TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India akutuna na Waziri Mahiga.
Tanzania imetakiwa kujifunza kutoka India kufuatia maendeleo
makubwa yaliyofikiwa na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali za viwanda,
teknolojia, TEHAMA, kilimo, usalama na afya. Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga
(Mb) alipokutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India, Bw. Amar
Sinha ofisini kwake
Waziri Mahiga alimweleza Katibu Mkuu huyo kuwa ushirikiano wa
Tanzania na India katika sekta ya uchumi unahitajika kwa kiasi kikubwa ili
Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli iweze
kufikia malengo yake ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka
2025.
Alisema kuna umuhimu wa Tanzania na India kushirikiana kwa
pamoja katika sekta za teknolojia, elimu, afya, elimu ya ufundi na TEHAMA ili
kuiongezea uwezo Serikali iweze kufikia malengo yake yaliyoainishwa kwenye Dira
ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2025.
Mhe. Waziri aliishukuru Serikali ya India kwa misaada ya
miradi ya maendeleo inayotoa kwa Tanzania. Misaada hiyo ni pamoja na ununuzi wa
matrekta kwa ajili ya kuboresha kilimo wenye thamani ya Dola za Marekani
milioni 40 unaosimamiwa na SUMA-JKT.
Msaada mwingine ni ujenzi wa miundombinu ya maji katika mikoa
ya Pwani na Dar es Salaam uliogharimu Dola za Marekani milioni 178.125. Aidha,
India imekubali kusaidia ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha maji kutoka Ziwa
Victoria hadi katika mikoa ya Shinyanga na Tabora utakaogharimu Dola za
Marekani milioni 268.35 pamoja na mradi mwingine wa maji utakaogharimu Dola za
Marekani milioni 92 utakaojengwa visiwani Zanzibar.
Awali, Bw. Sinha alifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima.
Wawili hao walisisitiza umuhimu wa nchi hizi mbili kuibua maeneo mapya ya
ushirikiano kwa ajili ya faida ya wananchi wa pande zote mbili. Maeneo
waliyoyainisha ni pamoja na kilimo, mafuta na gesi, madawa, afya, madini na
uchumi wa bahari (Blue economy).
Kuhusu uchumi wa Bahari, Balozi Mlima alieleza kuwa hilo ni
suala ambalo Mhe. Rais Magufuli analisisitiza kila siku katika vikao
mbalimbali. Alimuomba Katibu Mkuu huyo kuangalia uwezekano wa kusaidia kutafuta
wawekezaji wa uvuvi kwenye Bahari Kuu nchini ambayo kwa kauli ya Rais bado
haijafanyiwa kazi ipasavyo.
Kwa upande wake, Bw.Amar Sinha alisema kuwa ziara yake
imelenga kuimarisha mahusiano ya kihistoria yaliyopo kati ya Tanzania na India
pamoja na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano. Alisema India itaendelea
kushirikiana na Tanzania na inafurahishwa na mchango inaotoa ambao unasaidia
katika uchumi unaokuwa kwa wastani wa asilimia 7 kila mwaka.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 21 Juni 2016.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.