Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia maadhimisho, kutoka kulia ni Bi. Mindi Kasiga na Bw. Arnold Mchemwa. ==================================================
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI
WA MAMBO YA NJE ASHIRIKI KUMBUKUMBU YA MAUAJI YA KIMBARI DHIDI YA WATUTSI
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.
Augustine Mahiga (Mb) ameshiriki maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya
kimbari nchini Rwanda dhidi ya Watutsi, yaliyoandaliwa na kuratibiwa na Ubalozi
wa Rwanda nchini chini ya Mhe. Balozi Eugene Kayihura yaliyofanyika
katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City
Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Waziri akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya kumbukumbu
hiyo alieleza namna mauaji hayo ya Kimbari yaliyotokea mwaka 1994 yalivyoleta
simanzi na majonzi kwa wananchi wa Rwanda, nchi majirani wa Rwanda ambao sehemu
yao ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, Afrika nzima na Duniani kwa ujumla kwakuwa mauaji hayo yalipoteza
maisha ya Wanyarwanda wasio na hatia zaidi ya laki nane (800,000) ndani ya siku
mia moja (100).
"Nilishuhudia madhara
ya mauaji hayo mwezi Agosti 1994, wakati huo nikiwa Mwakilishi wa Umoja wa
Mataifa nikisimamia masuala ya Wakimbizi nchini Rwanda, hali niliyoikuta siku
chache baada ya mauaji hayo ilikuwa ya kusikitisha na inayotisha kwakua ardhi
ilikuwa imejaa miili ya watu waliouawa wa rika zote sambamba na mito iliyokuwa
imefurika miili hiyo" alisema Waziri Mahiga.
Pia alitumia nafasi hiyo
kueleza kuwa ni wakati sasa mataifa ya Afrika yakaangalia namna ya kuendesha
masuala ya kisiasa na ulinzi katika hali ya amani pasipo kuharibu utulivu wa
Taifa husika ili kuepuka kuharibu maisha ya watu wasio na hatia pamoja na nguvu
kazi kubwa ambayo ndio tegemeo la kuleta maendeleo sambamba na kukuza uchumi.
Aidha Mhe. Mahiga alieleza
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais wa awamu ya tano Mhe. John Pombe
Magufuli itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Rwanda katika
jitihada za kupigania na kukemea mauaji
kama hayo na kuhakikisha hayajirudii tena nchini Rwanda wala kutokea tena
katika Taifa lolote barani Afrika na Duniani kwa ujumla. Alisema katika
mahusiano ya kidiplomasia, yanapotokea machafuko yanayo hatarisha amani yanaharibu
shughuli za kidiplomasia zinazoendelea baina ya mataifa husika.
Balozi wa Rwanda nchini
Tanzania Mhe. Eugene Kayihura naye alitoa pole kwa wahanga wote walionusurika
na mauaji hayo na pia akatoa wito kwa Wanyarwanda wote popote walipo kuzidi
kuwafariji na kuwa karibu na wahanga hao ili waweze kujisikia wapo na ndugu zao
na kuwa na matumaini na maisha ya sasa na ya baadae ili waweze kuendelea
kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuinua uchumi wa Rwanda.
"Jumuiya zote za Kinyarwanda
popote zilipo zihakikishe zinakuwa ndugu kwa wahanga walionusurika na mauaji
hayo na kuzidi kuwapa matumaini ya maisha ya baadae ili kuondoa kisasi dhidi ya
jamii iliyosababisha mauaji ya ndugu zao" Balozi Kayihura alisema
Vilevile Mhe. Kayihura alitumia
fursa hiyo kumshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John
Pombe Magufuli kwa kufanya ziara nchini Rwanda na kushiriki maadhimisho ya
kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari pamoja na kutembelea maeneo ya kihistoria ya
mauaji hayo akiwa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame mapema
mwezi April mwaka huu.
Maadhimisho ya kumbukumbu hiyo
hapa nchini yalihudhuriwa na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania, Wakuu
wa Mashirika ya Kimataifa, Jumuiya ya Kinyarwanda iliyopo nchini na Watanzania
wengine walioalikwa kushiriki maadhimisho hayo wakiwemo wanafunzi wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam na wa Sekondari ya Wasichana ya Jangwani.
Imetolewa na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar
es Salaam,
10 Juni 2016.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.