Tuesday, May 28, 2024

MIRADI MIKUBWA YA VITEGA UCHUMI KATIKA BALOZI YAJA - WAZIRI MAKAMBA


 


Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeeleza kuwa inaratibu na kusimamia Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo katika viwanja vya Balozi za Tanzania nje wakati wa uwasilishaji wa makadirio ya bajeti ya Wizara bungeni jijini Dodoma tarehe 28 Mei, 2024.

Ufafanuzi huo umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) ambapo ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, Wizara iliidhinishiwa jumla ya shilingi 17,887,608,000 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi 8,400,000,000 ni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo kwenye balozi zetu.

Hadi kufikia mwezi Aprili, 2024 Wizara imepokea na kutumia fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali kiasi cha shilingi 16,762,726,958.61 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi 4,780,120,117 zimeelekezwa katika ukarabati wa majengo na ununuzi wa samani kwenye balozi sita (6) za Tanzania nje ya nchi ambazo ni Beijing, Geneva, Ottawa, Brussels, Stockholm na Windhoek. Wizara pia inaendelea na ukarabati wa jengo la zamani la ubalozi wa Tanzania Washington D.C.

Vilevile, Wizara inaendelea na mradi wa ukarabati wa majengo manne ya Ubalozi wa Tanzania Pretoria, Afrika ya Kusini. Mradi huu unahusisha jengo la ubalozi; makazi ya balozi; makazi ya mkuu wa utawala; na makazi ya mwambata utawala. 

Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya Dola za Marekani 523,561.43 sawa na shilingi 1,293,950,000. 


Kwa upande wa Ubalozi wa Tanzania Addis Ababa, Ethiopia, Wizara imesaini mkataba na Kampuni ya ALLURE CONSTRUCTION PLC ya Addis Ababa kwa ajili ya uendelezaji wa viwanja vya Ubalozi kwa gharama ya Shilingi 1,164,856,025 pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT). Mradi huu umeshaanza ujenzi wa uzio na unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka wa fedha 2024/25. 224.

Vilevile, Wizara imeingia Makubaliano ya ubia na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Kitega Uchumi katika Ubalozi wa Tanzania Nairobi. Mradi huo unahusu kuendeleza kiwanja kilichopo katika eneo la Upperhill jijini Nairobi kwa kujenga majengo pacha ya ghorofa ishirini na mbili (22).

Wizara pia kwa kushirikiana na Mfuko huo wa Hifadhi wa NSSF imekamilisha maandalizi ya nyaraka za kisheria kwa mradi wa Ujenzi wa jengo la Kitega Uchumi Kinshasa DRC. Utekelezaji wa mradi huo utahusisha ujenzi wa jengo la ghorofa ishirini na tano (25).

Mradi mwingine ni; pamoja na vitega uchumi katika viwanja vya Serikali vilivyopo katika balozi za Tanzania Kampala, Uganda, Abuja Nigeria na Lusaka Zambia. 

Katika utekelezaji wa miradi hiyo, Wizara inakamilisha taratibu za kupata washauri elekezi, kufanya upembuzi yakinifu, kupima udongo, kufanya marejeo ya michoro ya majengo husika, kupata vibali vya ujenzi kutoka mamlaka za miji hiyo na kuanza ujenzi.

Aidha, Waziri Makamba ameeleza kuwa katika kuweka mpango madhubuti wa kuendeleza viwanja na milki zake zilizopo nje ya nchi, Serikali imeunda Timu ya Wataalam, ikiwa na jukumu la kuishauri Serikali namna bora ya kuendeleza na kusimamia milki hizo nje ya nchi. 

Maandalizi yanaendelea ya kumpata Mshauri Elekezi mwenye uzoefu wa Kimataifa katika Masuala ya Milki atakayeandaa nyaraka mbalimbali za uwekezaji, miongozo pamoja na kuishauri Serikali namna bora ya uendelezaji wa milki hizo kulingana na maeneo ya Balozi husika.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.