Monday, September 6, 2021

SERIKALI YAAINISHA VIPAUMBELE SEKTA YA AFYA

Na Mwandishi Wetu, Dar

Serikali imeainisha vipaumbele vitakavyonufaika na mradi wa sekta ya afya kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ufadhili wa Serikali ya Italia.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee Prof. Abel Makubi amevitaja hivyo alipokutana na madaktari kutoka Italia leo Jijini Dar es Salaam ambavyo ni mafunzo kwa wataalamu wa afya katika hospitali za mkoa, kanda na Taifa kwa ujumla, kununua vifaa vya matibabu vya kisasa, kujenga na kukarabati hospitali za kanda na taifa.

“Vipaumbele vingine ni kuanzisha na kuendeleza ushirikiano katika sekta ya afya kati ya Tanzania na Italia, kuimarisha mifumo ya maabara katika hospitali na kuendelea kupambana na ugonjwa wa Uviko 19 ikiwa ni pamoja na kuelimisha umuhimu wa chanjo” amesema Prof. Makubi.

Kwa upande wake Balozi wa Italia hapa nchini, Mhe. Marco Lombardi amelipongeza Shirika la Maendeleo la Italia kwa kutenga Euro 1,250,000 za msaada wenye manufaa kwa sekta ya afya nchini.

“Ushirikiano baina ya Tanzania na Italia ni wa muda mrefu na imara, naomba nikuhakikishie kuwa Italia itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta ya afya pamoja na sekta nyingine kwa maslahi ya pande zote mbili na kwetu sisi kama Italia huu ni mwanzo na tunaamini kuwa kupitia mradi huu uhusiano wetu utaendelea kuimarika zaidi,” amesema Balozi Lombardi.

Nae Dkt. Davide Bonechi, Daktari kutoka Kituo cha Taifa la Italia cha Afya Duniani amesema kuwa kupitia mpango wao wa kuboresha na kuimarisha sekta ya afya katika ukanda wa Afrika, mbali na Tanzania nchi nyingine zitakazo nufaika na mpango huo ni Kenya na Uganda.

 

“Lengo letu ni kuboresha sekta ya afya kwa ujumla pamoja na kuwaongezea uwezo wataalamu wa afya ili waweze kukabiliana na magonjwa mbalimbali yanayowapata binadamu,” amesema Dkt. Bonechi

Tarehe 3 September ujumbe wa wataalam wa afya kutoka nchini Italia uliwasili Tanzania kwa ziara maalum ya kutathmini na kufahamu mahitaji na vipaumbele vya Tanzania katika ya afya kwa hospitali zilizopo nchini.

Ujumbe wa wataalam wa afya kutoka nchini Italia unaongozwa na Dkt. Davide Bonechi, Dkt. Giulia Dagliana, pamoja na Dkt. Beatrice Borchi, wote wakitoka katika Kituo cha Taifa la Italia cha Afya Duniani.

Tanzania imekuwa ikishirikiana na Italia katika miradi mbalimbali ya afya hapa nchini ambapo ushirikiano rasmi katika sekta ya afya ulianza mwaka 1968 kupitia Shirika la Madaktari wa Italia-CUAMM-Doctors with Africa. Kuanzia wakati huo, Serikali ya Italia imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya afya hapa nchini kama vile miradi ya kupambana na utapiamlo, afya ya watoto wachanga, afya ya uzazi na kupunguza maambizi ya virusi vya ukimwi.

Serikali ya Tanzania imekuwa ikipokea madaktari wa binadamu na wataalamu wa dawa za binadamu kutoka Italia ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wa kutoa huduma za matibabu. 

Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi (kushoto) akielezea jambo katika kikao cha Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam


Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi (kulia) akiwaelezea vipaumbele vya Serikali sekta ya afya madaktari kutoka Italia. Madaktari hao wameambatana na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi.   


Mmoja kati ya madaktari kutoka Italia akieleza jambo wakati wa kikao


Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi (kushoto) akifafanua jambo wakati wa kikao


Kikao kikiendelea 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.