Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju akipokea barua kwa ajili ya kuwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Shule ya Kimataifa ya
Wakimbizi kujngwa Tanzania
Balozi wa Shirika la Elimu,
Utamaduni na Sayansi la Umoja wa Nchi za Kiarabu (The Arab League Educational, Cultural and Scientific Organization-ALECSO),
Mhe. Amir Fehri anakusudia kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Samia Suluhu Hassan ili aombe ridhaa ya kujenga shule ya kimataifa kwa
ajili ya wakimbizi-watoto nchini Tanzania.
Balozi huyo kijana (17) na maarufu
duniani, raia wa Tunisia alibainisha hayo alipokutana na kufanya mazungumzo
hivi karibuni na Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju.
“Naomba kupatiwa nafasi ya kukutana
na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan
ili kumuomba nasaha zake (moral support) katika kampeni yangu ya kusambaza
salaam ya Amani na Uvumilivu duniani, lakini zaidi kuomba ridhaa ya Mheshimiwa
Rais ili niweze kujenga shule yenye hadhi ya kimataifa kwa ajili ya wakimbizi-watoto
nchini Tanzania”, Balozi Fehri alisema.
Akielezea kuhusu matarajio yake
hayo, alisema, shule hiyo itakuwa inatoa vyeti vya kimataifa ili kuwasaidia
watoto hao ama kupata kazi nchini Tanzania au wakirejea katika nchi zao. Aidha,
Mhe. Fehri ameomba apatiwe nafasi ya kukutana na wanafunzi wa shule na vyuo
mbalimbali nchini Tanzania ili kuwaelimisha kuhusu unyanyasaji unaofanyika
mashuleni (bullying) na madhara yake pamoja na njia za kukabiliana na kadhia
hiyo.
Kwa upande wake, Balozi Kasyanju
alimpongeza Mheshimiwa Fehri kwa jitihada zake thabiti na kumshukuru kwa
mapenzi yake juu ya Tanzania, lakini zaidi kwa dhamira yake ya kujenga shule ya
wakimbizi nchini Tanzania.
Alisema ni kweli kwamba, Tanzania
imekuwa ikipokea wakimbizi kwa zaidi ya miaka 40 na moja ya changamoto kubwa
inayojitokeza ni pale ambapo wakimbizi hao wanaporejea katika nchi zao kwa
hiari, wanashindwa kujumuika ipasavyo na jamii zao kutokana na ukosefu wa elimu
stahiki itakayowawezesha pamoja na mambo mengine kupata ajira.
Balozi Kasyanju alitumia fursa hiyo
pia kumpongeza sana Balozi Fehri kwa umaarufu wake duniani kama vile; kuteuliwa
kuwa Balozi wa Francophonie ulimwenguni; kuweza kuchapisha vitabu 4 akiwa na
umri wa miaka 12, ambavyo vilimpa tuzo 25 za kimataifa katika fasihi kama Sanaa
na Barua za Tuzo ya Kimataifa ya Ufaransa, 2014; na kuzungumza lugha saba
(Kikurdi-Kifaransa-Kichina-Kiingereza-Kijerumani-Kiarabu-Kilatini) sifa
iliyomuwezesha kuwasiliana na viongozi wakubwa duniani.
Balozi
Fehri anashirikiana na Rais wa Tume ya Ulaya, kupitia Mfuko wa Amir Fehri (Amir Fehri
Foundation) kufungua shule ya kwanza ya Kimataifa huko Mossoul, Iraq. Shule hiyo
itakuwa ishara halisi ya elimu kwani itajengwa ndani ya kambi za wakimbizi na
itatoa nafasi mpya kwa watoto wote wakimbizi.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.