Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine leo tarehe 27 Oktoba 2021 ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC) kati ya Tanzania na Rwanda kwa Ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika katika Ukumbi wa Wakimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine Mkutano wa Makatibu Wakuu umepitia na kuthibitisha agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwao na Wataalam kabla ya agenda hizo kuwasilishwa na kupitishwa kwenye Mkutano wa Mawaziri unaotarajiwa kufanyika jijini hapa tarehe 28 Oktoba 2021.
Akizungumza wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano huo, Balozi Sokoine amewapongeza Wataalam kutoka Tanzania na Rwanda kwa kukamilisha taarifa kwa wakati na ufanisi na kuwezesha mkutano wa makatibu wakuu kufanyika.
“Mkutano huu wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ni jukwaa muhimu katika kukuza ushirikiano baina ya Nchi zetu hizi mbili jirani na rafiki, kwani hutoa fursa ya kuangalia maeneo ya ushirikiano kwa upana wake pamoja na kutoa nafasi ya kubainisha maeneo ya kipaumbele na kuainisha mpango wa utekelezaji ili kuharakisha maendeleo ya wanachini kupitia programu na miradi tunayokubaliana kuitekeleza” ameeleza Balozi Sokoine
Aliongeza kusema, Mkutano huo wa 15 utatoa nafasi kwa nchi hizi kutathmini namna makubaliano ya awali yalivyotekelezwa, kuainisha changamoto zilizojitokeza kwenye utekelezaji na kutoa suluhu ya namna ya kuzitatua ili kuimarisha ushirikiano uliopo kwa manufaa ya nchi hizi mbili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Rwanda Bi. Shakilla K. Mutoni, ameeleza kuwa pamoja na kupiga hatua kwenye utekelezaji wa maazimio mengi yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa mwisho wa Tume hiyo uliofanyika mwezi Julai, 2016 nchini Rwanda, mkutano huu wa 15 umeongeza chachu katika utekelezaji wa makubaliano, programu na miradi ambayo bado iponyuma katika utelezaji. Aidha, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutekeleza ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambayo baada ya kukamilika kwa ujenzi itarahisisha usafirishaji wa bidhaa kuelekea nchini Rwanda.
Mkutano huu wa Makatibu Wakuu ni mwendelezo wa maandalizi ya Mkutano wa 15 wa Tume ya Kudumu ya Ushirikiano unaotarajiwa kuhitimishwa na Mkutano wa Mawaziri hapo tarehe 28 Agosti 2021.
Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Rwanda kwa Ngazi ya Makatibu Wakuu uliokuwa ukiendelea JNICC jijini Dar es Salaam |
Picha pamoja ya washiriki wa Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Rwanda kwa Ngazi ya Makatibu ulifanyika JNICC jijini Dar es Salaam |
Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Rwanda kwa Ngazi ya Makatibu ukiendelea JNICC jijini Dar es Salaam |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.