TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
HAKUNA TISHIO LA USALAMA NCHINI
Kumekuwa na taarifa kwenye
mitandao ya kijamii zinazosambazwa na watu wasioitakia mema nchi, zinazotishia
usalama wa raia na mali zao. Taarifa hizo zimewatia hofu baadhi ya raia wa
kigeni na wanadiplomasia wanaofanya kazi na kuishi hapa nchini.
Taarifa hizo zimekuwa zikidai kuwa
kutakuwa na maandamano yatakayofanyika tarehe 26 Aprili 2018 na zinawaonya raia
wa kigeni wasiende Zanzibar katika kipindi cha Sikukuu ya Pasaka na sherehe za
Muungano kwa sababu za kiusalama.
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawahakikishia wanadiplomasia na raia wote wa
kigeni wanaofanya kazi na kuishi nchini na wananchi kwa ujumla kuwa, waendelee
na shughuli zao ikiwemo kusafari kutoka eneo moja kwenda jingine bila ya hofu
yeyote kwa kuwa hakuna dalili zozote za uvunjifu wa amani, usalama na utulivu
wa nchi.
Vyombo vya usalama vipo makini
vinatekeleza majukumu yake ipasavyo kuhakikisha kuwa matukio yote ya uhalifu
yanadhibitiwa kabla ya kuleta madhara kwa umma.
Hivyo, Wizara inawaomba
wanadiplomasia, raia wa kigeni wanaoishi nchini na wananchi kwa ujumla
kuzipuuza taarifa hizo. Wananchi waendelee kushirikiana kwa karibu na Serikali yao
kupata taarifa sahihi kutoka vyanzo vinavyoaminika badala ya kutegemea propaganda
za watu wanaotumia mitandao ya kijamii kwa maslahi binafsi.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 29
Machi 2018
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.