Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, aliahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano na Ireland hasa ikizingatiwa kuwa nchini hizo zimekuwa na ushirikiano wa karibu kwa miaka mingi kupitia sekta za biashara, elimu, ujenzi wa uwezo, ulinzi wa kijamii, utalii, kilimo, ufugaji, pamoja na utawala bora.
Mhe. Chana alieleza kuwa Siku ya Mtakatifu Patrick ni Siku muhimu kwa Ireland na Tanzania inatumia siku hiyo kuendelea kuimarisha ushirikiano na uhusiano na Ireland.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Maendeleo, na Diaspora, Mhe. Neale Richmond, alisema maadhimisho ya Siku ya Mtakatifu Patrick ni tukio muhimu kwa Ireland, na kufanyika kwa hafla hiyo nchini kunatoa nafasi ya Nchi hiyo kuonyesha utamaduni wao na kuimarisha ushirikiano na Tanzania kupitia sanaa na muziki.
Sherehe hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Tanzania, akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato David Chumi (Mb), aliyemwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb).
Viongozi wengine ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza ambaye pia anawakilisha Ireland Mhe. Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mkurugenzi wa Idara ya Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi, Balozi John Ulanga.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na wanadiplomasia walioko nchini na wadau mbalimbali.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (kulia), Balozi wa Tanzania nchini Uingereza anayeiwakilisha Ireland pia Mhe. Balozi Mbelwa Kairuki (katikati) pamoja na Mkurugenzi idara ya Ulaya na Marekani katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (kulia)
Mkurugenzi idara ya Ulaya na Marekani katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (kulia) pamoja na Afisa Mambo ya Nje, Noel Mtafya (kushoto)