Monday, February 6, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Naibu Katibu Mkuu awatembelea Watanzania wanaoshikiliwa nchini Malawi

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi amewasihi Watanzaniawananewanaoshikiliwa katika Gereza Kuu la Mzuzu nchini Malawi kwa tuhuma za kuingia kinyume cha sheria katika mgodi wa urani wa Kayerekera kuwa  wavumilivu wakati Serikali ikitafutaufumbuzi wa suala lao.

Balozi Mwinyi aliyasema hayo alipowatembelea gerezani ambapo katika ziara hiyo alifuatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Hassan Bendeyeko pamoja na maafisa wengine kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi.

Balozi Mwinyi aliwaeleza Watanzania hao kuwa mazungumzo katika ngazi mbalimbali kati ya Tanzania na Malawi yanaendelea na kuna matumaini makubwa kuwa hivi karibuni ufumbuzi wa suala lao unaweza kupatikana.
Balozi Mwinyi aliendekea kuekeza kuwa yeye na wenzake wamekuja Lilongwe kushiriki kikao cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi,   lakini wameamua kusafari  takriban kilomita 400 kutoka Lilongwe  hadi Mzuzu kuja kuwaona na kuwafikishia ujumbe kuwa Serikali inafanya jitihada kuhakikisha kuwa suala hili linapatiwa ufumbuzi kwa haraka.

"Nikufahamisheni kuwa jitihada katika ngazi mbalimbali kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo lenu zinaendelea na hata Mhe.  Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokutana na Rais wa Malawi, Mhe. Prof. Peter Mutharika pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika nchini Ethiopia jambo lenu lilikuwa moja ya masuala  waliyoyajadili.

Naibu Katibu Mkuu alisema kuwa alifarijika kuwakuta watu hao wote wapo salama na wenye afya nzuri na kuwajulisha kuwa ziara hiyo ya kuwatembelea na nyingine zilizofanyika siku za nyuma ni ushahidi dhahiri kwao na kwa Watanzania kwa  ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. Magufuli imedhamiria kuwahudumia Watanzania wote wa kada mbalimbali popote pale wanapoishi.

Watanzania hao wanane walikamatwa mwishoni mwa mwezi Desemba, 2016 na hadi sasa wanashikiliwa katika gereza kuu la Mzuzu. Watanzania hao ambao kati yao wawili ni wanawake  wamejitambulisha ni wakulima na wachimbaji wadogo wa madini wanatoka katika mkoa wa Ruvuma na walikwenda Malawi chini ya Taasisi ya CARiTAS kujifunza athari za migodi ya urani katika jamii.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Tarehe 05 Februari 2017

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.