Friday, April 30, 2021

VACANCY ANNOUNCEMENT


 

BALOZI MULAMULA ATEMBELEA WATUMISHI WALIOPO KATIKA JENGO LA PSSSF

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongea na mmoja wa Watumishi katika Kitengo cha Uhasibu alipotembelea Ofisi hizo kwa lengo la kujionea utendaji 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha Manunuzi Wizarani Bw. Salifius Mligo wakati alipo watembelea Wafanyakazi walioko katika Ofisi hizo Jijini Dodoma kujionea namna wanavyotekeleza majukumu yao.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika Ofisi za Masijala wakati alipo watembelea Wafanyakazi walioko katika Ofisi hizo kwa lengo la kujionea namna wanavyotekeleza majukumu yao.

Wednesday, April 28, 2021

TANZANIA YAWAHAKIKISHIA MAZINGIRA MAZURI WAWEKEZAJI WA MAREKANI

 Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Serikali ya Tanzania imewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Marekani mazingira mazuri na kuwasihi kuendelea kuwekeza hapa nchini.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Mhe. Donald Wright katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Balozi Mulamula amesema makampuni mbalimbali kutoka Marekani yameonesha nia ya kuwekeza katika sekta za nishati, miundombinu, afya na kilimo hususani katika zao la korosho.

“Katika kikao changu na Balozi tumejadili na kusisitiza umuhimu wa Kampuni za Marekani kuwekeza nchini Tanzania.........na Balozi amenihakikishia baadhi ya kampuni hizo zipo tayari kuwekeza hapa nchini,” amesema Balozi Mulamula

Aidha, Mhe. Waziri Mulamula amewataka wafanyabiashara na wawekezaji wa Kitanzania kujipanga kutumia fursa ya kuuza Marekani bidhaa mbalimbali zinazozalishwa hapa nchini.

Kwa Upande wake Balozi wa Marekani, Mhe. Wright amesema uhusiano wa Marekani na Tanzania ni wa miaka mingi na kuahidi kuuendeleza na kuimarisha uhusiano huo.

“Suala la wawekezaji kuja kuwekeza hapa Tanzania nimemhakikishia Mhe. Waziri kuwa suala la wafanyabishara na wawekezaji wa Kimarekani kuja kuwekeza hapa Tanzania ni jambo ambalo nimelipa kipaumbele na ninalifanyia kazi kwa karibu ili wawekezaji wa Kimarekani waendelee kuja kuwekeza kwa wingi Tanzania,” amesema Balozi Wright

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mulamula amekutana kwa maongezi na Balozi wa Comoro hapa nchini, Mhe. Dr. Ahmada El Badasui pamoja na Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Zlatan Milišić ambapo wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano.

“Tumekubaliana kukutana na tume za ushirikiano ili tuweze kujadili na kuona ni jinsi gani tunaweza kuboresha masuala ya biashara na ushirikiano katika maeneo mbalimbali,” amesema Waziri Mulamula.

Nae Balozi wa Comoro hapa nchini amesema nchi yake  itaendelea kushirikiana na Tanzania na kuhakikisha uhusiano huo unaendelea kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Leo nimepokelewa na Waziri Mulamula na tumejadiliana masuala ya ushirikiano baina ya Comoro na Tanzania na pia tumeongelea masuala mbalimbali yanayohusu mabalozi hapa Tanzania pamoja na maeneo ambayo tutaanza kuyafanyia kazi kati ya Comoro na Tanzania,” amesema Mhe.  El Badasui.  

Kwa upande wake Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Milišić amesema kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha inafanikisha malengo ya maendeleo endelevu iliyojiwekea katika kuwaletea maendeleo watanzania.

