Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Ishirini na Sita (26) wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) unaofanyika tarehe 30 na 31 Mei, 2024 kwa njia ya mtandao huku ujumbe wa Tanzania ukiwa jijini Dodoma.
Pamoja na masuala mengine mkutano huo umejadili juu ya maboresho ya taasisi na kuongezeka kwa ushirikishwaji wa taasisi hizo kikanda pamoja na taarifa ya fedha na utawala.
Akichangia katika mkutano huo, Balozi Mussa ameipongeza Sekretarieti ya IORA kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za kikanda na kimataifa kwa maslahi mapana ya ukanda huo wa IORA.
Aidha, ameziomba nchi wanachama kuendelea kushirikiana ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotishia usalama katika shughuli za majini na bahari kwa ujumla ikiwemo uharamia, usafirishaji haramu wa bidhaa na dawa za kulevya pamoja na uharibifu wa mazingira.
Kadhalika amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama kushirikiana katika kutekeleza maeneo makuu manne ya kipaumbele katika IORA ambayo yatasaidia kukabiliana na changamoto ya utafutaji na uokozi pale ajali za majini zinapotokea.
Maeneo hayo ni pamoja na Utafutaji na Uokoaji, Kukabiliana na Uhalifu wa Majini, Kubadilishana Taarifa na kuimarisha Ulinzi na Usalama katika ukanda wa Bahari ya Hindi.
Kadhalika, Balozi Mussa ametoa rai kwa Sekretarieti ya IORA kuendelea kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali kutoka nchi wanachama pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa michango kwa wakati itakayowezesha utekelezaji wa majukumu ya IORA kwa tija kwa maslahi ya nchi wanachama.
======================================
Ujumbe wa Tanzania ukifatilia mkutano. |
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania ikifuatilia mkutano. |
Picha ya pamoja. |
Mkutano ukiendelea. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.