Wednesday, January 31, 2024

BALOZI MBAROUK APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO KUTOKA KWA BALOZI MTEULE WA BURUNDI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Leontine Nzeyimana.

Akipokea Nakala hizo Mhe. Mabarouk amemuhakikishia Mhe. Nzeyimana ushirikiano wa dhati utakaomwezesha kuitumikia Burundi kwa tija katika muda wake wa uwakilishi hapa nchini.

Vilevile, alieleza kuwa Tanzania na Burundi licha ya kuwa na ushirikiano wa ujirani pia ni ndugu kufuatia mwingiliano wa wananchi wa Nchi hizi mbili hususan kwenye masuala ya biashara.

“Tanzania itaendelea kuweka mikakati imara ya kukuza ushirikiano wa kibiashara sambamba na kusimamia ujenzi wa miundombinu inayounganisha nchi hizo ili kurahisisha shughuli za usafirishaji”. Mhe. Balozi Mbarouk

Naye Balozi Mteule, Mhe. Leontine Nzeyimana alishukuru kwa mapokezi mazuri aliyopata tangu alipowasili nchini na kwamba ana matumaini makubwa ya kupata ushirikiano utakaomwezesha kutekeleza majukumu yake ya uwakilishi kikamilifu.

Viongozi hao pia wamekubaliana kuendelea kuratibu utekelezaji wa makubaliano yaliyoafikiwa na Nchi zao kupitia Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ili kuleta tija kwa pande zote.

Pamoja na mambo mengine, kupitia ziara ya Rais wa Jamhuri ya Burundi nchini, Mhe. Evaristi Ndayishimye Tanzania ilikabidhi eneo la bandari kavu katika eneo la Kwala mkoani Pwani ili kukuza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo.

Asilimia 95 ya mizigo ya Burundi husafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam hivyo, bandari kavu ni chachu kubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akisalimiana na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania Mhe. Leontine Nzeyimana katika Ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania Mhe. Leontine Nzeyimana katika Ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania Mhe. Leontine Nzeyimana wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma
Picha ya pamoja

WAZIRI MAKAMBA ANADI FURSA ZA BIASHARA, UWEKEZAJI ITALIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amenadi fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana nchini katika mkutano wa wafanyabiashara, viongozi wa siasa na wa kijamii nchini Italia.

Katika mkutano huo, Waziri Makamba amewaeleza wafanyabiashara na wawekezaji wa Italia fursa mbalimbali za biashara zinazopatikana nchini  pamoja na mageuzi makubwa ya kuboresha mazingira ya uwekezaji yanayofanyika chini ya Uongozi imara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Makamba amesema mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ni salama na rafiki kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ili kuhakikisha wafanyabiashara wanatekeleza majukumu yao katika mazingira rafiki na salama. 

Kadhalika Waziri Makamba amesema kuwa Tanzania inazingatia misingi ya utawala bora pamoja na kuzungukwa na nchi saba ambazo hazina bandari na hivyo kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma kwenda katika nchi hizo.

Waziri Makamba ameongeza kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ya Tanzania ni salama kwa sababu Tanzania imeridhia sheria na mikataba ya kimataifa inayolinda mitaji na uwekezaji wa kigeni pamoja na Serikali kutambua sekta binafsi kama injini ya maendeleo ya kiuchumi.

“Napenda kuwasihi wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Italia kuja kuwekeza Tanzania kwani licha ya kuwa na mzingira salama, pia kuna fursa za kuwekeza katika sekta mbalimbali kama nishati, utalii, kilimo, afya na elimu,” alisema Waziri Makamba.

Kadhalika, Waziri Makamba ameongeza kuwa kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa Soko Huru la pamoja la Afrika (AfCFTA) ambalo linahusisha watu zaidi ya bilioni 1.5 hali ambayo itawezesha wafanyabiashara wa Italia kuwafikia watu hao kupitia soko hilo.

Waziri Makamba amesema kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Italia katika kutekeleza Mpango wa Mattei kwa maslahi ya pande zote mbili, na kuwasisitiza kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji nchini Tanzania na visiwani Zanzibar. 

Akiongea awali katika mkutano huo, Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari amesema kuwa utekelezaji wa mpango wa Mattei utakapoanza utazingatia maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa na wadau ambapo miradi ya kipaumbele kwa nchi nane za awali za Afrika ikiwemo Tanzania. 