“UN itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha inafanikisha agenda zake za maendeleo endelevu,” amesema Bw. Milišić.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongea na Balozi wa Comoro hapa nchini, Mhe. Dr. Ahmada El Badasui wakati wa maongezi yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam


Balozi wa Comoro hapa nchini, Mhe. Dr. Ahmada El Badasui akimuelezea jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula wakati wa mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiteta jambo na Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Donald Wright katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akipokea zawadi ya kitabu kutoka kwa Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Donald Wright. Kitabu hicho kinaelezea fursa za utalii pamoja na mbuga za wanyama nchini Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisalimiana na Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Zlatan Milišić katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam


Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Zlatan Milišić akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) wakati wa maongezi yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam





Tuesday, April 27, 2021

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA MABALOZI WA BURUNDI, UINGEREZA NA UMOJA WA ULAYA

 Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana kwa mazungumzo na mabalozi watatu wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na kupokea nakala ya hati za utambulisho za balozi mteule wa Italia hapa nchini.

Mabalozi hao wamekutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam ni Balozi wa Burundi Mhe. Gervais Abayeho, Balozi wa Uingereza Mhe. David Concar pamoja na Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Manfredo Fanti.

Pamoja na mambo mengine, Viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu Biashara na Uwekezaji na Utamaduni.

“Leo nimekutana na mabalozi watatu kutoka Burundi, Uingereza na Umoja wa Ulaya na nimejadiliana nao masuala mbalimbali ya ushirikiano katika masuala ya uchumi, biashara na uwekezaji na mahusiano baina yetu na nchi zao,” amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa “mabalozi wote watatu wameahidi kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia kwa manufaa ya nchi zetu………lakini pia tumejadili mipango ya kimkakati kutoka kwa Umoja wa Ulaya na Uingereza ambapo wangependa kuona inaendelezwa katika awamu hii,” amesema Balozi Mulamula.

Nae Balozi wa Burundi nchini Tanzania Mhe. Abayeho amesema uhusiano wa Burundi na Tanzania ni wa miaka mingi na wamefurahia kuuona uhusiano huo ukiendelea kuboreka zaidi na tunaamini uhusiano huo utaendelea kudumu kwa miaka mingi.

“Uhusiano wa Burundi na Tanzania ni uhusiano wa muda mrefu na tunafurahia kuona unazidi kuimarika. Mbali na masuala ya uhusiano umependekeza utekelezwaji wa miradi mikubwa kama vile ujenzi wa bandari, barabara na reli uharakishwe kwa manufaa ya nchi zote mbili,” Amesema Balozi Abayeho

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar amesema katika kikao chake na Mhe. Waziri wamejadili namna ya kuboresha uhusiano baina ya Uingereza na Tanzania na jinsi ya kufanya kazi kwa pamoja katika kudumisha na kuendeleza uhusiano huo.

Balozi wa Umoja wa Ulaya, Mhe. Manfredo Fanti amesema kuwa uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania   na Umoja wa Ulaya ni wa zaidi ya miaka 46 na umekuwa ukinufaisha pande zote mbili hivyo Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha kuwa inapata manendeleo kijamii na kiuchumi.

Katika tukio jingine, Mhe. Waziri Mulamula amepokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Italia hapa nchini Mhe. Marco Lombardi.

“Tanzania na Italia tuna uhusiano mzuri katika maeneo mbalimbali ikiwemo utalii, uwekezaji na elimu na tumejadiliana mambo aliyoagizwa na serikali yake katika kudumisha uhusiano wa Italia na Tanzania.

Kwa Upande wake Balozi Mteule, Mhe. Lombardi amesema Italia na Tanzania zina masuala mengi ya kushirikiana katika sekta mbalimbali za kiuchumi,kijamii na utamaduni na kwamba yuko nchini kuhakikisha  hayo yote yanatekelezeka kwa maslahi ya nchi zote mbili.

