Wafanyabiashara nchini kutafutiwa Soko
Ufaransa
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini
Ufaransa kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), inaratibu
ziara ya viongozi wa makampuni ya biashara zaidi ya 30 kutoka Ufaransa ambao ni
wanachama wa Taasisi ya Sekta Binafsi ya Ufaransa (MEDEF) yenye mtandao wa makampuni
zaidi ya 7100..
Ziara
hiyo itakayofanyika kuanzia tarehe 15 – 18 Aprili 2018, inalenga kukuza
ushirikiano wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Ufaransa; kutangaza
fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania; kushawishi makampuni
makubwa ya Ufaransa kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo nishati,
miundombinu, viwanda, maji n.k na kutoa fursa kwa wafanyabiashara kutoka
Tanzania na Ufaransa kubadilishana
uzoefu na kuanzisha ushirikiano baina yao.
Ukiwa
nchini, ujumbe huo utapata fursa ya kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa
serikali na kushiriki katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji baina ya
Tanzania na Ufaransa litakalofanyika tarehe 18 Aprili 2018, jijini Dar es
Salaam.
Aidha,
baada ya kongamano hilo, Wizara kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa kwa
kushirikiana na Mamlaka
ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) itafanya mkutano na
wafanyabiashara Wakitanzania wenye nia ya kutafuta masoko nchini Ufaransa,
tarehe 20 Aprili 2018. Ubalozi utaelezea fursa zilizopo nchini Ufaransa na
mikakati ya kufanya bidhaa za Tanzania hususan za kilimo ziweze kuuzwa nchini humo.
Wizara
inatoa wito kwa Wafanyabishara wa Tanzania kushiriki kikamilifu na kuchangamkia
fursa hii muhimu.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
13 Aprili, 2018
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.