Baadhi ya wafanyabiashara kutoka
Tanzania walioshiriki Kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya lililofanyika jijini Nairobi
na kuhudhuriwa na Marais wa nchi za
Kenya na Tanzania
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
ameihakikisha jumuiya ya wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya kuwa Serikali anayoiongoza
itaendelea kuchukua hatua kuondoa vikwazo vya kibiashara vilivyopo ili kuimarisha
sekta binafsi na hivyo kukuza uchumi wa nchi hizo.
Mhe. Samia alikuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa
Kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya lililofanyika jijini Nairobi
nchini Kenya na kuhudhuriwa kwa pamoja na Rais Samia na mwenyeji wake Rais wa
Jamhuri ya Kenya Me. Uhuru Kenyatta.
Amesema Serikali za nchi hizo zitahakikisha kunakuwa na sheria
nzuri, uwazi, mifumo ya kodi inayoeleweka na mifumo thabiti ya Mahakama itakayoshughulikia
kesi za biashara kwa haraka na uwepo wa mazingira mazuri ya uwekezaji katika
nchi hizo
Amesema kufanyika kwa Kongamano hilo kumewezesha kuwepo kwa
majadiliano ya pamoja kati ya Sekta Binafsi na Serikali, wafanyabiashara wao
kwa wao na kuelezea kuwa ni kitu kizuri kwani kinachangia juhudi za kuinua na
kuimarisha ukuaji wa biashara na sekta binafsi kwa maendeleo ya nchi zote mbili
Mhe. Rais Samia amesema Tanzania itaendelea kuchukua hatua
mbalimbali katika kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji na
kufanya biashara ili kuwawezesha wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa
amani na utulivu kwani Sekta binafsi ni muhimu katika ukuzaji wa uchumi kwa kutoa
ajira, kuleta masoko, hufungua fursa mbalimbali na kuchagiza moyo wa
ujasiriamali miongoni mwa wananchi.
Amesema Tanzania imedhamiria kwa dhati kuona Sekta binafsi
imara inayoweza kukabiliana na changamoto za uchumi za dunia kupitia
uanzishwaji wa viwanda na hivyo kuongeza ubora wa bidhaa zinazozalishwa nahivyo
kutoa ajira na utajiri wananchi kitu ambacho wafanyabiashara wanatakiwa
kukifikia.
Awali akizungumza katika Kongamano hilo Rais wa Jamhuri ya
Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta ameitaka jumuiya ya wafanyabiashara wa Tanzania na
Kenya kuchangamkia fursa za kibiashara
ambazo hazijafikiwa katika nchi hizo ili kukuza biashara katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki na kuleta maendeleo kwa watu wake.
Amewataka Mawaziri wanaohusika na biashara kukutana na kutatua
changamoto zinazokwamisha ukuaji wa biashara katika nchi hizo ili kukuza uchumi
na kuinua maisha ya wananchi wa nchi hizo na kuongeza kuwa ana imani kuwa hayo
yote yakifanyika kwa pamoja bila ya kushindana ni wazi kuwa watakaoibuka
washindi ni wananchi wa nchi hizo.
Amesema wawekezaji na wafanyabiashara wa Tanzania wanaweza
kwenda kuwekeza nchini Kenya bila ya kudaiwa viza za biashara ili mradi wafate
sheria kanuni na taratibu zilizopo. Amewagiza Mawaziri wanaohusika na mgogoro
uliopo eneo la mpaka la Taveta hadi Namanga wakutane ili kuona nanma ya kuondoa
changamoto na kutoa wiki mbili mahindi yaliyokwama huko yawe yameondolewa.
Mhe. Kenyatta pia amewataka Mawaziri wa Afya katika nchi hizo
kukutana na kuangalia namna ya kuondoa changamoto iliyopo sasa upimaji
wa virusi vya Corona na kutaka vyeti vilivyotolewa katik nchi moja vitambuliwe
katika nchi nyingine.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.