Mkutano wa Nane wha Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) umefunguliwa rasmi jijini Dakar nchini Senegal na kuhutubiwa na wenyeviti wenza kwa njia ya mtandao na moja kwa moja.
Awali mwenyekiti mwenza na Rais wa Senegal Mhe. Macky Sall alihutubia mkutano katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Abdou Diouf ulioko jijini Dakar.
Baadaye mwenyekiti mwenza ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping alihutubia mkutano huo kwa njia ya mtandao akiwa nchini China.
Mkutano huo wenye kauli mbiu ya “kuimarisha ubia wa China na Afrika na kukuza maendeleo endelevu na kujenga jamii ya China-Afrika yenye kesho ya pamoja katika zama mpya” unahudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya China Mhe. Wang Yi na Mawaziri wengine wa Mambo ya Nje akiwamo Balozi Liberata Mulamula .
Katika ufunguzi wa Mkutano huo ulihutubiwa pia kwa njia ya mtandao na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Felix Tshisekedi, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Rais wa Visiwa vya Comoro Mhe. Asumani Azali, Rais wa Umoja wa Afrika Mhe. Ndiya Musa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Getterez.
Viongozi hao wote kwa umoja wao wameelezea kuridhishwa kwao na ushirikiano imara uliopo kati ya China na Afrika na kupongeza juhudi zozote zinazochukuliwa katika kuimarisha zaidi uhusiano huo.
Viongozi hao pia wameelezea juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na nchi na viongozi wao katika harakati za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19 ikiwa ni pamoja na kuhakikisha maelfu ya watu wa Afrika wanapatiwa chanjo kama njia mojawapo ya kukabiliana na virus hivyo.
Pia wameongelea juu ya hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na nchi husika katika kuhakikisha mabadiliko ya hali ya hewa hayaleti changamoto zaidi kwa nchi zao.
Pamoja na mambo mengine viongozi hao wamesisitiza juu ya umuhimu wa kuendelea kuzingatia uimarishaji na ukuzaji wa demokrasia, haki za binadamu, usawa wa kijinsia na utawala wa sheria katika nchi zao
Katika hotuba yake rais wa China aliahidi kutoa dozi bilioni moja za chanjo ya covid 19 kwa nchi za Afrika ikiwa ni ziada ya dozi ambazo zimeshatolewa na China kwa nchi hizo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.