Tanzania ni moja kati ya nchi nane za Afrika zitakazopewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan) ambapo kiasi cha  Euro bilioni 5 za awali kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiteta jambo na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari katika ofisi za chama hicho, Jijini Roma Italia



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na  wafanyabiashara, viongozi wa siasa na wa kijamii nchini Italia



Tuesday, January 30, 2024

TANZANIA YASISITIZA MPANGO WA MATTEI UZINGATIE MAHITAJI STAHIKI YA AFRIKA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Mhe. January Makamba (Mb.) ambaye anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia amesisitiza umuhimu wa mpango wa Mattei kuzingatia mahitaji sahihi ya Afrika ili uweze kuleta matokeo stahiki barani Afrika.

Mheshimiwa Makamba alieleza kuwa mpango huo ukizingatia mahitaji stahiki ya Afrika changamoto nyingi zinazokabili nchi zilizoendelea zinazosababishwa na ukosefu wa maendeleo barani Afrika zitaondoka.

Awali akihutubia katika mkutano wa Nne wa Italia-Afrika, Waziri Mkuu wa Italia, Mhe. Giorgia Meloni amesema mpango wa Mattei utagusa masuala ya usalama wa nishati na matumizi ya nishati mbadala, maendeleo ya miundombinu, usalama wa chakula, elimu na mafunzo ya ufundi pamoja na kupambana na wahamiaji haramu, ameeleza 

Serikali ya Italia inatarajia kushiriki kwa kiasi kikubwa kukuza maendeleo barani Afrika kwa kupitia Mpango wake Mpya wa Mattei.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat ameomba Afrika ipewe muda wa kuchanganua Mpango wa Mattei kwanza kabla ya kuanza utekelezaji wa mpango huo.

"Tunahitaji kubadilisha maneno kuwa vitendo kwa sababu ni vyema tukajadiliana na kuona ni njia gani zinatumika kutekeleza miradi inayopendekezwa katika Mpango wa Mattei ili kuepuka kuwa na furaha na ahadi ambazo hazitekelezwi,” amesema Mahamat.

Viongozi wakuu wa baadhi ya nchi za Afrika; mawaziri, maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa, wawakilishi kutoka taasisi na mashirika ya kimataifa wafanyabiashara pamoja na mashirika ya kifedha wameshiriki mkutano huo unaoendelea Roma, Italia.

Waziri Mkuu wa Italia, Mhe. Giorgia Meloni akihutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akishiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia. Katika Mkutano huo, Mhe. Makamba anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Viongozi mbalimbali walioshriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia wakiwa katika picha ya pamoja







Monday, January 29, 2024

TANZANIA KUNUFAIKA NA MIRADI YA MPANGO WA MATTEI

Tanzania imechaguliwa kuwa moja ya nchi nane za Afrika zitakazopewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan) ambapo kiasi cha  Euro bilioni 5 za awali kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Miradi hiyo ya kipaumbele kupitia Mpango mpya wa Kimkakati wa Mattei (Mattei plan) ipo katika sekta ya nishati, elimu na kilimo.

Taarifa hiyo imetolewa na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) pembezoni mwa Mkutano wa Nne wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia unaendelea Roma, Italia.  

Mhandisi Cestari alieleza kuwa utekelezaji wa mpango huo utaanza mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika na Italia, ambapo Serikali ya nchi hiyo itafadhili miradi ya kipaumbele kwa nchi nane za awali za Afrika. Hatua hiyo itahusisha pia kugharamia gharama za upembuzi yakinifu ya miradi itakayopendekezwa. 

Kama hatua ya utekelezaji ya mpango huo, ujumbe wa wataalam kutoka Chemba ya Biashara ya Italia ikiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Mhe. Dkt. Edmondo Cirielli unatarajiwa kuwasili nchini Tanzania ndani ya mwezi mmoja kwa ajili ya kukutana na timu ya wataalam ya upande wa Tanzania kwa ajili ya kukamilisha hatua za awali za utiaji saini wa ushirikiano huo wa pande mbili utakaohusisha utekelezaji wa miradi itakayopitishwa na pande mbili. 

“Serikali ya Italia imetenga kiasi cha Euro bilioni 5 za awali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo katika nchi nane za kipaumbele za Afrika ikiwemo Tanzania,” alisema Mhandisi Cestari. 

Kwa Upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba ameipongeza Serikali ya Italia kwa kuonesha nia ya kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika kupitia Mpango mpya wa Kimkakati wa Mattei (Mattei plan) ambapo sekta ya nishati, elimu na kilimo zimepewa kipaumbele. 

