Monday, July 30, 2018

Balozi Mpya wa Kenya nchini Mhe. Dan Kazungu akabidhi Hati za utambulisho

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati za utambulisho
kutoka kwa Balozi mteule wa Kenya hapa nchini Dan Kazungu Ikulu jijini Dar es Salaam leo Julai 30, 2018

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo Balozi mteule wa Kenya hapa nchini Dan Kazungu  mara baada ya kuwasilisha Hati zake za Utambulisho Ikulu jijini Dar es Salaam leo Julai 30, 2018

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea zawadi ya Picha kutoka kwa Balozi mteule wa Kenya hapa nchini Dan Kazungu. Zawadi hiyo ya picha imetoka kwa Mama mzazi wa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, Mama Ngina Kenyatta na katika picha hiyo anaonekana Rais Dkt. Magufuli akiwa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta pamoja na Mama Ngina Kenya walipokuwa Nairobi nchini Kenya.

Saturday, July 28, 2018

TAARIFA KUHUSU MATOKEO YA AWALI YA NAFASI ZA AJIRA ZA SADC


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUHUSU MATOKEO YA AWALI YA NAFASI ZA AJIRA KATIKA SEKRETARIATI YA SADC ZILIZOTANGAZWA                                              KWA MWAKA 2018


Sekretarieti ya SADC ilitangaza nafasi 50 katika kada mbalimbali mwezi wa Mei, 2018. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti na Utumishi ilitangaza nafasi hizo kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Wizara inapenda kuutangazia umma kuwa baada ya mchujo wa duru ya kwanza uliofanywa na Kikosi Kazi Maalum, jumla ya waombaji 141 kati ya waombaji 1,472 wamepita katika uchambuzi wa awali. Katika muktadha huo, Wizara inaweka orodha ya awali ya mchujo wa Tanzania ya waombaji waliochaguliwa katika nafasi mbalimbali pamoja na jedwali lenye kuonyesha idadi ya waombaji hao.

Wizara inapenda kuutaarifu umma na waombaji wa nafasi za ajira zilizotangazwa na SADC kuwa taarifa zaidi itatolewa Sekretarieti ya SADC kwa wale tu watakao kuwa kwenye orodha ya mchujo wa duru ya pili (shortlisted) utakayofanywa na Sekretarieti ya SADC.

Aidha, tutakumbuka kuwa mwezi wa Mei, 2017 Sekretarieti ya SADC ilitangaza nafasi 48 ambapo zoezi la usaili wake lilikamilika mwaka huu. Kwenye nafasi 48, Tanzania imefanikiwa kupata nafasi tano za kimkakati. Nafasi hizo zinaainishwa kama ifuatazo:

i.      Afisa Mwandamizi anayeshughulikia masuala ya Sera na Mikakati ya Maendeleo, (Senior Officer - Policy and Strategy Development);

ii.    Afisa Mwandamizi Mipango anayeshughulikia masuala ya Viwanda na Ushindani, (Senior Programme Officer - Industrialization and Competitiveness);

iii.   Afisa Mipango anayeshughulikia masuala ya Ushuru na Utaratibu, (Programme Officer Customs and Procedures);

iv.   Afisa anayeshughulikia masuala ya Ufuatiliaji, Tathmini na utoaji wa Taarifa, (Monitoring, Evaluation and Reporting Officer); na

v.    Afisa anayeshughulikia masuala ya Fedha na Bajeti, (Finance Officer - Treasury and Budget )

Tunawapongeza kwa dhati wote waliochaguliwa na kufanikiwa kuingia kwenye orodha ya mchujo wa awali uliofanyika Tanzania kwa mwaka 2018. 

Aidha, kwa aina ya pekee, tunawapongeza maafisa waliochaguliwa kwenye nafasi tano (5) zilizotajwa na tunawatakia kila la heri katika mjukumu yao mapya sambamba na kuwasihi daima kukumbuka kuwa wanaliwakilisha Taifa letu kwenye nafasi hizo.

Mwisho, Wizara inapenda kutaarifu kuwa itaendelea kuzitangaza fursa kama hizi zitapojitokeza kupitia SADC na Jumuiya zingine za Kikanda na Kimataifa ambazo Tanzania ni nchi mwanachama, kwa manufaa ya watanzania wote. Hivyo, tunawaomba Watanzania wasikate tamaa na wasisite kuwasilisha maombi ya ajira kama hizi pale fursa zinapojitokeza.


