Tuesday, April 3, 2018

Tanzania na Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi zasaini Mkopo wa masharti nafuu


TANZANIA NA MFUKO WA MAENDELEO WA ABU DHABI ZASAINI MKOPO WA MRADI WA UJENZI WA BARABARA YA UVINZA-MALAGARASI YA MKOANI KIGOMA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi leo tarehe 02 Aprili, 2018 zimesaini mkataba wa mkopo nafuu wa Dola za Kimarekani milioni 15 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Uvinza-Malagarasi yenye urefu wa kilometa 51.

Hafla fupi ya uwekaji saini wa mkataba huo imefanyika katika makao makuu ya mfuko huo yaliyopo Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambapo Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa amesaini kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Mohamed Saif Al Suwaidi Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi amesaini kwa niaba ya Mfuko huo.

Kusainiwa kwa mkataba huo ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya  Tanzania na mfuko huo baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya barabara ya Kidahwe-Uvinza (KM 77) ambayo pia ilifadhiliwa na mfuko huo kwa mkopo nafuu wa Dola za Kimarekani milioni 57. Hivyo, kukamilika kwa barabara ya Uvinza –Malagarasi kutaunganisha Daraja la Malagarasi (Kikwete Bridge) ikiwa ni azma ya Serikali ya kuunganisha barabara za Kigoma, Tabora hadi Manyoni (Singida) ambapo pia itaiunganisha nchi jirani za Burundi na Kongo DRC.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Mhandisi Iyombe amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati kwa kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara ambapo kusainiwa kwa mkataba huo ni ishara mojawapo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi kwa upande wake amesema kuwa Mfuko huo uko tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini hususan katika kipindi hiki ambapo Serikali ya Tanzania imeidhihirishia dunia umakini katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa kufufua nidhamu ya fedha; kupambana na rushwa pamoja na uwajibikaji kwa manufaa ya watanzania.

Kwa upande wake, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Umoja wa Falme za Kiarabu Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk  amesema kuwa mahusiano baina ya nchi ya Tanzania na UAE yameendelea kukua siku hadi siku, na kwa sababu hiyo wawekezaji; wafanyabiasha na wadau wa maendeleo wa UAE ukiwamo Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi wamezidi kuiamini Tanzania na kuendelea kushirikiana kwa karibu.

Balozi Mbarouk alisema kuwa, UAE ina fursa nyingi sana katika uchumi ambapo Tanzania inaweza kunufaika nazo hususan kwenye upande wa uwekezaji, biashara na utalii. Tanzania inaweza kupata wawekezaji wakubwa kutoka UAE; kupata soko la bidhaa zake hususan mazao ya kilimo na mifugo pamoja na kukuza utalii kupitia familia za kifalme zinazokuja kutalii nchini lakini kwa kuvutia watalii wanaotembelea huku hususan Dubai ili waje pia Tanzania. “Hii yote inawezekana kutokana na mahusiano mazuri yalipo baina ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu yanayoendelea kukua siku hadi siku” …alisema Balozi Mbarouk.

MWISHO,
02 Aprili, 2018
ABU DHABI, UMOJA WA FALME ZA KIARABU


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.