TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mkutano wa Pili wa Chama Tawala
cha Msumbiji FRELIMO yatafanyika katika Jimbo la Niassa nchini Msumbiji tarehe
25 Julai 2018. Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi alimwalika Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM),
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kushiriki maadhimisho hayo. Kutokana na majukumu
mengine ya kitaifa Mhe. Rais Magufuli hatoweza kushiriki. Hivyo, kwa kuona
umuhimu wa mahusiano kati ya Tanzania na Msumbiji na umuhimu wa maadhimisho
hayo kwa historia ya nchi hizi mbili, amemteua Rais Mstaafu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Benjamin William Mkapa amwakilishe kwenye sherehe
hizo na ataambatana na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (Bara), Mhe.
Philip Mangula.
Mahusiano kati ya Tanzania na
Msumbiji
Mahusiano kati
ya Tanzania na Msumbiji ni mazuri
na yamekuwa yakiimarika kila wakati. Mahusiano kati ya nchi hizi yalianza enzi za harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa
Kireno nchini Msumbiji. Mahusiano hayo yalijengwa na waanzilishi wa mataifa
haya mawili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Samora Moises
Machel na yameendelea kuwa mazuri siku hadi siku na kuendelezwa na Viongozi wote
Wakuu waliofuata wa nchi hizi mbili. Ziara za Viongozi wa ngazi
mbalimbali wa Serikali na vyama tawala vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na FRELIMO
wameendelea kutembeleana na kudumisha uhusiano huo.
Ushirikiano
katika Chuo cha Diplomasia (Mozambique - Tanzania Centre for Foreign Relations
(CFR)
Chuo cha Diplomasia
(Mozambique-Tanzania Centre for Foreign Relations – CFR) kilichopo Kurasini
jijini Dar es Salaam ni moja ya alama
muhimu za ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji. Chuo cha Diplomasia
kilianzishwa mwaka 1978, kwa makubaliano ya nchi za Tanzania na Mozambique.
Chuo hichi kilianzishwa kwa lengo la kutoa mafunzo kwa Maafisa wa Mambo ya Nje
kutoka katika nchi hizi mbili katika taaluma ya Mahusiano ya Kimataifa na
Diplomasia.
Awali, kabla ya
kubadilishwa kuwa Chuo cha Diplomasia, ilikuwa ni kituo cha harakati za
kupigania uhuru wa Msumbiji. Hivyo, katika harakati za Ukombozi kutoka kwa
wakoloni, wapigania uhuru wa kutoka Msumbiji wakiongozwa na Hayati Eduardo
Mondlane waliweka kambi chuoni hapo na kuanzisha chama cha Ukombozi cha FRELIMO
mnamo mwaka 1962. Mwaka 1970 Hayati Samora Machel alishika madaraka ya kukiongoza
chama hicho baada ya kuuawa kwa Mhe. Mondlane
Ushirikiano wa kiuchumi na
kibiashara
Tanzania na
Msumbiji zimeendelea kushirikiana katika masuala ya kiuchumi na biashara kwa
kuzingatia ujirani na muingiliano mkubwa wa wananchi wa nchi hizi mbili, hususan katika Mikoa ya Ruvuma na Mtwara kwa upande
wa Tanzania, na Majimbo ya Niassa na Cabo Delgado kwa upande wa Msumbiji. Tanzania na Msumbiji zinauziana bidhaa
mbalimbali za kilimo na viwandani.
Kadhalika kuna Makampuni makubwa
kadhaa ya Kitanzania yaliyowekeza mitaji mikubwa nchini Msumbiji. Vile vile, wapo Watanzania wanaomiliki
makampuni ya usafirishaji wa abiria na biashara za kati na ndogo. Ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo
na misingi imara ya kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi hizi
mbili, Tanzania na Msumbiji ziliamua kujenga Daraja la Umoja linaloziunganisha
nchi hizo kwenye mpaka wa Mto Ruvuma ili kuboresha na kuimarisha mahusiano ya
kiuchumi.
Mhe.
Mkapa na Ujumbe wake wanatarajia kuondoka nchini tarehe 24 Julai, 2018 na
kurejea tarehe 26 Julai, 2018.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma.
23 Julai 2018
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.