Balozi wa Tanzania kwenye Muungano wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Chabaka Kilumanga akitunukiwa Nishani ya Juu (highest civilian honor) na Rais wa nchi hiyo, Mhe. Azali Assoumani hivi karibuni. |
Nishani hiyo imetolewa na Mhe Azali kwa kutambua mchango wa Balozi Kilumanga katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Comoro, pamoja na kumpongeza kwa utumishi uliotukuka. |
Hafla hiyo ilifanyika Ikulu ya
Comoro kwa ajili ya kumuaga Balozi Kilumanga baada ya kumaliza muda wake wa
kazi nchini humo
|
Mhe. Rais Azali (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Kilumanga na Mkewe |
Balozi Kilumanga akipongezwa na Mkuu wa Utawala Ubalozini, Bw. Mudrick Soragha mara baada ya kutunikiwa nishani na Rais wa Comoro |
============================================
BALOZI WA TANZANIA VISIWANI COMORO
ATUNUKIWA MEDANI YA JUU YA HESHIMA NA MHE. AZALI ASSOUMANI, RAIS WA MUUNGANO WA
VISIWA VYA COMORO TAREHE 16 FEBRUARI 2017
Balozi wa Tanzania ndani ya Muungano wa Visiwa vya Comoro
Mhe. Chabaka Kilumanga ametunukiwa Nishani ya Juu (highest civilian honor) na
Rais wa nchi hiyo Mhe. Azali Assoumani. Mhe. Balozi ambaye aliongozana na Mkewe
Bi Irene Kilumanga walishiriki katika hafla hiyo iliyofanyika Bait Salam, Ikulu
ya Comoro tarehe 16, Februari 2017. Wageni waalikwa walioshuhudia
hafla hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro, Mhe. Baccar Dossar na Katibu Mkuu Kiongozi wa
Serikali ya Comoro Mhe. Yousef Mohamed Yousef.
Hafla hiyo ilifanyika ikiwa ni sehemu ya sherehe ya
kumuaga Balozi huyo ambaye amemaliza muda wake wa kazi Visiwani Comoro na
kuelekea kustaaafu ifikapo tarehe 17 Machi, 2017. Mhe. Chabaka Kilumanga
anakuwa ndio Balozi wa mwanzo kutunukiwa nishani hiyo miongoni mwa mabalozi
wenzake wanao tumikia nchi zao Visiwani Comoro. Wakati akimtunuku medani hiyo,
Mhe Azali alieleza kutambua mchango mkubwa aliofanya Balozi huyo katika
kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Comoro, pamoja na
kumpongeza kwa utumishi uliotukuka.
Kwa upande wake Mhe. Balozi alieleza kufarijika sana
kwa kutunukiwa Nishahi hiyo ambayo imekuwa ni heshima kubwa kwake. Aidha, Balozi
Kilumanga alipongeza juhudi za Serikali ya Mhe. Azali kwa hatua inazochukua
katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Comoro. Pia alipendekeza kwa Serikali
hiyo kuanza kufanya taratibu za kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa
ni sehemu ya mkakati wa kupanua wigo wa ushirikiano baina ya Tanzania na Comoro.
Kutunukiwa kwa nishani hiyo kulikuwa ni kwa kushtukiza
kwani Mhe. Balozi hakutarajia kabisa kutunukiwa nishani hiyo ambayo kwa kawaida
hupewa raia wa Comoro ambao wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa
lao. Hivyo hii imekuwa ni heshima kubwa sio tu kwa Mhe. Balozi bali pia kwa
Tanzania.
Wakati
wakiagana na Mhe. Rais, Mhe. Balozi na Mkewe Bi Irene Kilumanga walieleza kuwa
kamwe hawatasahau upole na ukarimu wa Wacomoro na kwamba Comoro itaendelea kuwa
mioyoni mwao daima.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.