TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga ameupongeza Ubalozi wa Kuwait kwa kuwa wa kwanza kuitikia maombi yake ya kuchangia madawati kwa ajili ya shule za msingi na sekondari hapa nchini.
Pongezi hizo alizitoa jana wakati wa hafla ya kupokea madawati 300 ambayo Ubalozi huo uliahidi kuipa Serikali. Hafla ilifanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Tumeanza kupokea madawati kutoka kwa rafiki zetu, huu ni mwanzo tu, na wengine watafuatia na taarifa ya kila dawati litakalokuwa linapatikana nitaiwasilisha kwa Mhe. Waziri Mkuu. Dkt. Mahiga alieleza.
Mhe. Waziri aliwaambia wahudhuriaji wa hafla hiyo kuwa katika utekelezaji wa malengo ya milennia, Tanzania ilifanya vizuri katika baadhi ya maeneo hususan, elimu na afya ya mama na mtoto. Licha ya idadi ya watoto kuandikishwa mashuleni iliongezeka, bado kulikuwa na changamoto ya kuboresha ubora wa elimu na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia kama vile vitabu na majengo ya maabara na vifaa vyake.
Aliendelea kueleza kuwa baada ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kutangaza elimu bure, udahili mashuleni umeongezeka maradufu na hivyo kusababisha changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba mkubwa wa madawati.
“Kufuatia hali hiyo, Serikali imejipanga kutumia mbinu mbalimbali kutatua changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuwaomba marafiki zetu watusaidie. Hivyo, Kuwait imejitokeza kutusaidia na imeahidi kusaidia sio madawati tu bali, hata maeneo mengine yenye changamoto kwenye elimu”.
Kwa upande wake, Balozi wa Kuwait, Mhe. Jasem Al Najem alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya jitihada za Serikali yake kuunga mkono mkakati wa Rais Magufuli wa kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 23 Juni 2016.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.