Friday, October 8, 2021

TANZANIA, CZECH ZAAHIDI KUIMARISHA BIASHARA NA UWEKEZAJI

 Na Mwandishi wetu, Dar

 

Katika jitihada za kukuza na kuendeleza diplomasia ya uchumi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Czech zimeahidi kukuza na kuimarisha sekta ya biashara na uwekezaji.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek wakati alipokutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk leo katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam. 

Mhe. Staŝek amesema kuwa wamejadili masuala mbalimbali ya kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Czech hasa katika sekta ya biashara na uwekezaji wa viwanda hapa nchini………..”na leo nimeambatana na wafanyabiashara mbalimbali kutoka Czech ambao wamekuja kuangalia fursa za biashara zinazopatikana hapa Tanzania” amesema Mhe. Staŝek.

“Pia tunajitahidi kuleta teknolojia mpya hapa Tanzania kuinua uchumi, ambapo tunaamini itasaidia kutangaza fursa mbalimbali katika sekta ya biashara na uwekezaji,” Ameongeza Mhe. Staŝek

Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amesema katika mazungumzo yake na Waziri wa Jamhuri wa Czech Mhe. Staŝek yamejikita zaidi katika kukuza uhusiano wa uchumi hasa masuala ya biashara na uwekezaji.

Leo Mhe. Waziri ameambata na ujumbe wa wafanyabiashara waliokuja kujione fursa mbalimbali hapa nchini ili kuinua sekta ya biashara na uwekezaji…………..”leo pia watakuwa na mkutano ambao utawakutanisha na wafanyabiashara wa Tanzania ili kuona fursa za ushirikiano baina ya Tanzania na Czech,” Amesema Balozi Mbarouk.

“Tumeongelea suala la kuongeza uhusiano katika sekta ya elimu kwa kutoa fursa za masomo kwa wanafunzi wa Tanzania kwenda kusoma Czech ambapo wamekubali na kuahidi kuongeza nafasi za masomo kwa wanafunzi wa Tanzania ili kutoa fursa ya watanzania wengi kunufaika na elimu,” Ameongeza Balozi Mbarouk.

Pia viongozi hao wamejadili suala la kukuza sekta ya utalii hapa nchini ambapo Czech ipo katika mchakato wa kuanzisha safari ya ndege ya kuja Tanzania moja kwa moja ili kukuza na kutangaza Utalii lakini pia kukuza biashara kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Kadhalika, Balozi Mbarouk amemuahidi Mhe. Staŝek kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuhakikisha inalinda na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina yake na Jamhuri ya Czech kwa kuwa uhusiano wa mataifa hayo mawili ni wa muda mrefu na wenye maslahi ya mataifa yote mawili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek akiongea na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) wakati walipokutana leo kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek wakati walipokutana leo kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Majadiliano baina ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek akiongea na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) yakiendelea wakati wa mazungumzo leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Majadiliano baina ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek akiongea na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) yakiendelea wakati wa mazungumzo leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek akiongea akipokea zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro kutoka kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) leo Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) leo Jijini Dar es Salaam



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.