Thursday, January 25, 2024

RAIS DKT. SAMIA APOKELEWA RASMI INDONESIA, HATI SABA ZASAINIWA












Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Samia Suluhu Hassan amepokelewa rasmi katika Ikulu ya Bogor jijini Jakarta na mwenyeji wake Mhe. Joko Widodo baada ya kuwasili nchini Indonesia kwa ziara ya siku tatu ya Kitaifa iliyoanza tarehe 24 hadi 26 Januari, 2024.

Akipokelewa katika Ikulu ya Bogor na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Indonesia Mhe. Joko Widodo,  Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alikagua gwaride maalum lililoandaliwa kwa heshima yake na kupigiwa mizinga 21.

Baada ya tukio hilo Mhe. Rais Samia na mwenyeji wake walielekea sehemu iliyoandaliwa katika viwanja vya Ikulu ya Bogor jijini Jakarta kwa ajili ya kupanda mti wa kumbukumbu ya ziara yake nchini humo.

Rais Samia Suluhu Hassan na mwenyeji wake Mhe. Joko Widodo walipata wasaa wa kuzungumza katika Ikulu hiyo na baadaye walizungumza na Waandishi wa Habari kuelezea mazungumzo yao kwa ufupi na mambo waliyokubaliana kuyatekeleza.

Ziara hiyo ya kitaifa imeshuhudia Indonesia na Tanzania zikisaini Hati SABA za makubaliano na barua ya kusudio moja. Hati hizo ni Makubaliano Kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Indonesia kuhusu Ushirikiano katika Nyanja ya Uchumi wa Buluu. Hati hii ina lengo la kukuza biashara zitokanazo na shughuli za majini kama kuwezesha masoko ya samaki.

Hati ya pili ni Makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Indonesia kuhusu Ushirikiano katika Sekta ya Kilimo. Hati hii inalengo la kuongeza uwezo wa Taasisi za Kilimo hivyo kuimarisha ushirikiano  katika kutengeneza masoko ya bidhaa za kilimo.

Hati ya tatu ni Makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Indonesia kuhusu Ushirikiano katika Sekta ya Madini. Hati hii ina lengo la kuwezesha tafiti za madini na uchakataji wa uongezaji thamani ya madini ya vito.

Hati ya nne ni Makubaliano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje Indonesia kuhusu Ushirikiano wa Kujengeana Uwezo katika Masuala ya Kidiplomasia. Hati hii inatarajiwa kutekelezwa kupitia Vyuo vya Diplomasia vya nchi mbili hizi ikiwa na lengo la kuanzisha ushirikiano katika masuala ya Utafiti na kitaaluma, kubadilishana utaalamu katika mafunzo ya kidiplomasia na utafiti katika nyanja za uhusiano wa kimataifa na lugha.

Pia Barua ya Kusudio kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Indonesia kuhusu kukuza na kuwezesha Uwekezaji. 

 
Barua hiyo ina lengo la kuweka mazingira mazuri ya kiuwekezaji baina ya nchi mbili ili kuongeza kiwanjo cha uwekezaji kati ya Tanznaia na Indonesia. Barua hiyo imesainiwa kama sehemu ya kuonesha nia ya Serikali za nchi hizi mbili kuingia katika mkataba wa kukuza na kulinda Uwekezaji.

Mhe. Rais Samia yuko nchini Indonesia kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 24-26 Januari 2024 kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake Rais wa Indonesia Mhe. Joko Widodo ambaye alitembelea Tanzania mwezi Agosti,2023.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.