Thursday, February 19, 2026
TANZANIA NA MSUMBIJI KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA AFYA
![]() |
| Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit
Kombo (Kulia) akiwa na Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania Mhe. Ricardo Mtumbuida (Kushoto). |
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Msumbiji
zimeeleza dhamira ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa pande mbili katika maeneo
ya kimkakati, ikiwemo Sekta ya Afya ili kuleta maendeleo ya wananchi wake.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Balozi wa Msumbiji
nchini Mhe. Ricardo Mtumbuida, wameeleza dhamira hiyo walipokutana na kufanya
mazungumzo tarehe 18 Februari, 2026 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es
Salaam.
Mazungumzo hayo yalilenga kubainisha
maeneo ya ushirikiano zaidi kati ya nchi hizo mbili kwa lengo la kuongeza
ushirikiano katika Sekta ya afya, kukuza uchumi, na kujadili maandalizi ya
Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja unaotarajiwa kufanyika nchini mwaka huu.
Kwa upande wake Mhe. Balozi Kombo pia
amewakaribisha wananchi wa Msumbiji kunufaika na huduma za Afya za kibingwa na
kibobezi zinazopatikana nchini ikiwa ni sehemu ya kuendeleza mshikamano na
ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Msumbiji.
Naye Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe.
Ricardo Mtumbuida, ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano wa kindugu unaoendelea
kuipatia nchi yake, na kusisitiza azma ya Msumbiji ya kuimarisha uhusiano wa
kidiplomasia na kiuchumi na Tanzania ili kukuza ustawi wa wananchi wa mataifa
yote mawili
![]() |
| Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo |
![]() |
| Balozi wa Msumbiji nchini Mhe. Ricardo Mtumbuida |
|
|
Wednesday, May 28, 2025
BUNGE LAPITISHA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2025/2026
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha kwa kishindo makadirio ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 ya Shilingi 340,538,614,000 ambapo kati ya fedha hizo shilingi 294,998,588,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 45,540,026,000 ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.
Maombi ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara yaliwasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ambapo Bunge limepitisha na kuipongeza Wizara kwa jinsi ilivvyotekeleza majukumu yake kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 na ilivyojipanga kutekeleza majukumu yake ikiwemo Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la Mwaka 2024 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Mhe. Balozi Kombo aliwaeleza Wabunge kuwa Wizara, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 imefanikisha kwa kiasi kikubwa kutekeleza majukumu yake ya msingi ikiwemo kusimamia na kutetea maslahi ya Tanzania nje ya nchi pamoja na kukamilisha mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la Mwaka 2024 iliyozinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 19 Mei 2025.
Mhe. Waziri Kombo amesema kuwa, Sera hiyo pamoja na mambo mengine inaweka msisitizo katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ikiwemo kukuza upatikanaji wa masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi, kutangaza na kuvutia fursa za uwekezaji, utalii, uchumi wa buluu, kuhamasisha ushiriki wa Diaspora katika maendeleo ya Taifa na kutumia Kiswahili kama nyenzo ya diplomasia kwa manufaa ya kiuchumi.
Pia amesema Sera hiyo Sera hii imeweka msingi mpya wa kulinda mila, desturi na utamaduni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo pia alitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa Wizara, Taasisi, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kujumuisha malengo ya Sera ya Mambo ya Nje, Toleo la Mwaka 2024 katika mipango na programu zao.
“Napenda kutoa rai kwa Wizara, Taasisi, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kujumuisha malengo ya Sera ya Mambo ya Nje, Toleo la Mwaka 2024 katika mipango na programu zao kama ilivyoainishwa katika Mkakati wa utekelezaji ili kuwezesha Taifa letu kunufaika ipasavyo, alisisitiza Mhe. Waziri Kombo.
Aidha, Mhe. Waziri Kombo amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani pamoja na kushiriki katika operesheni za kulinda amani kikanda na kimataifa ambapo amesema hadi kufikia Mei, 2025 Tanzania ilikuwa na jumla ya walinda amani 1,890 ikiwa nafasi ya 11 kati ya nchi 119 zinazochangia walinda amani katika misheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa.
Kuhusu Tume za pamoja, Mhe. Waziri Kombo amebainisha kuwa, takribani mikutano Arobaini na Mbili (42) ya Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na nchi mbalimbali , Tume za Pamoja za Ushirikiano (JCC) na mashauriano ya kisiasa kati ya Tanzania na nchi nyingine. Mikutano hiyo imewezesha Serikali yetu kutetea maslahi ya Taifa na nchi hizo katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano kwa manufaa ya Taifa letu.
