TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa kuhusu Watanzania waliopata
matatizo nchini Msumbiji
Tumepokea taarifa za kukamatwa na kufukuzwa kwa raia wa Tanzania
waliokuwa wakiishi katika mji wa Monte Puez ulio Cabo Delgado, Jamhuri ya
Msumbiji.
Serikali ya Msumbiji imekiri kuwepo kwa operesheni maalum ya kuwakamata
na kuwarudisha raia wa nchi za kigeni wanaoishi katika mji huo bila kufuata
Sheria za Uhamiaji za nchi hiyo. Aidha, Serikali hiyo imetaarifu kwamba, zoezi
hilo limeanzia mji wa Monte Puez kwa kuwa una raia wengi wa kigeni
ikilinganishwa na miji mingine.
Kufuatia hali hiyo, Ubalozi wetu nchini Msumbiji upo eneo la tukio ili
kufuatilia suala hili na mamlaka husika. Aidha, unaendelea kufanya mawasiliano
ya Kidiplomasia na Serikali ya Msumbiji ili kuhakikisha usalama wa Watanzania
na mali zao, unapewa kipaumbele. Inakadiriwa kuwa Watanzania wapatao elfu tatu
(3,000) wanaishi na kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii katika mji huo wa
Monte Puez.
Kuanzia zoezi hilo lilipoanza, Raia wa Tanzania wapatao 132
wamesharudishwa nchini. Tarehe 11/02/2017 walirejeshwa raia 58. Tarehe
14/02/2017 wamerejeshwa raia 24 na leo tarehe 15/02/2017 wamesharejeshwa raia
50.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawahakikishia
Watanzania kuwa uhusiano kati ya Tanzania na jirani yetu Msumbiji ni mzuri, na
hivyo itafanya kila jitihada kuhakikisha hali ya usalama wa Watanzania na
biashara zao, inarudi kuwa shwari na kwa wakati. Mwezi Desemba 2016, Tanzania
na Msumbiji zilifanya mkutano wa ujirani mwema uliolenga kuimarisha ushirikiano.
Mkutano huo uliofanyika kwenye mji wa Pemba, Cabo Delgado uliainisha maeneo ya
ushirikiano yakiwemo masuala ya biashara na uhamiaji.
Serikali inaendelea kuwakumbusha Watanzania waishio ughaibuni, kufuata
Sheria na taratibu za nchi hizo, ikiwemo kuwa na vibali halali vya makazi na
biashara.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki
15 Februari, 2017
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.