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo umelenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji baina ya mataifa hayo mawili kupitia mpango mpya wa Mattei, (Mattei Plan).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na Ujumbe wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italian ukiongozwa na Rais wa Chama hicho, Mhandisi Alfredo Cestari pamoja na  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Mhe. Dkt. Edmondo Cirielli




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari 































Sunday, January 28, 2024

WAZIRI MAKAMBA ATETA NA MKURUGENZI MKUU IOM

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amekutana  kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji (IOM) Bi. Amy Pope jijini Roma, Italia.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Makamba ameipongeza IOM kwa kazi inazofanya nchini katika masuala ya Uhamiaji na amemuhakikishia Bi. Pope kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kufanya kazi na Shirika hilo kwa ukaribu zaidi.

Mhe. Waziri Makamba amesema Shirika hilo limekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala ya wakimbizi, majanga ya asili na kwamba ni matumaini yake kuwa Tanzania na IOM zitaendelea kushirikiana kwa manufaa ya pande zote mbili.

Waziri Makamba ameipongeza IOM kwa kuendelea na zoezi la kuwarejesha nyumbani raia wa Ethiopia waliokuwa katika magereza mbalimbali nchini na kuongeza kuwa kitendo hicho kimesaidia Tanzania kukabiliana na changamoto ya msongamano wa watu katika magereza yake.

Kwa upande wake, Bi. Pope ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa jinsi inavyoshirikiana na Shirika la IOM katika kutekeleza majukumu yake na kuahidi kuwa na mpango maalum wa kuendeleza ushirikiano  na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha majukumu yake. Aliongeza kuwa Shirika hilo litahakikisha kuwa wahamiaji wanapata haki zao za msingi na kuwa katika mazingira salama nchini.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji (IOM) Bi. Amy Pope jijini Roma, Italia

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akimfafanulia jambo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji (IOM) Bi. Amy Pope Jijini Roma, Italia

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji (IOM) Bi. Amy Pope akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba walipokutana kwa mazungumzo Jijini Roma, Italia

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji (IOM) Bi. Amy Pope Jijini Roma, Italia

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji (IOM) Bi. Amy Pope baada ya kumaliza kikao chao Jijini Roma, Italia


Saturday, January 27, 2024

TANZANIA, SUDAN KUSINI KUIMARISHA SEKTA ZA KIMKAKATI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Sudan Kusini zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati hususan biashara, utalii, utamaduni na kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa maslahi ya pande zote mbili.

Ahadi hiyo imeafikiwa wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini Mhe. James Morgan Jijini Roma, Italia leo tarehe 27 Januari 2024.

Waziri Makamba amesema kuwa ushirikiano wa sekta za kimkakati baina ya Tanzania na Sudan Kusini utasaidia mataifa hayo mawili kukuza na kuimarisha uchumi wake kupitia sekta za biashara, utalii, utamaduni pamoja na kubidhaisha lugha ya Kiswahili.

Viongozi hao wamekubaliana kuanzisha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC), kuimarisha masuala ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na ulinzi na usalama na kuendeleza ushirikiano wa kihistoria baina ya mataifa hayo uliodumu kwa muda mrefu. 

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini, Mhe. James Morgan amesema ushirikiano wa Sudan Kusini na Tanzania ni wa kihistoria kwani Tanzania na Sudan Kusini siyo tu majirani bali ni ndugu. 

Kadhalika, Mhe. Morgan amesema Sudan Kusini itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuendeleza sekta ya bishara hususan biashara ya mazao ya chakula kama vile mahindi.

Mhe. Morgan aliongeza Sudan Kusini itaendela kuimarisha na kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta ya biashara, utalii, utamaduni pamoja na kuendelea kukitangaza Kiswahili nchini humo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini Mhe. James Morgan Jijini Roma, Italia leo tarehe 27 Januari 2024

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini Mhe. James Morgan Jijini Roma, Italia leo tarehe 27 Januari 2024

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini Mhe. James Morgan akifafanua jambo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba walipokutana kwa mazungumzo  Jijini Roma, Italia tarehe 27 Januari 2024



Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini Mhe. James Morgan kikiendelea Jijini Roma, Italia tarehe 27 Januari 2024





 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini Mhe. James Morgan akisalimiana na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme Jijini Roma, Italia tarehe 27 Januari 2024




WAZIRI MAKAMBA KUMWAKILISHA MHE. RAIS SAMIA KATIKA MKUTANO WA NNE WA WAKUU WA NCHI WA AFRIKA NA ITALIA





Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akipokelewa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Leonardo Da Vinci, Roma Italia.




