Sunday, December 6, 2020

MAWAZIRI SADC - TROIKA WAJADILI UPIGAJI KURA KWA WAGOMBEA WA KAMISHENI YA AU

Mawaziri wa SADC Double Troika wamejadili na kutolea maamuzi mapendekezo ya namna ya kupigia kura kwa wagombea kutoka Kundi la Kusini wanaowania nafasi mbalimbali kwenye Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika katika Mkutano Mkuu wa 34 mwezi Februari, 2021.

Majadiliano hayo yamefanyika katika mkutano wa Mawaziri ulifanyika mwishoni mwa wiki (Ijumaa) kwa njia ya mtandao (Video Conference) chini ya Uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano kutoka Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. VerĂ³nica Nataniel Macamo Dlhovo.

Aidha, Mkutano wa Mawaziri ulitanguliwa na Kikao cha Makatibu Wakuu siku hiyo hiyo ambapo kikako hicho kilichoratibiwa chini ya Uenyekiti wa Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda na Kibara na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa SADC kutoka Jamhuri ya Msumbiji, Balozi Alfredo Fabiao Nuvunga.

Katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) aliwakilishwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.

Itakumbukwa kuwa, mnamo mwezi Juni, 2020 Umoja wa Afrika (UA) ulitangaza nafasi za kazi za ngazi za juu ikiwa ni pamoja na nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni (1), Naibu Mwenyekiti wa Kamisheni (1) na Makamishna (6). Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zilialikwa kushiriki katika mchakato huo kwa kutangaza na kuhamasisha umma kuomba nafasi hizo.  

Tanzania pia ni nchi mojawapo inayogombea nafasi mbalimbali kwenye Kamisheni ya Umoja wa Afrika. Nchi zilozoshiriki katika mkutano huo ni pamoja Msumbiji, Malawi, Tanzania, Botswana Afrika Kusini na Zimbabwe. 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiwasilisha mada katika Mkutano wa Mawaziri wa SADC Double Troika kwa njia ya mtandao (Video Conference) jijini Dar es Salaam  

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiwasilisha mada katika Mkutano wa Mawaziri wa SADC Double Troika kwa njia ya mtandao (Video Conference) jijini Dar es Salaam 

 




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.