TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China nchini
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China,
Mhe. WANG Yi anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini tarehe 09 Januari 2017.
Mhe. Waziri Wang Yi atapokelewa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga.
Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano
mazuri na ya kihistoria baina ya China na Tanzania ambayo yamedumu kwa zaidi ya
miaka hamsini tangu kuanzishwa kwake pamoja na kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano
wa kiuchumi baina ya Tanzania na China.
Wakati wa ziara hiyo Mhe. Wang Yi atakutana na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa lengo
la kumsalimia.
Aidha, Mhe. Wang Yi atafanya
mazungumzo rasmi na Mhe. Dkt. Mahiga kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano
baina ya Tanzania na China na ushirikiano wa kimataifa.
Itakumbukwa kwamba mwezi Desemba 2015 kwenye Mkutano wa
Wakuu wa Nchi za Afrika na China, China iliichagua Tanzania kuwa miongoni mwa
nchi nne Barani Afrika zitakazowezeshwa kupiga hatua kwenye maendeleo ya
viwanda. Kupitia mpango huo inatarajiwa viwanda takriban 200 vitajengwa au
kuwekezwa nchini kutoka China kabla ya mwaka 2020.
Mpango huu unaenda sambamba na Mpango wa Taifa wa
Maendeleo wa mwaka 2016/2020 na pia ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kujenga Tanzania ya viwanda. Ni
matarajio yetu ni kuwa, Watanzania takriban laki mbili watanufaika na ajira kupitia
mpango huu mahsusi wa kuendeleza viwanda.
Mbali na mpango wa uendelezaji wa viwanda, viongozi
hawa wawili watazungumzia miradi mingine ya miundombinu ambapo China imeahidi
kuisadia Tanzania ikiwa ni pamoja na maboresho makubwa ya Reli ya TAZARA;
Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo pamoja na ujenzi wa Reli ya Kati.
Aidha, Mhe. Wang anatarajiwa kuzungumza na Mwenyeji
wake kuhusu masuala ya ushirikiano wa kimataifa ikiwa ni pamoja na mageuzi ya
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo China inaunga mkono msimamo wa
Afrika na wa Tanzania wa kutaka Afrika ipewe viti viwili vya kudumu kwenye
Baraza hilo na kura ya turufu.
Vilevile viongozi hao watazungumzia masuala ya amani
na usalama katika eneo la Afrika Mashariki pamoja na eneo la Bahari ya Kusini
mwa China.
Mazungumzo hayo yatafuatiwa na
Mkutano wa Mawaziri na Vyombo vya Habari (Joint Press Conference) ambapo
wataeleza makubaliano waliyofikia kwenye mazungumzo yao.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
05 Januari, 2017
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.