Makamu
wa Rais na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Shell ya Uholanzi mwenye makazi
yake Tanzania, Bw. Jared Kuehl alitembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Uholanzi
na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Irene Kasyanju
hivi karibuni.
Katika mazungumzo
hayo, Pamoja na mambo mengine, Bw. Kuehl alimhakikishia Balozi Kasyanju utayari
na dhamira ya dhati ya Kampuni yake kuendelea kuwekeza Tanzania kwa kutekeleza
Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (Liquified Natural Gas - LNG) kwa
kushirikiana na Kampuni ya Equinor ya Norway.
Bw.
Kuehl alisema anafurahishwa na ushirikiano ambao Ofisi yake (Shell Exploration
& Production Tanzania Ltd) imekuwa inapata nchini Tanzania na kwamba hatua zinazochukuliwa
na Serikali hivi sasa ni za kuridhisha wakati kampuni hiyo inapojiandaa kufanya
majadiliano ya pamoja yanayolenga kufanikisha utekelezaji wa Mradi wa LNG.
“Kimsingi
Kampuni ya Shell imefurahishwa na uamuzi wa Serikali kukubali Kampuni hizi
mbili ziungane na zifanye kazi pamoja na namna inavyoandaa taratibu zinazohusu
masuala ya kisheria na kiufundi, udhibiti wa Mradi pamoja na masuala ya kikodi
yanayohusu Mradi huo wa NLG nchini”, Bw. Kuehl alisema.
Kwa
upande wake, Balozi Kasyanju alifurahishwa na ujio wa Kiongozi huyo na kutumia
fursa hiyo kumshukuru kwa kufika Ubalozini, kuishukuru Shell na Equinor
kuwekeza Tanzania, na kuelezea matarajio yake kwamba uwekezaji huo utakuwa ni
wa manufaa kwa pande zote mbili. Alimhakikishia Makamu wa Rais na Mwenyekiti
Mtendaji huyo ushirikiano endelevu wa Ubalozi wake na wa Serikali nzima kwa
ujumla. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.