Friday, April 13, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


ZIARA YA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA BRAZIL NCHINI 14 – 17, APRILI, 2018

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Brazil, Mhe. Balozi Fernando Jose Marroni de Abreu anatarajia kufanya ziara hapa nchini kuanzia tarehe 14 hadi 17 Aprili, 2018.
Katika ziara hiyo, pamoja na mambo mengine, atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt Susan Alphonce Kolimba tarehe 16 Aprili, 2018. Viongozi hawa watajadiliana namna ya kuboresha mahusiano na mashirikiano ya kidiplomasia baina ya Tanzania na Brazil, hususan katika eneo la uwekezaji na biashara.

Mhe. Dkt. Kolimba na Mhe. Balozi Fernando Jose Marroni de Abreu wanatarajiwa kushiriki kwenye majadiliano ya kisiasa, mambo makubwa yatakayojadiliwa ni; Ushirikiano wa kiuchumi na biashara ikiwemo, matokeo ya kusainiwa kwa mkataba wa msamaha wa deni la Tanzania kwa Brazil, pamoja na masuala mengine yenye maslahi kwa wote kiuchumi na kibiashara, taathmini ya utekelezaji wa Mradi wa Pamba Ziwa Victoria ‘Cotton Victoria Project’ na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya mifugo nchini hususan kusaidia jitihada za Serikali za kuboresha ufugaji wa ng’ombe aina ya zebu.

Aidha, katika majadiliano hayo pia watazungumzia  kuhusu Masuala ya kimataifa hususan mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na Masuala ya Kikanda hasa Migogoro ya kisiasa nchini Sudan ya Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
 13 Aprili, 2018



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.