“Tunaamini kupitia maongezi yetu ya leo tutaendelea kuimarisha uhusiano wetu wa kiuchumi na kisiasa kwa maslahi ya Italia na Tanzania, lakini pia nimemhakikishia Mhe. Waziri kuwa Italia itaendelea kuwa bega kwa bega na Tanzania katika kuhakikisha mahusiano yake ya kidiplomasia yanakua na kuimarika,” amesema Mhe. Lombardi 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongea na Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini Mhe. Manfredo Fanti wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimsikiliza Balozi wa Burundi hapa nchini Mhe. Gervais Abayeho wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam


Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimsikiliza Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akipokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi mteule wa Italia hapa nchini Mhe. Marco Lombardi jijini Dar es Salaam

 



Monday, April 26, 2021

BALOZI LIBERATA MULAMULA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CHINA,UFARANSA,ISRAEL,UBELGIJI NA UJERUMANI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Mb) Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China hapa Nchini Balozi Wang Ke. Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha mahusiano baina ya Nchi hizo katika nyanja za kiuchumi,kibiashara na uwekezaji ambapo moja ya suala walilolijadili ni kuanza kwa safari za ndege (ATCL) kwenda Guangzhou Nchini China mara moja kila baada ya wiki mbili
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Mb) Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Balozi Frederick Clavier mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masharika Jijini Dodoma. Mazungumzo hayo yalilenga kudumisha mahusiano baina ya chi hizo mbili katika Nyanja za diplomasia ya mahusiano na uchumi,biashara na uwekezaji
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Mb) Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Israel hapa Nchini Balozi Oded Joseph mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dodoma. Katika mazungumzo hayo Balozi Mulamula amemsihi Balozi Oded kuhakikisha Israel inakuwa na Ubalozi wake rasmi hapa Nchini na kumshukuru kwa hatua ya Israel kuwachukuwa vijana wa Kitanzania kwenda Nchini humo kwa mafunzo ya vitendo na nadharia kuhusu kilimo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Mb) Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Ubelgiji hapa Nchini Balozi Peter Van Acker mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dodoma. Mazungumzo hayo yalilenga pamoja na mambo menfine ukamilishwaji wa majadiliano ya ushirikiano katika sekta ya usafiri wa anga na kuimarisha ushirikiano katika sekta za kilimo na usambazaji wa maji safi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Mb) Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Balozi Regina Hess mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dodoma. Pamoja na masumla menfine Viongozi hao walijadili masuala ya ushirikiano katika sekta ya afya,elimu,biashara,uwekezaji pamoja na maliasili na utalii
 

Sunday, April 25, 2021

NAIBU WAZIRI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MWENYEKITI WA KAMATI YA SERIKALI YA URUSI

Tarehe 25 Aprili 2021, kwenye Ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi Oleg Ozerov, Mwenyekiti wa Kamati ya Serikali ya Urusi inayosimamia Maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika na Urusi ( Africa- Russia Summit). Mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Mheshimiwa Yuri Popov, Balozi wa Urusi hapa nchini. 

Mbali na majadiliano yaliyolenga kuimarisha na kuendeleza mahusiano baina ya Mataifa haya mawili pia walijadili namna bora ya kufanya Mkutano ujao (Afica-Russia Summit) utakaofanyika 2022 kuwa na tija zaidi kwa Mataifa ya Afrika ikiwemo kuona maeneo ambayo Urusi ingweza kuongeza uwekezaji wake barani Afrika badala ya mfumo wa sasa wa Makampuni ya Urusi kufanya biashara zaidi. Aidha, walibadilishana mawazo kuhusu agenda na mada zinazoweza kujadiliwa katika Mkutano huo wa pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika na Urusi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb),  akiagana na Balozi Oleg Ozerov, Mwenyekiti wa Kamati ya Serikali ya Urusi inayosimamia Maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika na Urusi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb),  akiwa katika  mazungumzo na Balozi Oleg Ozerov, Mwenyekiti wa Kamati ya Serikali ya Urusi inayosimamia Maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika na Urusi.

Friday, April 23, 2021

BARAZA LA MAWAZIRI LA KISEKTA LA AFYA LA AHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA KATIKA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA AFYA

Mkutano wa Kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya ngazi ya Mawaziri uliofanyika leo katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania; umekubaliana na kuahidi kuendelea kushirikiana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya katika Jumuiya. 

