Monday, January 30, 2017

Balozi wa Indonesia nchini Tanzania aagwa baada ya kumaliza muda wake

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiani wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt.Susan Kolimba, Balozi wa Indonesia Nchini Tanzania Mhe. Zakaria Anshar (kushoto) na Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ramadhani Mwinyi wakijadili jambo kwenye hafla fupi ya kumuaga Balozi wa Indonesia aliyemaliza muda wake wa kuhudumu nchini

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Bibi Justa Nyange (kulia) akifuatilia jambo kwenye hafla hiyo, kushoto ni Mke Balozi wa Indonesia Mhe. Anshar aliyemaliza muda wake wa kuhudumu nchini 
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Mindi Kasiga akifurahia jambo wakati wa hafla hiyo, Kulia na Afisa kutoka Ubalozi wa Indonesia Bw. Nanang Eko K.P.P.

Naibu Waziri Mhe. Dkt. Susan Kolimba akimkabidhi picha ya baadhi vivutio vya kitalii vilivyopo nchini kwa Balozi wa Indonesia Mhe.Anshar na mke wake wakati hafla fupi ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kuhudumu nchini


Picha ya pamoja

Friday, January 27, 2017

India yaadhimisha miaka 68 ya Uhuru kwa kuzindua Jengo jipya la Ubalozi nchini

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 68 ya Uhuru wa India. Maadhimisho hayo yaliyoenda sambamba na ufunguzi wa Jengo la Ubalozi mpya wa India yalifanyika kwenye Jengo hilo lililopo Mtaa wa Shaaban Robert Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Januari,
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Ausralasia, Bibi Justa Nyange wakifuatilia hotuba ya Makamu wa Rais (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya miaka 68 ya Uhuru wa India


Sehemu ya wageni waalikwa wakiwemo Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini wakifuatilia hotuba ya Makamu wa Rais (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya miaka 68 ya Uhuru wa India
Balozi wa India nchini, Mhe. Sandeep Arya nae akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 68 ya Uhuru wa India
Sehemu nyingine ya wageni waalikwa wakisikiliza hotuba ya Balozi wa India (hayupo nchini)

Balozi Baraka Luvanda, Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na Naibu Balozi wa China, Bw. Gou Haudong na Bi. Sun kutoka Ubalozi wa China wakati wa maadhimisho ya miaka 68 ya Uhuru wa China.
Wageni waalikwa
Wanafunzi wakiimba nyimbo za mataifa ya Tanzania na India wakati wa maadhimisho ya miaka 68 ya Uhuru wa India
Kikundi cha Burudani kikitumbuiza wakati wa maadhimisho ya miaka 68 ya Uhuru wa India
Makamu wa Rais, Mhe. Suluhu katika picha ya pamoja
==================================================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

India yaadhimisha miaka 68 ya Uhuru

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan ameipongeza India kwa kuadhimisha miaka 68 ya Uhuru wa nchi hiyo. Pongezi hizo alizitoa jana wakati wa hafla ya kuadhimisha Siku ya Uhuru wa nchi hiyo ambayo ilienda sanjari na ufunguzi wa jengo jipya la Ubalozi lililopo Mtaa wa Shaaban Robert Jijini Dar es Salaam.

Mama Samia Suluhu aliipongeza India kwa hatua kubwa ya maendeleo iliyopata katika nyanja mbalimbali tokea ilipopata uhuru kutoka kwa Mwingereza ambaye pia aliitawala Tanzania.

Makamu wa Rais aliitaja India kuwa sio tu ni rafiki mkubwa wa Tanzania bali ni ndugu wa karibu wanaounganishwa na bahari ya Hindi ambayo imekuwa kiunganishi kikubwa cha wafanyabiashara hata kabla ya uhuru.
Alieleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na India ni wa kuridhisha na umeimarika zaidi kufuatia ziara ya Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi iliyofanyika nchini mwezi Julai 2016. “Wakati wa ziara hiyo mikataba mbalimbali ilisainiwa kati ya nchi hizi mbili ambayo inalenga uedelezaji wa sekta tofauti kwa faida ya pande zote mbili”. 

Mama Samia aliendelea kueleza kuwa ushirika wa Tanzania na India ni wa kimaendeleo ambapo Tanzania imekuwa ikifaidika na misaada mbalimbali ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na msaada wa kuendeleza miundombimu ya maji katika mikoa ya Dar es Salaan na Pwani pamoja na Zanzibar; msaada wa kituo cha TEHAMA katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela mkoani Arusha na uimarishaji wa vyuo vya ufundi.

Mhe. Samia Suluhu alitumia fursa hiyo pia kuishukuru India kwa msaada iliyotoa wa zaidi ya Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko la Kagera lililotokea mwezi Septemba 2016. 