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dar es Salaam,

27 Julai, 2018


Tuesday, July 24, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA MKURUGENZI WA WFP NCHINI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Bw. David M. Baesley atafanya ziara ya kikazi nchini kuanzia tarehe 25 Julai 2018 hadi tarehe 03 Agosti 2018. Ziara hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Serikali ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na WFP.

Wakati wa ziara hiyo nchini, Bw. Baesley ataonana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa kitaifa kwa lengo la kujadiliana nao kuhusu maeneo ya ushirikiano kati ya WFP na wakulima wadogo kupitia mpango wa “Social Protection Programmes”; Mfumo wa Serikali wa Usalama wa Chakula; na masuala ya Wakimbizi na Jamii zinazozunguka hifadhi za wakimbizi pamoja na njia za kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Bw. Baesley anatarajiwa kuwasili nchini tarehe 25 Julai, 2018 kwa ajili ya kuanza ziara hiyo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma.
24 Julai 2018

Balozi Mabumba awasisitiza Watanzania waishio nchini Comoro (TADICO) kuwekeza nyumbani


 Balozi wa Tanzania Visiwani Komoro Mhe. Sylvester Mabumba alikutana na kufanya mazungumzo na uongozi mpya wa Diaspora ya Watanzania waishio Komoro (TADICO) tarehe 23 Julai 2018. Viongozi hao wapya walifika ofisi za Ubalozi kwa ajili ya kujitambulisha ambapo miongoni mwa mambo waliyojadili ni pamoja na  kutoa ahadi ya kuinua Diaspora ya Watanzania waishio Comoro ambapo kwa muda mrefu Diaspora hiyo imeonekana kuwa nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na Diaspora za nchi nyingine.

Kwa upande wake Mhe. Balozi Mabumba alichukua fursa hiyo kuwapongeza viongozi hao wapya waliochaguliwa pamoja na kuwatakia kila la kheri katika nafasi zao hizo mpya walizoaminiwa na Watanzania wenzao. Aidha, Mhe. Mabumba alisisitiza juu ya umuhimu wa wanachama kulipa michango ya uanachama na vilevile kuwaomba viongozi kuwa wasimamizi wazuri wa matumizi ya fedha za wanachama hao.

Katika hatua za kuhuisha chama hicho wajumbe walishauriwa pia kuwa wabunifu katika mikakati yao na vilevile waangalie njia gani bora za kuibua vyanzo vipya vya mapato badala ya kutegemea michango ya wanachama pekee. Pia Balozi Mabumba aliwahimiza viongozi hao kutosahau kuwekeza nyumbani na vilevile kuchangamkia fursa za biashara ambazo zinapatikana Tanzania na kuzitangaza  Visiwani humo.


Balozi wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Balozi Sylivester Mabumba (kati) akiwa katika picha ya pamoja na maafisa Ubalozi na viongozi wa Diaspora visiwani Comoro. Kutoka Kushoto ni Bw.. Hussein Banoga, Makamu Mwenyekiti; Bw.. Khamis Salum, Mweka Hazina; Bw.. Thabit Khamis, Afisa Ubalozi; Bw.. Fikiri Salum, Katibu Mkuu; Bw. Salum Ali, Mwenyekiti; Bw. Fuastine, Bw. Isakwisa na Bw. Mudrick Soragha.
Viongozi wakiwa katika picha ya pamoja.

Monday, July 23, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA MHE. MKAPA NCHINI MSUMBIJI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mkutano wa Pili wa Chama Tawala cha Msumbiji FRELIMO yatafanyika katika Jimbo la Niassa nchini Msumbiji tarehe 25 Julai 2018. Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi alimwalika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kushiriki maadhimisho hayo. Kutokana na majukumu mengine ya kitaifa Mhe. Rais Magufuli hatoweza kushiriki. Hivyo, kwa kuona umuhimu wa mahusiano kati ya Tanzania na Msumbiji na umuhimu wa maadhimisho hayo kwa historia ya nchi hizi mbili, amemteua Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Benjamin William Mkapa amwakilishe kwenye sherehe hizo na ataambatana na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (Bara), Mhe. Philip Mangula.