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akiteta jambo na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Leonardo Da Vinci, Roma Italia.



Friday, January 26, 2024

RAIS SAMIA ATEMBELEA KIWANDA CHA INDESSO CHA JAKARTA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan akiangalia baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na uchakataji wa majani ya karafuu alipotembelea Makao Makuu ya Kiwanda hicho jijini Jakarta. Kiwanda hicho kinachakata majani ya karafuu na kutengeneza mafuta kwa ajili ya matumizi mbalimbali na kimewekeza kisiwani Pemba.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan na ujumbe wake wakisikiliza maelezo ya jinsi kiwanda cha INDESSO kinavyoendesha shughuli zake walipotembelea Makao Makuu ya Kiwanda hicho jijini Jakarta .

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan na ujumbe wake wakisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Indesso, Bw. Robby Gunawan (hayupo pichani) walipotembelea Makao Makuu ya Kiwanda hicho jijini Jakarta

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan na ujumbe wake wakiwa katika kigari maalum walipotembelea Makao Makuu ya Kiwanda cha INDESSO kinachochakata majani ya karafuu na kutengeneza mafuta kwa ajili ya matumizi mbalimbali.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan na ujumbe wake katika picha ya pamoja na uongozi wa Kiwanda cha INDESSO alipotembelea Makao Makuu ya Kiwanda hicho kinachochakata majani ya karafuu na kutengeneza mafuta kwa ajili ya matumizi mbalimbali.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ametembelea Makao Makuu ya Kiwanda cha INDESSO kinachochakata majani ya karafuu na kutengeneza mafuta kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Katika ziara hiyo kwenye kiwanda cha INDESSO ambacho kimewekeza kisiwani Pemba, Mhe. Rais Samia alijionea mchakato mzima wa uchakataji majani ya Karafuu na kutengeneza mafuta kupitia vinu vitano vilivyopo kwenye kiwanda hicho.

Akizungumza mbele ya Mhe. Rais Samia, Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Indesso, Bw. Robby Gunawan alisema Indesso inajivunia mafanikio mbalimbali iliyofikia ikiwemo kuwa kichocheo cha mabadiliko katika tasnia ya karafuu ya Tanzania".

"Kwa kuwekeza katika eneo hili, hatujafungua tu fursa za ukuaji wa kiuchumi bali pia tunachangia katika maendeleo endelevu ya jamii za wenyeji," alisema.

Aliongeza kuwa biashara ya kuchemsha mafuta ya majani ya karafuu bado iko katika hatua za awali za maendeleo nchini Tanzania na inaweza kuwa njia ya kusukuma ukuaji wa kiuchumi na maendeleo vijijini.

Alisema Indesso ina matumaini kuwa mipango yao itakuwa kichocheo, kuhamasisha watu kuanzisha vituo zaidi vya kuchemsha mafuta ya karafuu ndani ya Tanzania.

Katika ziara hiyo, Mhe. Rais aliambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar Mhe. Mudrick Ramadhan Soragha, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Mhe. Makocha Tembele na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jat Miko.

Mhe. Rais Dkt. Samia na ujumbe wake wameondoka Indonesia kurejea nchini baada ya kumaliza ziara ya kitaifa ya siku tatu iliyofanyika nchini humo kuanzia tarehe 24-26 Januari, 2024.

Thursday, January 25, 2024

RAIS SAMIA ATETA NA WANAWAKE VIONGOZI JIJINI JAKARTA

 





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekutana na kuzungumza na wanawake viongozi wanaojihusisha na biashara, uwekezaji na utumishi wa umma jijini Jakarta.

Akizungumza katika kikao na wanawake hao viongozi, Mhe. Rais Samia amewatia moyo na kuwatakaa waendelee na jitihada na harakati za kujikwamua kiuchumi ili kuhakikisha wanatimiza ndoto zao za kuleta maendeleo ya kweli kwao binafsi na nchi zao kwa ujumla.

Mhe. Rais Samia yuko nchini Indonesia kwa Ziara ya Kitaifa ya Siku Tatu iliyoanza tarehe 24- 26 Januari, 2024 kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake Rais wa jamhuri ya Indonesia Mhe. Joko Widodo.