiwemo 420 wa Kitanzania kutoka maeneo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na Zanzibar. Aidha, viongozi wa Serikali akiwemo
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi. Robert
Gabriel Luhumbi;
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Zanzibar, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudriki
Soragha; Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana, Kazi na Ajira, Mhe.
Patrobas Katambi; Waziri wa Jiji la Kampala, Hajatti. Minsa Kabanda; wabunge wanne
kutoka Uganda waliungana na Mhe. Mhagama katika Siku ya Tanzania kwenye maoesho
hayo. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.