Mahusiano kati ya Tanzania na Msumbiji

Mahusiano kati ya Tanzania na Msumbiji ni mazuri na yamekuwa yakiimarika kila wakati. Mahusiano kati ya nchi hizi yalianza enzi za harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa Kireno nchini Msumbiji. Mahusiano hayo yalijengwa na waanzilishi wa mataifa haya mawili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Samora Moises Machel na yameendelea kuwa mazuri siku hadi siku na kuendelezwa na Viongozi wote Wakuu waliofuata wa nchi hizi mbili.  Ziara za Viongozi wa ngazi mbalimbali wa Serikali na vyama tawala vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na FRELIMO wameendelea kutembeleana na kudumisha uhusiano huo.

Ushirikiano katika Chuo cha Diplomasia (Mozambique - Tanzania Centre for Foreign Relations (CFR)

Chuo cha Diplomasia (Mozambique-Tanzania Centre for Foreign Relations – CFR) kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam  ni moja ya alama muhimu za ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji. Chuo cha Diplomasia kilianzishwa mwaka 1978, kwa makubaliano ya nchi za Tanzania na Mozambique. Chuo hichi kilianzishwa kwa lengo la kutoa mafunzo kwa Maafisa wa Mambo ya Nje kutoka katika nchi hizi mbili katika taaluma ya Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia.

Awali, kabla ya kubadilishwa kuwa Chuo cha Diplomasia, ilikuwa ni kituo cha harakati za kupigania uhuru wa Msumbiji. Hivyo, katika harakati za Ukombozi kutoka kwa wakoloni, wapigania uhuru wa kutoka Msumbiji wakiongozwa na Hayati Eduardo Mondlane waliweka kambi chuoni hapo na kuanzisha chama cha Ukombozi cha FRELIMO mnamo mwaka 1962. Mwaka 1970 Hayati Samora Machel alishika madaraka ya kukiongoza chama hicho baada ya kuuawa kwa Mhe. Mondlane

Ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara

Tanzania na Msumbiji zimeendelea kushirikiana katika masuala ya kiuchumi na biashara kwa kuzingatia ujirani na muingiliano mkubwa wa wananchi wa nchi hizi mbili, hususan  katika Mikoa ya Ruvuma na Mtwara kwa upande wa Tanzania, na Majimbo ya Niassa na Cabo Delgado kwa upande wa Msumbiji.  Tanzania na Msumbiji zinauziana bidhaa mbalimbali za kilimo na viwandani.

Kadhalika kuna Makampuni makubwa kadhaa ya Kitanzania yaliyowekeza mitaji mikubwa nchini Msumbiji.  Vile vile, wapo Watanzania wanaomiliki makampuni ya usafirishaji wa abiria na biashara za kati na ndogo. Ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na misingi imara ya kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi hizi mbili, Tanzania na Msumbiji ziliamua kujenga Daraja la Umoja linaloziunganisha nchi hizo kwenye mpaka wa Mto Ruvuma ili kuboresha na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi.

Mhe. Mkapa na Ujumbe wake wanatarajia kuondoka nchini tarehe 24 Julai, 2018 na kurejea tarehe 26 Julai, 2018.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma.
23 Julai 2018

Naibu Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje aongoza maadhimisho ya siku ya Taifa la Misri

Balozi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Msri nchini,  Mhe. Mohamed Yassin El Shawaf akimkaribisha mgeni rasmi ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan M. Mwinyi katika Sherehe ya Kitaifa ya Misri iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi, Barabara ya Kingsway, Osterbay jijini Dar es Salaam. Kulia kwa Naibu Katibu Mkuu, ni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Valentino Mlowola na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Makamba Dahari (kushoto kwa Naibu Katibu Mkuu)
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ramadhan M. Mwinyi akisikiliza hotuba ya Balozi wa Misri Mhe. Mohamed Yassin El Shawaf wakati wa maadhimisho ya siku ya taifa la Misri
Viongozi mashuhuri waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu Mstaafu na Bw. Valentino Mlowola, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU wakiwa katika meza moja na Naibu Katibu Mkuu na Balozi El Shawaf
Picha ya pamoja