Na Waandishi wetu, Dar
Serikali ya Tanzania imezihakikishia kampuni za Uswisi
mazingira salama ya biashara na uwekezaji nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipokutana kwa
mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi.
Patricia Daanzi katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Balozi Mulamula amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita
imetilia mkazo katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni
pamoja na kupitia sheria na kuondoa baadhi ya kodi zilizokuwa ni kikwazo kwa
wawekezaji.
“Serikali imepitia sheria zetu na kuweza kuondoa kodi
zilizokuwa kero............na kupitia pia sheria ya uwekezaji kwa lengo la kuboresha
zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini,” amesema Balozi Mulamula
Balozi Mulamula ameongeza kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi pamoja na ujumbe wake wameoneshwa kuridhishwa na juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na kuahidi kuendelea kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uswisi kuja kuwekeza Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi amesema pamoja na mambo mengine,
wamejadiliana mazingira ya biashara na uwekezaji na vitu ambavyo kampuni za Uswisi
zinahitaji ili kuwekeza zaidi Tanzania.
“Tumeridhishwa na juhudi za Serikali ya Tanzania za
kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na tumemhakikishia Waziri Mulamula
kuwa tutaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara kutoka Uswisi kuja kuwekeza
Tanzania,” amesema Bi. Daanzi
Bi. Daanzi ameongeza kuwa mbali na kuwahamasisha
wafanyabiashara na wawekezaji pia kuna maeneo ya ushirikiano ambayo Serikali ya
Uswisi itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha maisha ya
watanzania.
Katika tukio jingine, Balozi Mulamula amekutana na
kufanya mazungumzo na Balozi wa China Nchini Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo
za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao pamoja na mambo mengine, wamejadili kuhusu
Mkutano wa nane (8) wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na
Afrika (FOCAC) unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 - 30 Jijini Dakar nchini
Senegal.
Katika Mkutano huo Rais wa China Mhe. Xi Jinpign anatarajiwa kuhutubia kwa njia ya Mtandao
ambapo Tanzania itawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.
Mkutano huo utawajumuisha viongozi na wawakilishi
kutoka Bara la Afrika na China ambapo utatoa fursa ya viongozi hao kujadili na
kuangalia jinsi ambavyo China ilivyotekeleza hatua za ushirikiano kwa kipindi
cha miaka mitatu 2018 - 2021 kwenye
maeneo ya ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda barani Afrika, ujenzi wa
miundombinu ya nishati, usafirishaji, habari na mawasiliano, kukuza wigo wa
biashara kati ya China na mataifa ya Afrika.
Maeneo mengine ni kampeni ya mapinduzi ya kijani,
mpango maalum wa mafunzo ya ufundi, kuboresha sekta ya Afya, ulinzi na usalama
na ushirikiano katika masuala ya habari, utamaduni sanaa na michezo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi
Bi. Patricia Daanzi akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini
Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi zaadi ya picha Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi, Balozi wa
Uswisi Nchini Mhe. Didier Chassot, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika
katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Swahiba
Mndeme. Wengine ni ujumbe ulioambatana na Bi. Daanzi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Liberata Mulamula akimkaribisha Balozi wa China Nchini Mhe.
Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Balozi wa China Nchini Mhe. Chen Mingjian akiteta jambo
na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata
Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.