Rais Shein
afungua Kongamano la tatu (3) la Diaspora
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein amefanya ufunguzi wa Kongamano la tatu la
Watanzania waishio Ughaibuni “Diaspora home coming” lililofunguliwa leo na linatarajiwa
kufanyika kwa muda wa siku mbili katika
Hotel ya Zanzibar Beach Resort Visiwani Zanzibar.
Kongamano hilo lenye kauli mbiu isemayo “Bridging
Tanzania Tourism and Investment: A new Outlook” MTU KWAO NDIO NGAO ikiwa na
lengo la kusisitiza kuunganishwa kwa sekta ya Utalii na Uwekezaji ili kwenda
sambamba na kasi ya maendeleo ya Serikali. Kongamano hili kwa mara ya kwanza
linafanyika Zanzibar na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, lilitanguliwa na
Makongamano mawili yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Shein katika hotuba yake ya ufunguzi,
alieleza jitihada za makusudi zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano katika kutambua haki na wajibu wa Watanzania waishio Ughaibuni. Hivyo kufuatia umuhimu huo Serikali iliamua
kuanzisha Idara ya Diaspora ambayo inasimamia masuala yote ya jumuiya za
wanadiaspora popote walipo katika mataifa mengine, sambamba na kuandaa sera ya
diaspora ambayo itamtambua mwanadiaspora pamoja na kuainisha fursa za uwekezaji
zilizopo katika sekta ya utalii na uchumi na namna Wanadiaspora hao wanavyoweza
kuchangia katika bajeti ya Serikali kwa kuchangia fedha katika akaunti maalum
na katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.
Vilevile
Mheshimiwa Rais Shein akaongeza kwa kusema kuwa “endapo sera hiyo ikikamilika
jumuiya za wanadiaspora zitaweza kusoma sera hiyo kupitia Tovuti ya Ikulu na
pale itakapohitajika kutunga sheria basi mamlaka zitafanya hivyo”.
Wazizi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ambaye
pia alishiriki katika hafla hiyo ya ufunguzi wa Kongamano, alitumia fursa hiyo
kuwaeleza kuwa Tanzania inavivutio vingi na kuwashauri ni vema wakatumia fursa hiyo kuvitangaza vivutio
vilivyopo na pia kuvipa kipaumbele vivutio ambavyo bado havijatambuliwa ili
viweze kutambuliwa rasmi na kutangazwa duniani kwote na kuiwezesha nchi ya
Tanzania kushika nafasi ya juu miongoni mwa mataifa yenye vivutio na maajabu
mengi duniani.
Pia alieleza Wizara kupitia Idara ya diaspora
inaendelea na utaratibu wa kuandaa mfumo wa kuwatambua wanadiaspora na
utekelezaji wake unaelekea kukamilika na kwamba zoezi hilo litakuwa la
kuendelea ambapo takwimu zitakuwa zikihuishwa mara kwa mara katika ofisi zote
za Ubalozi zinazoiwakilisha nchi ya Tanzania katika mataifa mengine.
Pia aliwaasa wanadiaspora hao kujiepusha kushiriki
katika makosa ya kihalifu na makosa mengine ambayo yanapingana na sheria na
taratibu za nchi husika. “Wizara yangu wakati mwingine imekuwa ikipokea taarifa
za vitendo ambavyo zinaichafua sifa ya nchi yetu au kuleta masikitiko kwa ndugu
na jamaa” alisema Waziri Mahiga.
Hivyo ni wakati sasa kila mwanadiaspora akawa balozi wa
Tanzania katika nchi anayoishi kwa kutumia vizuri fursa za kimaendeleo zilizopo
katika Taifa analoishi, pamoja na kudumisha sifa nzuri ya upendo, amani na
mshikamano iliyojengeka tangu siku nyingi, ikiwa ni pamoja na kudumisha utamaduni
wa Taifa.
Aidha, Watanzania waishio Ughaibuni walipata fursa ya
kusikiliza mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa na watoa mada kutoka
katika Taasisi na Idara za Serikali pamoja na sekta binafsi zilizolenga katika
kuwapa taarifa za taratibu za uwekezaji
na miradi mbalimbali inayotekelezwa na
mashirika ya Umma na Makampuni binafsi sambamba na kuwaeleza fursa nyingine mpya za miradi ya kiuchumi kama
ujenzi, masoko kwaajili ya biashara mbalimbali,
utalii pamoja na uwekezaji katika sekta ya viwanda kwa lengo la kuunga
mkono sera ya serikali ya awamu ya tano katika adhima yake ya kujenga Tanzania
ya viwanda.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.