Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria Balozi Baraka Luvanda (wapili kushoto) akichangia hoja wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC).
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wizara ya Mambo ya Nje yaadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima amewaasa watumishi wa Wizara hiyo kutekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo haiwezi kufikiwa bila ya wao kutimiza wajibu wao kikamilifu.
Dkt. Mlima alitoa kauli hiyo leo wakati wa kikao cha pamoja na watumishi kujadili mafanikio na changamoto zinazoikabili Wizara hiyo kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. Kikao hicho kilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo itahitimishwa tarehe 23 Juni 2016.
Aliwataka watumishi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, ubunifu na kwa kushirikiana ili kuongeza kasi ya ufanisi wa Wizara. “Nataka Wizara yetu iwe moja kati ya taasisi za Serikali zinazotoa huduma bora kabisa hapa nchini, hivyo tekelezeni wajibu wenu bila hofu kwa kuwa haki na maslahi ya kila mtumishi yatazingatiwa”.
Dkt. Mlima alipongeza uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wa kupunguza kodi ya mapato ya watumishi (payee) kutoka asilimia 11 hadi 09 na kubainisha kuwa hiyo ni ishara ya wazi kwamba ahadi ya Mhe. Rais ya kuboresha maslahi ya watumishi itatimizwa.
Katibu Mkuu alihitimisha nasaha zake kwa kuwaomba watumishi kuongeza saa moja ya ziada siku ya kilele cha maadhimisho ya Wiki ya utumishi wa umma ili itumike kutoa huduma kwa wananchi jambo ambalo liliungwa mkono na watumishi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 23 Juni 2016.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.