Mkutano huu uliotimishwa  leo tarehe 23 Aprili 2021, umefanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 19 hadi 23 Aprili 2021, ulikuwa na lengo la kufanya mapitio ya hatua ya maendeleo iliyofikiwa katika utekelezaji wa maamuzi na maagizo yaliyotolewa na Mkutano uliopita wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na la Kisekta, sambamba na kuibua maeneo mapya yanayohitajika kupewa kipaumbele kulingana na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati za Wataalamu.

Mkutano huu uliokuwa ukiongozwa na Mhe. Mutahi Kagwe Waziri wa Afya wa Kenya ambale pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, pamoja na masuala mengine umepitia kujadili na kutoa maelekezo katika kutatua changamoto mbalimbali, zinazokwamisha utekelezaji wa mikakati ya pamoja ya kukabiliana na Ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu unaosababishwa na Virusi vya Korona (UVIKO-19), na usalama wa dawa na chakula katika Jumuiya. 

Kila Nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa nyakati tofauti katika mkutano huo imeeleza utayari wake wa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mikakati na mipango mbalimbali waliyokubaliana kuitumia katika kutatua changamoto za sekta ya afya. 

Mkutano huu umehudhuriwa na Mawaziri kutoka Nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaosimamia masuala ya Afya. Tanzania imewakilishwa na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy O. Gwajima (Mb)

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Jamii Mhe. Christophe Bazivamo (kulia) na Kaimu Mkuu wa Idara ya Afya, Sekretarieti ya Jumuiya Dkt. Michael Katende wakiratibu Mkutano wa 20 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya.
Mkutano wa 20 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya ukiendelea jijini Arusha Tanzania
Mkutano wa 20 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya ukiendelea jijini Arusha Tanzania
Kaimu Mkurugezi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Bw. Eliabi Chodota (wa kwanza kushoto) akifuatilia Mkutano wa kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya uliokuwa ukiendelea jijini Arusha, Tanzania.
Washiriki wa Mkutano wa 20 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya kutoka Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja.

Thursday, April 22, 2021

VACANCY ANNOUNCEMENT


 

ANGLOGOLD ASHANTI, TANZANIA ZAKUBALIANA KUENDELEZA USHIRIKIANO

Na Mwandishi wetu, Dar

Kampuni ya Madini ya Anglogold Ashanti ya Afrika Kusini imeahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika sekta ya madini na kuhakikisha kuwa sekta hiyo inakuwa mstari wa mbele kuchangia uchumi.

Ahadi hiyo imetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Anglogold Ashanti – Afrika, Bw. Sicelo Ntuli wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) leo Jijini Dar es Salaam.

Akiongea mara baada ya mazungumzo hayo Balozi Mulamula amesema kuwa, Anglogold Ashanti ni wadau wakubwa katika sekta ya madini na wameonesha utayari wao wa kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kukuza na kuendeleza sekta ya madini. 

“Leo hii nimekutana na uongozi wa Kampuni ya Madini ya Angogold Ashanti na tumejadili pamoja na mambo mengine, utayari wa Kampuni hiyo kushirikiana na Serikali katika kukuza sekta ya madini hapa nchini,” Amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa kitendo cha kukutana na wadau wa madini kama Anglogold Ashanti na kujadiliana nao masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kukuza sekta ya madini ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya Uchumi.

Kwa Upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Anglogold Ashanti Bw. Ntuli amesema kuwa uongozi wa Anglogold umefarijika kukutana na Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje na kuweza kujadiliana nae mambo mbalimbali ikiwemo suala la kukuza ushirikiano baina ya Kampuni hiyo na Serikali ya Tanzania.

