Thursday, October 9, 2014

Mchakato wa kuanzisha Agenda ya Maendeleo unaridhisha, Balozi Mwinyi


Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Ramadhani Mwinyi akitoa hotuba kwa wajumbe wa Kamati ya Pili inayoshughulikia masuala ya uchumi na maendeleo jijini New York, Marekani. Wanaoekana nyuma ni Bw, Songelael Shilla, Afisa wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa na Bibi Haikael Shishira, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. 
Balozi Mwinyi akiendelea kuwasilisha hotuba yake, huku Bw. Shilla na Bibi Shishira wakisikiliza kwa makini.


wajumbe wakisikiliza hotuba ya Balozi Mwinyi hayupo pichani.

Na. Ally Kondo, New York

Serikali ya Tanzania imebainisha kuwa inaridhishwa na hatua zilizochukuliwa katika mchakato wa kuandaa Agenda ya Maendeleo baada ya Mwaka 2015. Hatua hizo ni pamoja na Jopo Maalum la Umoja wa Mataifa kuchambua na kupendekeza shabaha na Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo kwa kauli moja yamekubalika yatumike kuwa moja ya chanzo muhimu cha kuandaa Agenda ya Maendeleo baada ya Mwaka 2015.

Hayo yalisemwa na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Ramadhani Mwinyi wakati alipokuwa anahutubia Kamati ya Pili ya  Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya Uchumi na Maendeleo jijini New York siku ya Jumatano tarehe 08 Oktoba 2014.

Hata hivyo, Balozi Mwinyi alitahadharisha kuwa wakati mchakato wa kuandaa Agenda ya Maendeleo baada ya Mwaka 2015 ukiendelea, nchi zisijisahau kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Milenia (MDGs) ambayo yanafikia mwisho ifikapo mwaka 2015. Alielezea matumaini yake kuwa Agenda ya Maendeleo itakapoidhinishwa rasmi mwezi Septemba 2015 itazingatia kazi nzuri iliyofanywa katika utekelezaji wa MDGs.
Balozi Mwinyi aliahidi kuwa yeye na timu yake itashiriki kikamilifu katika kazi za Kamati hiyo kwa kuwa inajadili agenda muhimu zinazohusu maendeleo endelevu. Moja ya agenda hizo ni mabadiliko ya tabianchi ambayo ni changamoto kubwa kwa maisha ya ulimwengu wa sasa.

 Alisema wakati nchi zinajiandaa kuelekea katika mkutano utakaojadili namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika Lima, Peru mwezi Desemba 2014 na baadaye Paris, Ufaransa mwezi Desemba 2015 kuna umuhimu wa kuhimiza ili mikutano hiyo imalizike kukiwa kumepatikana makubaliano yenye nguvu ya Kisheria kuhusu namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake.

Aidha, Balozi Mwinyi aliwambia wajumbe wa Kamati ya Pili kuwa nchi yake inalipa kipaumbele suala la kilimo kwa kuwa ni chanzo cha chakula na ndio shughuli ya Watanzania wengi. Kwa minajili hiyo, Serikali yake inaunga mkono wito wa kujumuisha masuala ya maendeleo ya kilimo, usalama wa chakula na lishe katika Sera na Programu za Maendeleo katika ngazi za Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

Kwa upande wa Kitaifa, Mhe. Mwinyi alitaja baadhi ya hatua ambazo Serikali imezichukuwa katika kuendeleza sekta ya kilimo. Hatua hizo ni pamoja na Mpango wa Kilimo Kwanza na kuanzishwa kwa Mpango Maalum wa Kukuza Kililmo katika Ukanda Kusini (SAGCOT).  


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.