Akizungumzia masuala ya Diaspora, Mhe. Waziri Kombo amesema Wizara imeendelea kuratibu na kuhamasisha ushiriki wa diaspora katika shughuli za kiuchumi, kielimu na kijamii hapa nchini kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwaunganisha na taasisi mbalimbali nchini ili waweze kupata huduma na bidhaa zinazorahisisha ushiriki wao katika maendeleo ya Taifa ambapo amesema kwa mwaka 2024 diaspora waliwekeza kiasi cha shilingi 7,500,000,000 ikilinganishwa na shilingi 6,400,000,000 mwaka 2023 katika Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa UTT-AMIS.
“Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba 2024 fedha zinazotumwa na Diaspora kuja nyumbani ni shilingi 2,116,188,355,632.06 ukilinganisha na shilingi 2,045,855,200,000 kwa kipindi cha mwaka 2023. Kiasi hicho kina mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya familia zao, kusaidia uwekezaji na kuchangia ukuaji wa sekta ya fedha nchini”alieleza Mhe. Waziri Kombo.
Vile vile, hotuba ya Bajeti ya Mhe. Waziri Kombo imeainisha vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2025/2025 ikiwemo kuendelea kuimarisha uratibu na ushirikiano wa uwili pamoja na ushiriki wa Tanzania katika jumuiya na mashirika ya kikanda na kimataifa ili kulinda maslahi ya taifa; pamoja na kustawisha diplomasia ya kisiasa na kujenga mahusiano ya karibu na nchi washirika.
![]() |
| Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi akijibu hoja mbalimbali za Wabunge wakati wa uwasilishwaji wa Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 |
![]() |
| Sehemu ya wageni waaalikwa wakiwemo Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa waliopo nchini wakifuatilia uwasilishwaji wa Bajeti ya Wizara Bungeni kwa mwaka wa fedha 2025/2026 |
![]() |
| Sehemu nyingine ya wageni waalikwa |
![]() |
| Wageni waalikwa |
![]() |
| Viongozi wa Wizara na wageni waalikwa |
![]() |
| Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara, Balozi Mindi Kasiga akitambulishwa Bungeni |
![]() |
| Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa waliopo nchini wakiwa Bungeni |
Friday, May 16, 2025
TANZANIA NA FINLAND ZAJIDHATITI KUSHIRIKIANA KATIKA BIASHARA NA UWEKEZAJI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.)
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Thabit Kombo (Mb.), amesisitiza dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na Jamhuri ya Finland kwa manufaa ya pande zote.
Msimamo huo ameutoa jijini Dar es Salaam alipozungumza katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Finland, lililowakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi za Tanzania na Finland.
Mhe. Kombo amewahakikishia wawekezaji kutoka Finland kuwa Tanzania imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini na kuongeza kuwa maboresho hayo yanalenga kurahisisha utoaji wa leseni, kupunguza urasimu na kuboresha mifumo ya forodha ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa wawekezaji.
Amebainisha kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na kuhudumia wawekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Waziri Kombo ametaja teknolojia ya habari na mawasiliano, afya, dawa, na teknolojia za kilimo kuwa ni miongoni mwa sekta zenye fursa kubwa za uwekezaji na ushirikiano.
Amesema Tanzania haitaki kuwa soko tu la bidhaa kutoka Finland, bali inataka kuwa mshirika wa muda mrefu na wa kuaminika katika biashara na uwekezaji.
Aidha, amewahimiza wafanyabiashara wa Kitanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika soko la Finland na kubainisha kuwa Finland inathamini ubora, uendelevu na uwazi ambapo bidhaa za asili kutoka Tanzania zina uwezo wa kuvifikia na hivyo kuimarisha biashara kati ya nchi hizo.
Naye Rais wa Jamhuri ya Finland, Mheshimiwa Alexander Stubb, amepongeza jitihada za Tanzania za kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuelezea kuwa Finland iko tayari kushirikiana bega kwa bega na Tanzania katika maeneo ya Elimu na Ufundi, nishati, afya, kilimo na mazingira kwa manufaa ya pamoja.
Mheshimiwa Rais Stubb amesisitiza kuwa Finland inaiona Tanzania kama lango muhimu kuelekea masoko ya Afrika Mashariki.
Rais wa Finland yupo nchini kwa ziara ya kitaifa na ameambatana na ujumbe wa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Finland.
Rais wa Jamhuri ya Finland, Mheshimiwa Alexander Stubb
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.)
Rais wa Jamhuri ya Finland, Mheshimiwa Alexander Stubb
Rais wa Jamhuri ya Finland, Mheshimiwa Alexander Stubb
Naibu Waziri wa Biashara za Kimataifa wa Finland, Mhe. Jarno Syrjälä.
Mkurugenzi idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga.









.jpeg)




























