Thursday, March 29, 2018

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

HAKUNA TISHIO LA USALAMA NCHINI

Kumekuwa na taarifa kwenye mitandao ya kijamii zinazosambazwa na watu wasioitakia mema nchi, zinazotishia usalama wa raia na mali zao. Taarifa hizo zimewatia hofu baadhi ya raia wa kigeni na wanadiplomasia wanaofanya kazi na kuishi hapa nchini.
Taarifa hizo zimekuwa zikidai kuwa kutakuwa na maandamano yatakayofanyika tarehe 26 Aprili 2018 na zinawaonya raia wa kigeni wasiende Zanzibar katika kipindi cha Sikukuu ya Pasaka na sherehe za Muungano kwa sababu za kiusalama.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawahakikishia wanadiplomasia na raia wote wa kigeni wanaofanya kazi na kuishi nchini na wananchi kwa ujumla kuwa, waendelee na shughuli zao ikiwemo kusafari kutoka eneo moja kwenda jingine bila ya hofu yeyote kwa kuwa hakuna dalili zozote za uvunjifu wa amani, usalama na utulivu wa nchi.
Vyombo vya usalama vipo makini vinatekeleza majukumu yake ipasavyo kuhakikisha kuwa matukio yote ya uhalifu yanadhibitiwa kabla ya kuleta madhara kwa umma. 
Hivyo, Wizara inawaomba wanadiplomasia, raia wa kigeni wanaoishi nchini na wananchi kwa ujumla kuzipuuza taarifa hizo. Wananchi waendelee kushirikiana kwa karibu na Serikali yao kupata taarifa sahihi kutoka vyanzo vinavyoaminika badala ya kutegemea propaganda za watu wanaotumia mitandao ya kijamii kwa maslahi binafsi. 

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 29 Machi 2018

Wednesday, March 28, 2018

UBALOZI WA TANZANIA NCHINI UHOLANZI WASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA MAJI DUNIANI


Wanafunzi wa Shule za Msingi mbalimbali mjini Gouda,

 wakishiriki matembezi huku kila mmoja akiwa amebeba

mgongoni lita 6 za maji kila mmoja.

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe.Irene Kasyanju

 akikaribishwa Gouda na Bibi Rola

Hulsbergen, Mwenyekiti wa Rotary Club ya nchini Uholanzi

 Meya wa Wanafunzi wa Gouda,

 Bi. Romaissa Magou (kulia) akimkabidhi Balozi Kasyanju 

mfano wa Hundi ya kiasi cha fedha kilichokusanywa baada

 ya matembezi hayo.

Balozi Kasyanju na Bibi Hulsbergen wakisikiliza kwa makini

 shairi kuhusu Tanzania lililoandaliwa na wanafunzi wa 

Gouda.

=====================================================

UBALOZI WA TANZANIA NCHINI UHOLANZI WASHIRIKI KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA MAJI DUNIANI YALIYOFANYIKA MJINI GOUDA, UHOLANZI TAREHE 21 MACHI 2018

Katika kuadhimisha Siku ya Maji Duniani, Manispaa ya mji wa Gouda nchini Uholanzi, kwa kushirikiana na Taasisi za Rotary na shule za msingi za mji huo zilimwalika Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju kushiriki katika matembezi ya hisani maarufu kama Walking for Water yaliyoandaliwa kwa lengo la kuisaidia Tanzania katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa maji safi inayowakabili watoto katika nchi zinazoendelea.

Matembezi hayo yalishirikisha walimu, wazazi na wanafunzi wa shule za msingi za mjini Gouda ambao walitembea umbali wa kilometa 6 huku kila mmoja akiwa amebeba lita sita (6) za maji kuashiria kutambua changamoto kubwa ya ukosefu wa maji safi inayowakabili watoto, hususan katika Nchi Zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Maadhimisho ya Siku hii kwa mwaka huu, yalilenga kuisaidia Tanzania ambapo sambamba na matembezi hayo, kiasi cha Euro 24,021.29 kutoka mji wa Gouda kilichangwa kwa ajili ya kusaidia miradi ya afya na ujenzi wa vyoo inayoendeshwa katika Mikoa ya Tabora na Dodoma. Mhe. Balozi Irene Kasyanju alikabidhiwa mfano wa Hundi ya kiasi hicho cha fedha kilichokusanywa kutokana na michango ya Taasisi husika, wazazi wa wanafunzi na wadau mbalimbali.

Akipokea mfano wa Hundi hiyo Mhe. Balozi Irene Kasyanju, kwa niaba ya wananchi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa shukrani za dhati kwa waandaaji, wadhamini na hususan wanafunzi kwa matembezi pamoja na mchango huo mkubwa na kueleza kuwa utasaidia kubadilisha maisha ya watoto na wananchi wa maeneo husika kwa ujumla. Aidha, Mhe. Balozi Kasyanju alisisitiza umuhimu wa matumizi makini ya maji kwani maji ni muhimu kwa viumbe pamoja na mimea.

Jumla ya kiasi cha Euro 360,000.00 kinatarajiwa kukusanywa kutokana na michango iliyotolewa kutokana na matembezi kama hayo katika miji mingine ya Uholanzi siku hiyo pamoja na Serikali ya Uholanzi kuisaidia Tanzania hususan kwenye mikoa tajwa.