Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limeridhia na kupitisha makadirio ya Mapato
na Matumizi ya Shillingi Bilioni 241 kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 Jijini Dodoma leo Mei 28, 2024
Awali akiwasilisha bungeni hotuba yake, Waziri Mhe. January Makamba amelieleza Bunge kuwa katika mwaka ujao wa fedha, Wizara imejipanga kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa nguvu mpya ili kuchochea Uwekezaji, Utalii, na Biashara pamoja na kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa maendeleo ya Nchi.
Kadhalika amesema, Wizara itaendelea kukuza ushirikiano wa uwili wa kimkakati pamoja na kuhakikisha ushiriki wenye tija wa Tanzania katika jumuiya na mashirika ya kikanda na kimataifa ili kulinda maslahi mapana ya taifa; pamoja na kustawisha diplomasia ya kisasa na kujenga uhusiano wa karibu na nchi washirika.
Amesema kipaumbele kingine kwa Wizara ni kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi, kuimarisha utawala bora na rasilimaliwatu pamoja na kutekeleza miradi ya ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya ofisi, makazi ya watumishi na vitega uchumi katika Balozi za Tanzania na makao makuu.
Mhe. Makamba amelifahamisha Bunge kuwa, Wizara imekamilisha rasimu ya awali ya Mkakati wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ambao umeainisha maeneo saba ya kipaumbele ambayo Wizara itayatilia mkazo katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ikiwemo Kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje; na Kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi.
Maeneo mengine ni kuvutia watalii kuja Tanzania; Kutafuta misaada na mikopo ya masharti nafuu kutoka nje; Kutafuta fursa za ajira na masomo kwa Watanzania nje ya nchi; Kujenga taswira nzuri ya nchi yetu kimataifa na Kujenga uwezo wa kitaasisi wa Wizara, na Wizara na Taasisi nyingine kusimamia vizuri utekelezaji wa Mkakati wa Diplomasia ya Uchumi.
Kuhusu Diaspora, Mhe. Makamba amesema Wizara inatambua mchango wao katika maendeleo ya nchi na kwamba Serikali imejumuisha masuala ya Diaspora katika mapitio ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 na Sera Mpya ya Ardhi ya 2024 na kutoa Hadhi Maalum (Special Status) kwa Raia wa Nchi Nyingine Wenye Asili ya Tanzania ili kuwapa haki na upendeleo mahsusi.
Amesema katika kutekeleza jukumu hilo, mwezi ujao, Serikali itawasilisha katika Bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria utakaokuwa na marekebisho madogo ya Sheria za Uhamiaji Sura ya 54 na Sheria ya Ardhi Sura ya 113 nia ikiwa ni kukamilisha utoaji wa Hadhi Maalum kwa Raia wa Nchi Nyingine Wenye Asili ya Tanzania.
Katika medani za kimataifa na kikanda Mhe. Makamba amelijulisha Bunge kuwa, sauti ya Tanzania imeendelea kusikika na kukubalika ambapo kuanzia mwezi Agosti, 2024 Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), nafasi ambayo itaiwezesha Tanzania kuratibu na kuongoza majadiliano na maamuzi yote yanayohusu masuala ya siasa, ulinzi na usalama.
Aidha, nafasi hii itaimarisha ushawishi wake katika ukanda wa SADC katika masuala haya hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa Waasisi wa SADC walioshiriki kwa hali na mali katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.
Aidha, Mhe. Makamba ametumia jukwaa hilo kuwahimiza watanzania wenye sifa, wakiwemo Wabunge kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika taasisi za kikanda na kimataifa huku akimpongeza Mhe. Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile (Mb.) kwa kujitokeza kuwania nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani – Kanda ya Afrika.
Mkuu wa Itifaki, Balozi Yusuph Mndolwa (kushoto) akiwa Bungeni na wageni wengine waalikwa walioshiriki uwasilishwaji wa Bajeti ya Wizara Bungeni jijini Dodoma |
Sehemu ya Mabalozi na Wakuu wa Mashirikia waliopo nchini wakifuatilia uwasilishwaji wa Bajeti ya Wizara |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.