Kwa upande wake, Balozi wa India, Mhe. Sandeep Arya aliridhishwa na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na India na kubainisha kuwa ziara ya Mhe. Modi mwezi Julai 2016 imeboresha na kuimarisha zaidi mahusiano hayo. Aliahidi kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali kama ilivyokuwa inafanya siku za nyuma. 

Alisema mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili ni makubwa na kwamba nchi yake imeisaidia Tanzania katika maeneo mengi ikiwemo mikopo ya masharti nafuu, mafunzo ya muda mfupi na mrefu, mafunzo ya ufundi, ujenzi wa vituo vya TEHAMA, na vifaa vya matibabu. 

Alizungumzia pia mahusiano ya asasi za kiraia za Tanzania na India, ushirikiano katika masuala ya utamaduni, ziara za Watanzania kwenda India kwa ajili ya matibabu na michezo ambapo aliitolea mfano wa ziara ya timu ya Taifa ya Serengeti Boys nchini India mwaka jana. 

Mhe. Balozi alihitimisha hotuba yake kwa kusifu uamuzi wa Tanzania na India kufuta viza kwa watu wenye Hati za Kusafiria za Kidiplomasia na zile za Serikali.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 27 Januari 2017.

Watanzania 14 washiriki maonesho ya Sanaa nchini Kenya

Maonesho ya sanaa za uchoraji ya Wasanii 14 kutoka Tanzania yameanza rasmi tarehe 25 Januari 2017 kwenye ukumbi wa maonesho wa Village Market Nairobi.
Watu waliotembelea maonesho hayo siku ya kwanza ni pamoja na Mabalozi na wadau mbalimbali wa sanaa kutoka Kenya na nchi za nje. Maonesho hayo yatachukua wiki mbili.
Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Bi. Talha Mohamed Waziri (kulia) akimkaribisha Balozi wa Msumbiji kwenye maonesho hayo.

Ofisa wa Ubalozi wa Venezuela Nairobi, Jose Gregorio Ayila Torres (katikati) akibadilishana mawazo na Kaimu Balozi wa Tanzania (kulia). Kushoto ni mmoja wa wasanii wa Tanzania, Raza Mohamed.
Raia wa Uswisi waliofika kwenye maonesho.

Wapenda sanaa wa Kenya wakikagua kazi za wasanii wa Tanzania

Wadau wa sanaa wakifurahia maonesho



Thursday, January 26, 2017

Tanzania na Malawi kufanya Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere, tarehe 26 Januari, 2016. Katika kikao hicho Bi. Mindi alizungumza kuhusu  tuzo za ubunifu zilizotolewa na Umoja wa Afrika (AU) kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mamlaka ya Mapato Tanzania ambazo zilikuwa miongoni mwa taasisi zilizoshindanishwa na kuibuka  washindi.Pia alitumia fursa hiyo kuwaarifu waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika unaoendelea nchini Ethiopia-Addis Ababa na Mkutano wa Tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi unaotarajiwa kufanyika tarehe 3 hadi 5 Februari, 2017.
Kutoka kushoto ni Bw. Felix Tinkasimile Meneja wa Mradi wa Mfumo wa Forodha wa TANCIS, kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Richard Kayombo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka TRA, Bi. Sarah Kibonde kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Bw. David Nghambi kutoka Mamlaka hiyo
Bi. Sarah akizungumza kuhusiana na tuzo iliyotolewa kwa SSRA ambapo alieleza wameshinda Tuzo hiyo katika kipengele cha utunzaji data ambapo wamekuwa wakishirikiana na taasisi za Serikari zinashughulika na umma katika masuala mbalimbali kama Mamlaka ya Vitambulika, Mamlaka ya Mapato na RITA.

Bw. Richard Kayombo akizungumzia tuzo hizo ambapo aliishukuru Wizara ya Mambo ya Nje kwa uratibu  na kutambua umuhimu wa huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato kwa umma katika kuboresha utendaji na kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano.

Bi Mindi  akimkabidhi Bi. Sarah kombe la ushindi kwa niaba ya Wizara. Bi. Kibonde aliipokea zawadi hiyo kwa niaba ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Meneja wa Mradi wa Mfumo wa Forodha wa TANCIS kutoka TRA akipokea zawadi ya cheti cha ushindi kutoka kwa Bi. Mindi Kasiga.

