Balozi wa Tanzania
nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akitoa hotuba kumpongeza Bwana Patel kwa
kukubali kuiwakilisha Tanzania jijini Mumbai na kumtaka kuiwakilisha vema nchi. |
Balozi wa Tamzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania Jijini Mumbai Bwana Nayan Patel wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wageni walioshriki halfla ya uwekaji saini wa Mkataba wa Kazi wa Mwakilishi wa Heshima. |
Tanzania yafungua ofisi ya Mwakilishi
wa Heshima jijini Mumbai
Serikali ya Tanzania imefungua rasmi
ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika Jiji la Mumbai katika hafla
iliyofanyika jijini humo tarehe 04 Desemba 2020.
Mumbai ni jiji kuu la biashara na
viwanda nchini India (commercial and industrial hub) ambapo linachangia zaidi
ya asilimia 6 la pato la India na pia linachangia zaidi ya asilimia 25 ya
uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani nchini India (25% of industrial
output).
Aidha, Mumbai ni jiji mojawapo kati
ya majiji kumi duniani, yanayoongoza kwa biashara, hususan katika mzunguko wa
fedha duniani (global financial flow). Vilevile, Mumbai ni Jiji linaloongoza
kuwa na mabilionea wengi nchini India, ambapo linashika nafasi ya 9 kuwa na
mabilionea wengi duniani.
Kadhalika, shughuli za biashara na
huduma za kifedha katika Jiji hilo lenye watu zaidi ya milioni 20 zinachangia
mzunguko wa fedha katika uchumi wa India kwa zaidi ya asilimia 70.
Ni kutokana na umuhimu wa Jiji hilo,
Serikali iliamua kusogeza karibu huduma za kikonseli, biashara, uwekezaji,
utalii na mengineyo kwa kuwa na Mwakilishi wa Heshima atakayeratibu shughuli
hizo kwa karibu. Ikumbukwe India ni nchi kubwa yenye uchumi mkubwa na idadi
kubwa ya watu duniani wanaofikia bilioni 1.2. Hivyo, si rahisi kwa nchi zenye
uwakilishi mjini New Delhi kuweza kuhudumia kwa ukamilifu nchini India bila
kuwa na ofisi za aina hii.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Balozi
wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda alielezea juu ya umuhimu wa ofisi
ya Mwakilishi wa Heshima jijini Mumbai kuwa itasaidia kutoa huduma za Kikonseli
kwa karibu zaidi na pia itasaidia zaidi kuvutia na kutangaza fursa mbalimbali
za biashara, uwekezaji zilizopo nchini, kutafuta masoko ya bidhaa za kilimo na
viwanda vya Tanzania pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii wa Tanzania ili
kukuza sekta ya utalii nchini.
Aidha, Balozi Luvanda alieleza kuwa
ofisi hiyo itachangia katika kukuza biashara zaidi kati ya Jiji la Dar es
Salaam na Mumbai kufuatia kuimarishwa kwa huduma za usafiri wa anga baada ya
Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) kuanza safari zake za ndege za moja
kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Mumbai tangu mwezi Julai 2019. Vilevile,
majiji haya yanaunganishwa na bandari kuu muhimu ambazo ni Bandari ya Dar es
Salaam, kwa upande wa Tanzania, na Bandari ya Mumbai, kwa upande wa India.
Bwana Nayan Patel, ni raia wa India
na mfanyabiashara mwenye mtaji mkubwa jijini Mumbai na amekwishaanza rasmi kazi
ya Uwakilishi wa Heshima baada ya kukamilika kwa taratibu zote za
kidiplomasia.
Bwana Patel aliishukuru Serikali ya
Tanzania kwa kumpa heshima kubwa ya kuiwakilisha Tanzania jijini Mumbai na
maeneo mengine ya jirani na akaahidi kuitendea haki nafasi hiyo kadri
atakavyoweza.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.