Mkutano wa 32 wa Baraza la Mawaziri la kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango umefanyika leo tarehe 05 Novemba, 2021 jijini Arusha, Tanzania.
Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ambaye ameambatana na; Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohammed Mchengerwa, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda- Zanzibar Mhe. Omar Said Shaaban, na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe.
Viongozi wengine walioshiriki katika mkutano huo ni pamoja na; Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine, Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda – Zanzibar, Dkt. Islam Seif Salum; na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Harshil Abdallah, na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa,.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri pamoja na masuala mengine umejadili na kutoa maamuzi mbalimbali ya kisera katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Baadhi ya agenda zilizojadiliwa ni; Taarifa ya utekelezaji wa maamuzi na maelekezo yaliyopita ya Baraza la Mawaziri la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango; Hali ya ulipaji wa michango ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Nchi Wanachama; Mapendekezo ya maeneo ya vipaumbele vya jumla na mahsusi vya Jumuiya kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023; na taarifa ya kadi ya alama (score card) ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2020.
Agenda nyingine ni
pamoja na; Taarifa ya andiko la Mkutano wa Kazi (high level retreat) wa Wakuu wa
Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu hali iliyofikiwa katika
kuondoa Vikwazo Vya Kibiashara Visivyo Vya Kikodi (NTBs) katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki; na Mapitio ya Sheria ya Uondoshaji Vikwazo Vya Kibiashara
Visivyo Vya Kikodi (NTBs) ya Kikanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na
Ukamilishwaji wa Kanuni za utekelezaji wa Mkataba.
Mkutano wa 32 wa Baraza la Mawaziri la kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango umefanyika ana kwa ana na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Kenya, Jamhuri ya Burundi, na Jamhuri ya Uganda. Wajumbe wengine kutoka Jamhuri ya Rwanda na Jamhuri ya Sudan Kusini wameshiriki kwa njia ya mtandao.
======================
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania |
Sehemu nyingine ya ujumbe kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania |
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Burundi |
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Kenya |
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Uganda |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.