Picha ya pamoja ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje, TRA na SSRA.
Mkutano ukiendelea.
 ==================================================


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Taarifa kuhusu Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi, Tuzo za AU kwa SSRA na TRA na Mkutano wa AU-Addis Ababa

Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi umepangwa kufanyika mjini Lilongwe, Malawi tarehe 03 hadi 05 Febuari 2017. Mkutano huo utawakutanisha viongozi na wataalamu wa sekta mbalimbali kutoka Tanzania na Malawi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine P. Mahiga (Mb),   anategemewa kuongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo. Aidha, Uongozi wa Mkoa wa Mbeya  ambao umekuwa ukishiriki katika vikao vya maandalizi, unategemewa kushiriki katika mkutano huo.

Lengo la mkutano huu ni kujadili na kutathmini hatua zilizofikiwa katika utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano wa Tatu wa JPCC uliofanyika Tanzania, tarehe 24 hadi 30 Juni, 2003.

Miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa kwenye utekelezaji wa makubaliano ya mikutano iliyopita kwa upande wa Tanzania ni pamoja na; Kuanzishwa kwa mradi wa Kituo cha Huduma za Pamoja Mipakani (One Stop Border Post – OSBP)  katika mpaka wa Kasumulu/Songwe ambao umefikia katika hatua nzuri; Idara za Uhamiaji, Polisi na Forodha za nchi zetu mbili zinaendelea kushirikiana katika kutoa huduma na kudhibiti abiria na mizigo katika maeneo ya mpakani.

Pia, Mamlaka ya Bandari Tanzania imeruhusu Mamlaka za Malawi kuwa na maeneo yao katika bandari zetu, kwa ajili ya kuhifadhia mizigo na bidhaa nyingine zinazopitia nchini kabla ya kwenda Malawi. 

Aidha, mkutano huo utatoa fursa kwa nchi zetu mbili kujadiliana na kukubaliana kuhusu maeneo  mapya ya ushirikiano. Miongoni mwa maeneo hayo (kwa upande wa Tanzania) ni pamoja na: Kuanzisha ushirikiano katika sekta ya usafiri wa majini, ambapo mbali na faida za kiuchumi, safari hizo zitaimarisha mwingiliano  wa watu na kupunguza tofauti zilizopo. Kwa hivi sasa Serikali inajenga meli tatu, mbili kwa ajili ya kusafirisha mizigo na moja kwa ajili ya abiria. 

Maeneo mengine ni kuanzisha Mkataba wa ushirikiano katika Sekta ya Usafiri wa Anga (BASA); Kuanzisha mfumo wa kurahisisha ufanyaji biashara kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo hasa katika maeneo ya mpakani; Kuanzisha ushirikiano katika uhifadhi wa mazingira na masuala ya afya ikiwemo magonjwa ya mlipuko hususan maeneo ya mipakani; na Kuanzisha ushirikiano katika sekta ya elimu ya vyuo vikuu na vyuo vingine vya amali.

Tangu kuanzishwa kwa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi nchi hizi mbili zimeshafanya vikao vinne vya Tume hiyo. Kikao cha mwisho kilifanyika hapa Dar es Salaam, Tanzania tarehe 24 hadi 30 Juni, 2003 na kuhudhuriwa na viongozi na wataalam wa sekta mbalimbali kutoka nchi zetu mbili.

Wakati huohuo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga kwa niaba ya Wizara  amekabidhi tuzo kwa wawakilishi wa taasisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Bi. Sarah Kibonde na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Richard Kayombo baada ya kuibuka washindi wa Tuzo zilizotolewa na Umoja wa Afrika (AU). 

Akipokea kombe baada ya  kuibuka mshindi  kwenye kipengele B kuhusu “Innovative Partnership in Service Delivery for its National Social Security Collaborative Database Bridging Project" Bi. Kibonde alisema kuwa ushindi huo ni chachu ya taasisi yao kufanya vizuri zaidi katika kutoa huduma bora kwa wananchi wote kwa ujumla. 

Naye Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Bw. Kayombo ambaye taasisi yake imefanikiwa kushika nafasi ya pili kipengele C kuhusu "Tanzania customs Integrated System" ameushukuru Umoja wa Afrika kwa kuandaa mashindano hayo ambayo ni muhimu katika kujenga uwazi kwenye eneo la ulipaji kodi. 

Pia  ameushukuru Ubalozi wa Tanzania kwa kupokea Tuzo hizo kwa niaba yao na kuishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki kwa kukabidhi ushindi huo kwao.

Katika hatua nyingine, Bi. Kasiga alizungumzia juu ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika (AU Summit) unaotarajiwa kufanyika Jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 30 na 31 Januari, 2017. Mkutano huo umetanguliwa na kikao cha Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu na Maafisa Waandamizi kilichofanyika tarehe 22 hadi 24 Januari, 2017 na kufuatiwa na kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoanza tarehe 25 hadi 27 Januari, 2017.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 26 Januari, 2017