Mkutano wa kujadili mapendekezo ya miradi ya uwekezaji kutoka kwa Watanzania wanaoishi nje (Diaspora) umefanyika kwa njia ya mtandao leo tarehe 09 Novemba 2021 ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa Mdahalo wa Kitaifa kuhusu “Umuhimu wa Diplomasia ya Uchumi na Ushirikiano wa Kimataifa katika Kuwaletea Wananchi Maendeleo” uliofanyika tarehe 06 Novemba 2021.
Mkutano huo ambao umeratibiwa
na kuongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya
Diplomasia ya Uchumi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Edwin Rutageruka umepokea mapendekezo ya miradi 12 iliyowasilishwa na Watanzania hao ambao ni Bw. Hassan Ng’anzo wa Norway,
Dkt. Swabury Alawi wa Ujerumani na Bw. Patrick Dyauli wa Uingereza.
Wakiwasilisha mapendekezo ya
miradi hiyo ambayo imejikita kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za Afya,
Mazingira, Nishati, Madini, Ujenzi na Uchukuzi, Watanzania hao ambao pia ni
wamiliki wa Kampuni za ANICO, ESSB na SE
Holdings, wameiomba Serikali kuwapatia ushirikiano wa kutosha ili kuwezesha
miradi hiyo ambayo itatekelezwa kwa kushirikiana na wawekezaji wa uhakika, kuja nchini kwani ina manufaa makubwa kiuchumi na itatengeza ajira
kwa Watanzania.
Kwa upande wake, Balozi
Rutageruka amewashukuru na kuwapongeza Watanzania hao kwa hatua hiyo ya
kizalendo ya kuwa tayari kuja kuwekeza nchini na kuahidi kuendelea kutoa
ushirikiano watakaohitaji ili kufanikisha lengo hilo. Kadhalika, amewahimiza Diaspora wengine kujitokeza kwa wingi kuja kuwekeza au kuleta wawekezaji na wafanyabiashara wenye tija nchini.
Mkutano huo pia umewashirikisha
wadau muhimu zaidi ya 20 kutoka ndani na nje ya nchi akiwemo Balozi wa Tanzania
nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi, Balozi wa Tanzania nchini Kenya,
Mhe. Dkt. John Simbachawene, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahamoud
Thabit Kombo, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Diapora katika Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago, Mwakilishi
wa Balozi wa Tanzania nchini Sweden na Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini
Marekani.
Wadau wengine walioshiriki ni kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Nishati, Wizara ya Madini, TIC, ZIPA na TANTRADE.
Balozi Rutageruka akimsikiliza Dkt. Swabury Alawi, Mtanzania anayeishi Ujerumani wakati wa mkutano wa kujadili mapendekezo ya miradi ya uwekezaji kutoka kwa Watanzania wanaioshi nje (Diapora) |
Mkutano ukiendelea huku Maafisa kutoka Idara ya Diplomasia ya Uchumi, Bw. Magabilo Murobi (kulia) na Bw. Herman Berege (kushoto) wakinukuu masuala muhimu yanayojadiliwa. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.