Mhe. Waziri Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiingia rasmi katika Ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo mjini Dar es Salaam. Kulia ni Mhe. Balozi Rajabu Gamaha, Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mhe. Waziri Membe akiwa katika mazungumzo na Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mhe. Jaji Warioba akimkaribisha Mhe Waziri Membe wakati wa mazungumzo yao kuhusu uraia wa nchi mbili.
Mhe. Waziri Membe akielezea kuhusu suala la uraia wa nchi mbili.
Mhe. Jaji Warioba akiwa na Dkt. Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Tume ya Katiba, Katibu wa Tume ya Katiba na Naibu Katibu Mkuu wa Tume ya Katiba.
Balozi Bertha Semu-Somi (kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora, Bw. James Lugaganya, Mkurugenzi Idara ya Sera na Mipango na Bi. Naomi Zegezege, Afisa wa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakisikiliza kwa makini mazungumzo yanayoendelea.
Mhe. Jaji Warioba akielezea maoni ya Watanzania kuhusu uraia wa nchi mbili.
Kikao kikiendelea.
Balozi Bertha Semu-Somi, Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akielezea changamoto mbalimbali za wanadiaspora na uraia wa nchi mbili.
Dkt. Salim Ahmed Salim (kushoto), pamoja na Katibu wa Tume ya Katiba (katikati) na Naibu Katibu wa Tume ya Katiba wakimsikiliza Balozi Semu-Somi.
Mkutano ukiendelea.
Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba na Dkt. Salim Ahmed Salim wakisiliza kwa makini maoni ya Waziri Membe (hayupo pichani).
Jaji Mkuu Mstaafu Agostino Ramadhani, Makamu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (katikati) akielezea jambo wakati Mhe. Jaji Warioba na Mhe Waziri Membe wakimsikiliza.
Mhe Waziri Membe akitoka katika Ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba mara baada ya kumaliza mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Jaji Joseph Warioba.
Membe alonga
na Warioba kuhusu Uraia wa Nchi Mbili
Na Tagie
Daisy Mwakawago na Fatma Salum
“Uwepo
wa Diaspora ni lazima utambulike
Kikatiba,” asema Waziri Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa.
Waziri
Membe aliyasema hayo alipokutana na Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo katika Ofisi za Tume hiyo zilizopo mjini
Dar es Salaam.
Katika
mazungumzo yao, viongozi hao walijadili suala la uraia wa nchi mbili (dual citizenship) ambalo linapiganiwa
kwa kiasi kikubwa na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora).
“Tumekuja
kuwasilisha masuala muhimu mawili: moja,
uwepo wa uraia wa nchi mbili katika Rasimu ya Katiba na pili, Katiba mpya iruhusu
raia yoyote wa Tanzania aweze kuwa na uraia wa nchi nyingine pasipo kuukana uraia
wa Tanzania,” alieleza Waziri Membe.
Alisema
kuwa Wizara yake inatambua suala la uraia wa nchi mbili kuwa ni la msingi,
ambalo halikugusiwa katika Rasimu ya Katiba iliyopo.
“Chimbuko
la uraia wa nchi mbili lilitokana na wingi wa Watanzania walioko nje ya nchi ambao
wanatafuta fursa ya kuwekeza na kuinua maendeleo ya nchi yao,” alisema Waziri
Membe.
Aliongeza
pia, “Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005 inawatambua Watanzania
hao na kutaka wapewe fursa ya kuwa na uraia wa nchi mbili katika kuinua
maendeleo ya nchi.”
Watanzania
hao wamekuwa wakikabiliana na matatizo kadhaa ambayo yanawanyima haki za
msingi, kama vile afya, elimu na masuala ya ajira. “Kilio chao kimekuwa kero kubwa kwa vile
wakati mwingine wanatibiwa kwa gharama kubwa sana ambazo hazilingani na kipato
chao,” alisema Waziri Membe.
Aidha,
changamoto hizo zimekuwa ni chanzo kikubwa cha kuwashawishi Watanzania hao
kuchukua uraia wa nchi za kigeni ili kuwawezesha kupata huduma muhimu za
kijamii kama vile elimu na afya.
“Hivi
sasa sheria yetu haimruhusu Mtanzania kuchukua uraia wa nchi mbili pasipo kuukana
uraia wa nchi yake,” alisema Membe, na kufafanua kuwa “Ilani ya CCM
inamuhamasisha Mtanzania huyo achangie maendeleo ya nchi yake kupitia uraia wa
nchi mbili.”
Waziri
Membe alisema kuwa Watanzania wakiwa nje wanakosa fursa za kazi zenye kipato
kikubwa wasipokuwa na uraia wa nchi hiyo, jambo linalopelekea maisha magumu na
kushindwa kujikimu na kuchangia kipato chochote kwa ndugu zao walioko
nchini.
“Badala
yake, unakuta Watanzania wananaswa na tamaa ya ‘kujilipua’ kwa kubadili uraia wa
nchi nyingine zinazokubali uraia wa nchi mbili na kuachana na uraia wa Tanzania,” alieleza Waziri Membe.
Kwa
upande wake, Mhe. Warioba alisema kuwa maoni hayo ya uraia wa nchi mbili yamekuwa
yakijitokeza katika ukusanyaji wa maoni sehemu mbalimbali. Na kuongeza kuwa, hofu kubwa ya wananchi ni
usalama wa nchi yao endapo uraia wa nchi mbili utaruhusiwa.
Mhe.
Waziri Membe alikuwa ameambatana na Balozi Gamaha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Balozi Bertha Semu-Somi, Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora na Bw. James Lugaganya, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Kwa upande wa Mhe. Warioba, alikuwepo Jaji Mkuu Mstaafu Agostino Ramadhani, Makamu wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Salim Ahmed Salim, Mjumbe wa Tume, pamoja na
Katibu na Naibu Katibu wa Tume ya Mabadiliko.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.