Wednesday, October 13, 2021

Balozi Bana awapokea Wanajeshi watakao shiriki Michezo ya Amani na Mshikamano ya Kijeshi, nchini Nigeria.


Balozi wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana amewapokea Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliowasili nchini humo kujumuika na wanamichezo wengine kutoka nchi mbalimbali za Barani Afrika kushiriki michezo ya Amani na Mshikamano ya Kijeshi ya Sahel Barani Afrika iliyoandaliwa na Taasisi ya Michezo ya Kijeshi Afrika (Organization of Military Sports in Africa - OSMA) Sahel Countries Military Games for Peace and Solidarity.

Sambamba na kuwajengea utimamu wa mwili na akili washiriki Wanajeshi wanaoshiriki michezo hii, michezo hiyo pia inalenga kujenga umoja, ushirikiano na udugu miongoni mwao hasa katika kupambana na vitendo vya uhalifu katika eneo la Sahel na kuleta amani katika eneo hilo ambalo limekuwa na matatizo ya uasi na changamoto nyingine za kiusalama. 

Akizungumza wakati wa mapokezi ya Wanajeshi hao Balozi Bana ameongeza kusema ushiriki wa Tanzania katika michezo hiyo kutasaidia kuimarisha na kuongeza ushirikiano katika masuala mbalimbali ikiwemo kubadilishana taarifa katika eneo la ulinzi na usalama na nchi zingine za Afrika

“Wakati huu dunia inapokabiliana na changamoto mbalimbali za kiusalama ni muhimu pia kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuendelea kuimarisha mahusiano na vyombo vingine vya nje ya nchi ili kwa pamoja kuweza kushirikiana katika kukabiliana na changamoto hizo.” Balozi Bana. 

Michezo hiyo ilifunguliwa Oktoba 11, 2021 jijini Abuja, na Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu Mhe. Dkt. Ogbonanya Onu wa Serikali ya Shirikisho la Nigeria. Katika ufunguzi Dkt. Onu alibainisha kuwa michezo hiyo ni muhimu kwa sasa kwa kuzingatia hali ya usalama ya sasa inayokabili taifa hilo.

Michezo hiyo inatarajiwa kuudhuliwa na washiriki takribani 327 kutoka nchi 14 zikiwemo Nigeria, Burkina Faso, Cameroon, Congo Brazzaville, Guinea Conakry, Kenya, Mali, Tanzania na Chad. Michezo mingine itakayofanyika ni mpira wa miguu na gofu.
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wanariadha wa JWTZ wanaoshiriki michezo ya Amani na Mshikamano ya Kijeshi ya Sahel Barani Afrika



Chuo Kikuu cha Port Harcourt cha nchini Nigeria chaonesha nia ya kufundisha Lugha ya Kiswahili
Balozi wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana ameeleza kuwa Chuo Kikuu cha Port Harcourt kimeonesha utayari wa kuanza kufundisha tena somo la lugha ya Kiswahili kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Slaam kama ilivyokuwa halo awali. 

Balozi Bana amebainisha hayo baada ya kutembelea na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Chuo cha Port Harcourt Prof. Owunari Abraham Georgewill, ambapo pamoja na masuala mengine walijadili kuhusu uwezekano na namna ya kuanza kufundisha somo la Kiswahili katika Chuo hicho.

“Taratibu zimeanza kufanyika ili kukamilisha makubaliano ambayo yatapelekea somo la Kiswahili kufundishwa chuoni hapo, hii itatoa fursa kwa Walimu wa Kiswahili wa Tanzania kufundisha somo hilo katika chuo hicho, pia ni fusa muhimu katika kukuza lugha ya Kiswahili ambayo ni sehemu ya Utamaduni wa Mtanzania” Amesema Balozi Bana.

Miongo minne iliyopita Chuo kikuu cha Port Harcourt kilikuwa kikifundisha somo la Lugha ya Kiswahili. Hata hivyo kutokana na sababu ambazo hazikuwekwa wazi, Chuo hicho hakikuendelea kufundisha somo hilo. Wakati huohuo Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Taasisi ya vyombo vya Habari vya Serikali ya Shirikisho la Nigeria (inayojulikiana kama Voice of Nigeria-VON) wameingia makubaliano ya kukuza lugha Kiswahili nchini humo. 

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa ziara ya Mkurugenzi wa TBC Dkt. Ayubu Rioba Chaha aliyofanya nchini Nigeria ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa VON Bw. Osita Okechukwu. Katika mazungumzo hayo TBC ilikubali kushirikiana na VON kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili VON katika uandaaji na utangazaji wa vipindi vya Kiswahili ikiwemo kubadilishana program, wataalamu na ujuzi katika sekta ya utangazaji.

Mbali na kutembelea VON Dkt. Ayubu Rioba Chacha akiambatana na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana na Maafisa wengine wa Ubalozi pia alitembelea; Federal Radio Cooperation of Nigeria (FRCN), Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria na Nigeria Television Authority (NTA)

VON tayari ina kipindi maalumu kinachoendeshwa kwa lugha ya Kiswahili ambacho kilianzishwa mwaka 1969 na iliyokuwa Federal Radio Corporation of Nigeria (FRCN). Matangazo kwa lugha ya Kiswahili yalianzishwa ili kuwafikia wasikilizaji wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini wakati wa juhudi za kupigania ukombozi wa Afrika.
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana (kulia) na Mkuu wa Chuo cha Port Harcourt Prof. Owunari Abraham Georgewill wakiwa katika picha ya pamoja.
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana (kulia) wakibadilishana nyaraka na Mkuu wa Chuo cha Port Harcourt Prof. Owunari Abraham Georgewill
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana (wa kwanza kulia) na Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayubu Rioba Chacha (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria walipotembelea Wizara hiyo.
Mkutano ukiendelea baina ya Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayubu Rioba Chacha, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana, Maafisa wa Ubalozi na Watendaji wa Nigeria Television Authority (NTA) walipotembelea Taasisi hiyo.
Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayubu Rioba Chacha (kulia) na Mkurugenzi wa Voice of Nigeria Bw. Osita Okechukwu (kushoto) wakiwa na nyaraka baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano jijini Abuja, Nigeria.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.