“Sisi kama Anglogold tumefarijika kuona Serikali ya Tanzania ipo tayari kuendeleza ushirikiano na Sisi…….tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” Amesema Bw. Ntuli

Aprili 16, 2021 Kampuni ya Anglogold Ashanti iliingia ubia na Kampuni ya BG Umoja ya nchini Tanzania kwa ajili ya kuchimba madini katika miradi ya Nyankanga na Geita Hill. Anglogold ni Kampuni mama ya Geita Gold Mine (GGML) imeipatia BG Umoja mkataba wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 186 kwa miaka miwili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Afisa Mtendaji Mkuu wa Anglogold Ashanti – Afrika, Bw. Sicelo Ntuli wakati walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam


Afisa Mtendaji Mkuu wa Anglogold Ashanti – Afrika, Bw. Sicelo Ntuli akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongoza kikao chake na Kampuni ya Madini ya Anglogold Ashanti ya Afrika Kusini kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam


 

Wednesday, April 21, 2021

MKUTANO WA KAWAIDA WA 20 WA BARAZA LA MAWAZIRI LA KISEKTA LA AFYA UNAENDELEA KUFANYIKA JIJINI ARUSHA, TANZANIA.

Mkutano wa Kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya umeendelea kufanyika kwa siku ya tatu leo, katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania. 

Mkutano huu ambao utafanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 19 hadi 23 Aprili 2021,una lenga kufanya mapitio ya hatua ya maendeleo iliyofikiwa katika utekelezaji wa maamuzi na maagizo yaliyotolewa na Mkutano uliopita wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na la Kisekta. Vilevile mkutano huu ataangazia masuala mengine muhimu katika Sekta ya Afya ndani ya Jumuiya. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huu katika ngazi ya wataalamu Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo amewashukuru wataalamu wa Sekta ya Afya kwa juhudi zao za kutatua changamoto mbalimbali na kutoa mapendekezo na ushauri wa kitaalamu kwa ngazi za maamuzi ambayo yamepelekea utekelezaji wa mipango ya ubunifu katika sekta ya Afya na kuunganisha vipaumbele vya uwekezaji kwenye sekta hiyo katika Jumuiya. 

Katika ngazi ya Wataalamu mkutano huu unafuatilia na kutathimini maendeleo ya utekelezaji wa masuala mbalimbali katika sekta ya afya kama ilivyoelekezwa na Mkutano uliopita wa Baraza la Mawaziri na la Kisekta, ikiwemo; maendeleo ya utekelezaji wa mikakati ya pamoja ya kukabiliana na Ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu unaosababishwa na Virusi vya Korona (UVIKO-19), usalama wa dawa na chakula, masuala ya afya ya uzazi, Watoto na Lishe na hali ya utekelezaji wa miongozo na taratibu za taaluma na huduma za afya katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano katika ngazi ya wataalamu Dkt. Leonard Subi Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto ameeleza kuwa; Tanzania imeendelea kuongeza mikakati ya kuzuia na kudhibiti janga la UVIKO-19 tangu lilipozuka katikati ya Machi 2020. Ameongeza kusema kuwa UVIKO-19 ni ugonjwa mpya wa aina yake kwani tumeshuhudia tishio la ukuaji wa uchumi wa ulimwengu na umegharimu maisha ya watu wengi sehemu mbalimbali duniani, hivyo mshikamano ni muhimu ili kuukabili. “Tanzania tunadhamini juhudi zinazofanywa na Wanasayansi mbalimbali ulimwenguni katika kupata suluhisho la kudhibiti ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na mshikamano ulioonyeshwa na WHO, GAVI na Taasisi zingine zinazounga mkono jitihada hizo. Tanzania haikatai chanjo ya UVIKO-19, isopokuwa tunafanya tathmini thabiti kabla ya kukubali matumizi ya chanjo nchini. Mathalani, Tanzania nyakati zote imekuwa na rekodi za juu kwenye matumizi ya chanjo kwa watoto wachanga walio chini ya miaka 5 hivyo tutaendelea kutoa ushirikiano mzuri kwa wadau wa ndani na Wakimataifa katika mapambano dhidi ya janga la COVID-19.” Ameeleza Dkt.Subi

Mkutano huu unaofanyika kwa njia mbili ya ana kwa ana na video, umehudhuriwa na nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Aprili 22, 2021 watakutana Makatibu Wakuu na Aprili 23, 2021 watakutana Mawaziri wanaosimamia masuala ya Afya kutoka nchi Wanachama.

