Waziri Membe akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali wakati wa mahojiano na waandishi wa habari kuhusu Warsha hiyo ya Amani na Usalama Barani Afrika. Picha zote na Rosemary Malale
=================================================
Na Ally Kondo, Arusha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal amesema kuwa, licha ya machafuko yanayoendelea hivi sasa katika Bara la Afrika, nchi za Afrika hazina budi kuunganisha nguvu ili ziweze kukabiliana na changamoto mpya zinazoibuka ambazo zinatishia amani, usalama na utulivu wa Bara hili. Changamoto hizo ni pamoja na ugaidi, uharamia, biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi, biashara ya dawa za kulevya, na biashara haramu ya binadamu.
Hayo aliyasema jijini Arusha siku ya Jumanne tarehe 21 Oktoba 2014 alipokuwa akifungua Warsha ya Ngazi ya Juu kuhusu Amani na Usalama iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika ambayo itafanyika kwa siku tatu hadi Alhamisi tarehe 23 Oktoba 2014.
Makamu wa Rais alieleza kuwa ugaidi ni changamoto kubwa katika Afrika kwa sababu hakuna hata nchi moja ambayo imesalimika na uovu huo. Alisema kuwa, licha ya nchi za Afrika kulengwa na mashambulizi ya kigaidi pia zinatumika na magaidi kufanya mashambulizi yanayolenga maslahi ya nchi za kigeni, kujificha, kuandaa na kusajili magaidi wapya pamoja na kuwa chanzo cha mapato kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao hizo haramu.
Aidha, Dkt. Bilal alibainisha kuwa katika kipindi cha miongo miwili iliyopita Bara la Afrika limeshuhudia likikumbwa na zaidi ya migogoro 20 ambayo imelifanya bara hilo kutambulika na sifa ya kuwa eneo la vita. Ukweli huo unadhihirishwa na idadi kubwa ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa ambapo kati ya vikosi 17 duniani, vikosi 9 vipo Barani Afrika. Aidha, asilimia 60 ya agenda za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinajadili namna ya kurejesha na kuimarisha amani Barani Afrika.
Dkt. Bilal alihimiza nchi za Afrika kuunganisha nguvu ili ziweze kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro katika Bara la Afrika kwa kuwa athari zake ni kubwa. Athari hizo ni pamoja na kudumaza uchumi wa nchi na kuharibu miuondombinu ya kijamii ambayo ilijengwa kwa miaka mingi; kukwamisha juhudi za kupunguza umasikini; ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na kuzalisha wakimbizi na wakimbizi wa ndani.
Hata hivyo, Dkt. Bilal alisifu juhudi zinazofanywa na AU na washirika wake ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kupunguza migogoro Barani Afrika. Kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita, Bara la Afrika limeshuhudia kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe, usuluhishi wa migogoro ya muda mrefu na migogoro ya baada ya uchaguzi katika nchi za Angola, Liberia, Sierra Leone, Rwanda, Burundi, Cote d’Ivoire na Madagascar.
“Kutokana na kuimarika kwa amani barani Afrika, uchumi wa bara hilo umeendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo kati ya nchi kumi duniani ambazo uchumi wake unakua kwa haraka katika kipindi cha muongo mmoja uliopita nchi sita zinatoka barani Afrika. Aidha, matarajio katika kipindi cha muongo mmoja ujao, nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara uchumi wake utakua kwa kiwango cha asilimia saba” alisema Dkt. Bilal.
Makamu wa Rais aliendelea kueleza kuwa Bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto za kiusalama kama ilivyo katika nchi za Libya; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; Sudan; Somalia; Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini.
Kwa upande wa Sudan Kusini, alisema kuwa Serikali imekubali ombi la Rais wa nchi hiyo, Mhe. Salvar Kiir la kusaidia usuluhishi wa mgogoro huo. Hivyo, Chama cha Mapinduzi tokea tarehe 12 – 18 Oktoba 2014 kimekuwa kikifanya majadiliano na vyama hasimu nchini Sudan Kusini kutafuta suluhu ya mgogoro huo. Alisema kuwa majadiliano hayo hayataingilia au kuharibu majadiliano yanayoendelea nchini Ethiopia ambayo nayo yanalenga kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
Warsha kuhusu amani na uslama Barani Afrika inayoendelea jijini Arusha ni ya tano kufanyika ambapo warsha zilizotangulia zilifanyika katika nchi za Misri na Cote d’Ivoire. Warsha hizo ambazo huwa zinawakutanisha Wajumbe Maalum, Mabalozi, Wataalamu wa masuala ya usalama zinalenga kujadili changamoto za usalama na namna ya kukabiliana nazo barani Afrika.
-Mwisho-
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.