Na Mwandishi Wetu, Dar
Serikali imewaelekeza mabalozi
walioteuliwa hivi karibuni kuhakikisha kuwa wanatekeleza na kusimamia
diplomasia ya uchumi kwa maslahi mapana ya Taifa.
Maelekezo hayo yametolewa
na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata
Mulamula (Mb) katika hafla ya kufunga mafunzo maalumu ya wiki mbili yaliyokuwa
yanatolewa kwa mabalozi hao katika Chuo cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam.
“Leo nimefunga mafunzo ya
wiki mbili kwa mabalozi wetu walioteuliwa hivi karibuni, na imekuwa ni utaratbu
wa Wizara kuwanoa kabla ya kwenda katika vituo vyao vya kazi. Mafunzo haya
huwajengea uwezo mabalozi kupata ufahamu zaidi pamoja na kujua majukumu yao
katika kuendeleza diplomasia ya uchumi, kuhamasisha wawekezaji, utalii na
maeneo mengine mengi,” Amesema Balozi Mulamula.
Pamoja na mambo mengine,
Balozi Mulamula amewasisitiza mabalozi umuhimu wa kufahamu na kutekeleza Diplomasia
ya Siasa iliyopo ndani ya Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi CCM
(2020-2025) ili kuweza kuwasaidia kujua dira a nchi.
Pia Balozi Mulamula
aliwataka mabalozi kuhakikisha kuwa wanaendeleza lugha ya Kiswahili katika
mataifa wanayoenda kuiwakilisha Tanzania kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia
sana kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.
“Kubwa zaidi nimewaagiza
kuhakikisha kuwa wanaendeleza lugha ya Kiswahili, kwa sasa lugha ya Kiswahili
imekuwa ni bidhaa muhimu sana……..kiswahili ni muhimu sana na sasa Kiswahili
kinazungumzwa na zaidi ya watu milioni 500 duniani,” Amesema Balozi Mulamula.
Aidha, Waziri Mulamula
amewataka mabalozi kuhakikisha pamoja na mambo mengine, wanatekeleza majukumu
yao vyema na kujenga taswira nzuri ya Serikali.
Awali akiongea na
mabalozi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi Fatma Rajab aliwapongeza kwa uteuzi na kuwashauri kuendelea kujituma
katika kazi na kuleta mabadiliko ambayo Serikali imeyapanga hasa katika
diplomasia ya uchumi.
Balozi Fatma amewaasa
mabalozi waliomaliza mafunzo yao kuhakikisha kuwa wanatekeleza diplomasia ya
uchumi pamoja na diplomasia ya siasa kwa weledi ili kuleta manufaa ya Taifa.
Tarehe 27 Julai, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliwaapisha mabalozi 13 Ikulu jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Chuo cha
Diplomasia Balozi Abdulrahman Kaniki (aliyesimama) akiongea na mabalozi
waliomaliza mafunzo maalumu chuoni hapo jijini Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akiongea
na mabalozi waliomaliza mafunzo maalum katika Chuo cha Diplomasia Jijini Dar es
Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongea na
mabalozi waliomaliza mafunzo maalum katika Chuo cha Diplomasia Jijini Dar es
Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab katika
picha ya pamoja na mabalozi walimaliza mafunzo maalum katika Chuo cha
Diplomasia Jijini Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.