Kaimu Mkurugezi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Bw. Eliabi Chodota akichangia jambo kwenye Mkutano wa kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya unaoendelea kufanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Dkt.Leonard Subi akifuatilia mkutano wa kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya unaofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Dkt.Leonard Subi akifafanua jambo kwenye Mkutano wa Kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya unaoendelea kufanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania

 

Ujumbe kutoka Tanzania wakifuatilia Mkutano
Mkutano wa kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya ukiendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania.

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JAMHURI YA AFRIKA KUSINI

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Grace Naledi Pandor kujadili mambo ya kuendeleza mashirikiano baina ya Jamhuri ya Afrika Kusini na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Balozi Mulamula amefanya mazungumzo hayo Pretoria nchini Afrika Kusini ambapo pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula alieleza kuwa mahusiano kati ya Afrika Kusini na Tanzania ni ya kihistoria na yameendelea kuimarika tangu enzi a kupigania uhuru kwa nchi za kusini mwa Afrika.

Kwa upande wake Waziri Pandor ameishukuru kwa ujio wa Balozi Mulamula na kwa kufika nchini Afrika Kusini na pia alieleza kuwa Jamhuri ya Afrika Kusini inathamini mashirikiano ya kihistoria kati ya nchi zetu mbili na hivyo kinachohitajika ni kuendeleza na kuimarisha mashirikiano ya kiuchumi na kisiasa tuliyonayo sasa hivi. Jamhuri ya Afrika Kusini inayo azma ya kushiriki kikamilifu kujenga makumbusho ya urithi (heritage museum) ya harakati za kupigania uhuru kusini mwa Afrika zenye chimbuko lake nchini Tanzania na vilevile kuonyesha juhudi za Tanzania katika harakati za kupigania uhuru na kwa nchi za kusini mwa Afrika.

Mawaziri hao wamejadili pia mchakato wa tathimini ya utekelezaji wa Bi-National Commission (BNC) ambapo kwa mwaka huu Afrika Kusini ndiyo itakuwa mwenyeji wa tathimini hiyo ambayo hujumuisha ngazi ya watedaji wakuu wa sekta mbalimbali wan chi hizi mbili, Mawaziri na huitimishwa na Waheshimiwa Marais wa nchi zote mbili. 

Aidha, Balozi Mulamula kabla ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, alikutana na watumishi wa ubalozi wa Tanzania Pretoria katika mkutano ulifanyika Ubalozini, Mhe. Waziri alipokea taarifa ya eneo la uwakilishi la Ubalozi ambalo linajumuisha Afrika Kusini, Botswana, Falme ya Lesotho na SADC. Taarifa hiyo ilieleza juhudi za Ubalozi katika kukuza mahusiano na nchi za eneo la uwakilishi, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, diplomasia ya siasa, wanadiaspora wa eneo la uwakilishi.

Balozi Mulamula ameutaka Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kuendela kufanya kazi kwa malengo, watumishi kujiwekea malengo ili kufanikisha malengo ya Ubalozi na hatimaye Ubalozi kuchangia malengo ya Wizara kwa ujumla.

“Nawasihi kuendeleza mahusiano na nchi za uwakilishi na Balozi nyingine zilizopo katika nchi za uwakilishi na suala hili la kujenga mahusiano na watumishi wote na siyo Balozi pekee yake,” amesema Balozi Mulamula.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Pretoria nchini Afrika Kusini. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Grace Naledi Pandor  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Grace Naledi Pandor


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo